Sarah Mossi na Is-haka Omar, Zanzibar
HOFU imetawala visiwani Zanzibar huku vyombo vya ulinzi na usalama vikidaiwa kuwakamata watu na kuwapeleka kusikojulikana.
Vitendo hivyo vinadaiwa kufanywa na viongozi waandamizi wa Serikali na chama tawala na baadhi yao wanadaiwa kuwa ndiyo wamekuwa wakiendesha kampeni ya kupinga Serikali ya Umoja wa Taifa Visiwani humo.
Akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Kibanda Maiti mjini Unguja, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yanayomkuta aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mansour Himid Yussuf hayana tofauti na kilichomkuta yeye baada ya kufukuzwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema msimamo wake ndani na nje ya Serikali ya Zanzibar ulimfanya afukuzwe na hata kuwekwa kizuizini kwa tuhuma za uhaini kama anavyofanyiwa Mansour hivi sasa.
Seif alisema Mansour anapita katika njia alizopitishwa yeye katika siasa na kusisitiza kwa kufanya hivyo hawamkomoi bali wanamkomaza katika masuala ya siasa.
“Atakapotoka gerezani atakuja kusimamia mamlaka ya Zanzibar ipasavyo, wanachofanya ni sawa na chuma kukipitisha kwenye moto kinazidi kuwa imara.
“Kilichomkuta Mansour siwezi kuamini alikamatwa kwa kuwa ametoka ndani ya CCM, bali kakamatwa kwa kutetea mamlaka kamili ya Zanzibar,” alisema Maalim Seif.
Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema Mahakama Kuu ya Zanzibar itatenda haki kwa mujibu wa sheria kwa vile tuhuma dhidi ya Mansour kuwa ni za kuonewa.
Kwa mujibu wa Maalim Seif, anaamini uonevu anaopitia Mansour unafungamana na itikadi za siasa na kusisitiza waliofanya hivyo watambue yaliyomkuta yanaweza kumkuta mtu yeyote.
“Wewe uwe ni waziri au nani yanaweza kukupata. Mbona alifungwa Nabii Yussuf jela na baadaye akaja kuwa Mfalme wa Misri, mimi nimefungwa na kuteswa lakini leo hii mimi ni Makamu wa Rais.
“Hii ni nyota njema kwa Mansour katika kutetea masilahi ya Wazanzibari, anachofanya ni ukombozi na kinakubalika kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika kutetea haki za wananchi wa Zanzibar,” alisema.
Alisema kuna njama zinafanywa na kikundi cha watu saba wanaofanya mikakati ya kumkwamisha Mansour katika siasa na kusisitiza kundi hilo linaendeshwa na chama kimoja.
“Siasa za chuki zimepitwa na wakati, kuna haja kila chama kujenga hoja; hoja za CUF za Serikali mbili ni kero kwa wananchi tunaamini Serikali tatu zitaleta ukombozi kwa wananchi.
‘Miongoni mwa hoja za msingi ni kwamba Zanzibar itambulike kwa sababu thamani ya Rais wa Zanzibar mwisho wake ni Chumbe,” alisisitiza Maalim.
Mansour ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Ujenzi na Nishati, pia aliwahi kuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar katika utawala wa Dk. Amani Karume. Yuko kizuizini kwa tuhuma za kukutwa na silaha na risasi kinyume na sheria ya Zanzibar.
Kutokana na misukosuko iliyompata Mansour katika siasa, Seif alimfananisha na kadhia aliyopitia baada ya kufukuzwa uanachama wa CCM mwaka 1987 kwa madai ya kukisaliti chama hicho na baadaye mwaka 1989 aliwekwa kizuizini kwa kukutwa na nyaraka za siri za Serikali.
Mwishoni mwa mwaka 1991, Seif alitolewa kizuizini baada ya kutopatikana na hatia ya kosa hilo lakini kwa sharti la kutohutubia mkutano wowote wa hadhara katika ardhi ya Tanzania.
Jussa, Riyami waibua mpya
Nao wajumbe wa iliyokuwa Kamati ya Maridhiano, Ismail Jussa Ladhu na Eddie Riyami wakizungumzia suala la Mansour wamewataka viongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kuacha kuchukua watu usiku na kuwapeleka wanakotaka wao.
Wajumbe hao walitoa tamko hilo jana kwa niaba ya Mwenyekiti wao, Hassan Nassor Moyo, baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo.
Wa kwanza alikuwa ni Eddy Riyami ambaye alikuwa mjumbe wa tume akiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM). Yeye aliishutumu Serikali ya Umoja wa Taifa akidai inabeba watu usiku na kuwapeleka kusikojulikana pamoja na kuchukua simu zao za mkononi.
“Tunamuomba Maalim na Makamu wake, Serikali yao inabeba watu inawapeleka wanakotaka, inachukua simu zao, tunasema wakome, lakini tunawataka pia Lukuvi na Wassira wakome kukaa Dodoma kuizungumzia Zanzibar.
“Hatuko tayari pia kuona Bunge linakwenda hivi linavyokwenda, tunataka Serikali ya Zanzibar iliyo na meno na si hivi tena meno yanayotafuna si kibogoyo, ili mwakani tuiondoshe Serikali hii dhalimu,” alisema Riyami.
Katibu wa Kamati ya Maridhiano, Ismail Jussa Ladhu, alisema yanayofanyika sasa yametokana na mipango inayofanywa na kundi la watu saba linalojaribu kuvuruga maridhiano.
“Hawa wana shaka na kurudi kwenye majimbo yao mwakani, mmoja wao kafika mbali eti anapanga ‘time’ agombee urais 2015, tunawapa salamu hakuna hata moja watakalopanga tusilijue.
“Watatukamata wote lakini hawamuondoi mtu katika suala la maridhiano, lakini pia wajue hakuna mtu watakayemkasirisha ili aingie barabarani, wananchi waambieni tunasikiliza viongozi wetu,” alisema Jussa.
Jussa aliwatoa hofu wanachama na kusema kazi ya kuhakikisha Mansour anakuwa nje inafanywa kwa kushirikiana na mawakili mashuhuri nchini.
Katika mkutano huo, Jussa pia aligusia suala la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katika kutoka CUF na kusema hakuna mjumbe wa CUF anayehudhuria vikao hivyo.
“Wanajisahau waacheni wenyewe hakuna Katiba bila UKAWA kurudi bungeni, mara hii wamekwama, mtarimbo umenasa,” alisema Jussa huku akishangiliwa.