24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mayanja: Niko tayari kufukuzwa Simba

mayanjaNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

KOCHA wa timu ya Simba, Jackson Mayanja, amesema yuko tayari kufukuzwa kazi Simba endapo atapangiwa kikosi na kiongozi yeyote wa klabu hiyo, licha ya kufahamu uwepo wa wachezaji wanaomilikiwa na viongozi hao.

Kauli hiyo ya Mayanja imekuja siku chache baada ya Kamati ya Utendaji ya timu hiyo kumsimamisha nahodha wake msaidizi, Hassan Isihaka kwa muda usiojulikana pamoja na kuagiza alipwe nusu mshahara kwa kile kinachodaiwa kuonesha kitendo cha utovu wa nidhamu kwa kocha wake.

Akizungumza na MTANZANIA, Mayanja alisema kuwa licha ya kufahamu uwepo wa wachezaji wanaomilikiwa na viongozi wa klabu hiyo, hatokuwa tayari kulazimishwa kuwatumia wachezaji ambao hawapo kwenye mpango wake.

“Kumiliki mchezaji ni jambo ambalo linatumika sehemu nyingi si hapa Tanzania, kwani hata Ulaya wanafanya hivyo lakini mchezaji atacheza kulingana na mipango ya kocha na si mtu tofauti kupanga timu ya kucheza.

“Sikuwahi kupangiwa na hakuna wa kunipangia mchezaji wa kucheza kwenye klabu hii, mimi ni kocha ninayefuata misingi ya taaluma yangu hivyo sitaweza kuogopa kusema ukweli, ndio maana nimelizungumza hili bila hofu ili kila mtu afahamu wajibu wake,” alisema Mayanja.

Akizungumzia mgogoro wa klabu hiyo dhidi ya Isihaka, alisema kuwa kila klabu ina utaratibu wake wa kuwaonya wachezaji wanapokosea.

“Nilimsamehe kabla hivyo sina tatizo na Isihaka, kilichofanyika ni utaratibu wa klabu katika kutoa onyo kwa wachezaji wake wanapofanya makosa ili jambo hilo lisijirudie tena.

“Mbali na kusikia kwenye vyombo vya habari hadi sasa hajafika kwangu kuniomba msamaha, hata hivyo sikuona ulazima wa yeye kuzunguka pembeni wakati alikuwa na nafasi ya kuniomba msamaha siku ambayo alifanya tukio hilo na si kusubiri hadi hali iwe mbaya,” alieleza.

Aliongeza kuwa licha ya kuchafuliwa na kuonekana kuwa chanzo cha mgogoro ndani ya klabu hiyo, hakuwahi kuwa na tatizo na mchezaji yeyote tangu aanze kuwa kocha wa soka.

“Tangu niwe kocha nimezifundisha klabu mbalimbali lakini sikuwahi kuwa chanzo cha ugomvi, kama kuna mtu kazi yake ni kunigombanisha na klabu ni bora akafanya yake kuliko kuzungumza mambo ambayo si ya kweli.

“Hata kama ni kweli aliyekuwa kocha wa timu hii, Dylan Kerr alisema hayo, ningependa afanye mambo yake wakati wake ulishapita,” alisema Mayanja.

Aidha, Mayanja alisema kuwa alimkanya mshambuliaji wa timu hiyo, Hamis Kiiza kutojiingiza na mambo yasiyomhusu badala yake alimtaka kujielekeza zaidi kwenye kuisaidia timu hiyo ili kupata ushindi kwenye michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles