27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge la Katiba: Mjumbe ataka atumiwe tiketi ya ndege Marekani

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Bw, Deus Kibamba
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania Bw, Deus Kibamba

Na Fredy Azzah, Dodoma

MWENYEKITI wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, amesema mmoja wa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hadi sasa hajahudhuria vikao vya Bunge hilo kwa vile aliteuliwa akiwa Marekani.

Amesema mjumbe huyo pia amekuwa akiitaka Ofisi ya Bunge la Katiba imtumie tiketi ya ndege aweze kuhudhuria vikao hivyo vinavyoendelea mjini Dodoma.

Kibamba akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, alisema tathmini ya wiki moja tangu kuanza tena kwa Bunge hilo imebaini wajumbe wengi kutoka CCM na UKAWA hawajahudhuria vikao hivyo.

Alisema kitendo cha Bunge hilo kuendelea na vikao kwa kuwa na wajumbe wachache hakiwezi kulipatia Taifa Katiba Mpya iliyoridhiwa na pande zote za jamii.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Katiba Tanzania alipotakiwa na waandishi wa habari kutaja jina la mjumbe huyo, aligoma akisema wanaotakiwa kutoa taarifa na hata kutaja jina ni ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba.

“Huyu mjumbe alivyoteuliwa alitaka alipiwe tiketi ya ndege kutoka Marekani afike Dar es Salaam ale bata kidogo ndiyo aje Dodoma, Bunge Maalumu likakataa.

“Kwa hiyo tunasisitiza kuwa bado tunataka ufafanuzi wa idadi ya wajumbe wa Bunge hili hasa wale 201 na taarifa zao.

“Wapo watu walioteuliwa kwa tiketi ya wakulima na mpo nao nyie (waandishi wa habari), tunataka tuambiwe hawa wanalima wapi. Wapo walioteuliwa kuwawakilisha waganga wa kienyeji, tuambiwe tu hata huo ulinzi wao kwa hao waganga ulianza lini,” alisema na kuhoji.

Mbali na suala hilo, Kibamba alizungumzia gharama za Bunge hilo na kusema baada ya kujiongezea siku kupitia marekebisho ya kanuni, kwa sasa litatumia Sh bilioni 40 hadi mwisho wa mkutano wa sasa.

Alisema gharama hizo ni pamoja na Sh bilioni 10 zilizotumika kwenye awamu ya kwanza ya Bunge hilo.

“Baada ya kubadilisha kanuni wamejiongezea fursa ya posho. Rais alisema ameongeza siku 60 na zisipotosha basi lakini baada ya kuondoa siku za Jumamosi na sikukuu, siku za wajumbe hao kukaa Dodoma sasa zitakuwa ni kati ya 84 ama 90 kutegemea na sikukuu zitakazokuwapo.

“Hii ni kujiongezea nafasi za posho kwa sababu kila siku watakapokuwa hapa watakuwa wanalipwa,” alisema Kibamba.

Alisema kanuni hizo zililenga kuhakikisha mchakato huo unawabana watu ambao hawahudhurii lakini haziwagusi mawaziri na manaibu wao.

“Wao hawa wanatakiwa tu wamwambie Waziri Mkuu kuwa wanaenda kutembelea vivuko, wapo wanaotumia nafasi hiyo kwenda kupitapita kwenye majimbo yao.

“Ndiyo maana tunasema mchakato huu uahirishwe mpaka mwaka 2016, itakuwa hawa hawapitipiti tena majimboni kwa sababu wakati huo hata wakipigiwa simu wanaangalia mara mbilimbili kabla ya kuzipokea,” alisema.

Akizungumzia kauli ya Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta ya kutaka vyombo vya habari vidhibitiwe, alisema ilijikita katika kuingilia uhuru wa maoni na kubana vyombo vya habari.

“Alitakiwa apongeze vyombo vya habari na badala yake akataka vishughulikiwe, ukisema vishughulikiwe unakuwa na maana mbaya; unaweza kushughulikiwa hata kwa kuuawa.

“Kuminyaminya vyombo vya habari ni kubana uhuru na kuvunja Katiba hii ya mwaka 1977. Huyu mwenyekiti ni mtu ambaye alikuwa anafikiriwa kwa mambo makubwa kabla ya hapo na ni mwanasheria aliyebobea,” alisema.

Alisema pia kuwa Katiba ni suala linalohitaji unyenyekevu na siyo kutumia nguvu.

“Hata wakulima na wafugaji ambao wanapigana sasa, hili Bunge ndiyo lilitakiwa kuwa sehemu ya kuanzia kuwasuluhisha lakini kwa sasa hali imekuwa tofauti,” alisema.

Kibamba alizungumzia pia mpasuko ndani ya CCM na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema ni sababu nyingine inayoonyesha umuhimu wa kusimamishwa shughuli za Bunge hilo.

Alieleza mchakato ulivyo sasa hata ndani ya CCM kuna mpasuko kwa sababu yapo makundi matatu na kila moja lina masilahi yake.

“Hata UKAWA hawapo pamoja, wangekuwa pamoja kusingekuwa na wengine hapa,” alisema.

Alisema vyama hivyo vimekuwa na dhana ya kushughulikia watu wenye mitizamo tofauti suala alilosema siyo zuri kwenye uandikaji wa Katiba.

Alisema kwa sasa Bunge la Katiba halina ukomo, ni vema rais akaliahirisha mpaka wakati mwingine na litakaporejea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ibadilishwe na Tume ya Jaji Warioba itambulike kuwa ni washauri wakubwa wa Bunge hilo.

Kibamba pia alizungumzia hatua za usuluhishi zinazoendelea kwa kueleza kuwa baada ya msajili wa vyama aliyetumwa na Rais kuelekea kushindwa, sasa Rais Jakaya Kikwete ameonyesha dalili za kukutana na pande hizo.

Alisema ni lazima afikirie pia kuahirisha Bunge hilo kwa vile hata kama Katiba itapatikana kwa mwendo huu haiwezi kutumika mwaka 2015.

Alisema Tume ya Uchaguzi imesema kuwa hata Katiba ikipatikana sasa, mchakato wa kura za maoni hauwezi kufanyika kabla ya Machi mwakani.

Kauli ya Bunge

Akizungumzia madai ya mjumbe ambaye aligoma kuhudhuria vikao hivyo kutoka nchini Marekani, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad, alisema hana taarifa za mjumbe ambaye hajawasili kwenye Bunge hilo tangu lilipofunguliwa.

Alisema anachofahamu ni taarifa za mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo ambaye anawakilisha Watanzania waishio nje ya nchi ambaye amekuwa akihudhuria tangu vilipoanza vikao vya Bunge hilo.

“Najua kuna mjumbe mmoja anatoka kwenye Diaspora na huyu tayari yupo na jana (juzi) nilikuwa naye alikuwa na suala lake la uraia pacha (uraia wa nchi mbili) na alikuwa na document (nyaraka) alitaka kuzigawa kwa wajumbe kutokana na suala hilo na nilimruhusu.

“Huyu yupo na ameleta hata tiketi yake na nimewasiliana na mwenyekiti na viongozi wengine kuona jinsi ya kumrudishia fedha zake. Huyo ambaye hajaripoti kwa kweli sina habari zake,” alisema Katibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles