25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mayanja jeuri bwana

mayanja-picha-500x300NA JUDITH PETER, DAR ES SALAAM

KOCHA Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja, ameanza tambo na kuwarushia vijembe watani wao wa jadi, Yanga akidai kamwe hawezi kuwahofia kwa kuwa kikosi chao hakina tofauti na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa muda mfupi tangu Mayanja aanze kibarua cha kuinoa Simba, amepata mafanikio makubwa baada ya kuiwezesha timu hiyo kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na kuwapumulia vinara hao, Yanga waliowazidi kwa pointi moja.

Jeuri ya kocha huyo kwa Yanga inatokana na matokeo ya ushindi waliyopata katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu, ambayo yamewawezesha kuvuna jumla ya pointi 12 na mabao 12.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, ndio wanaongoza katika msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 40, huku Simba wakishika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 39 wakifuatiwa na Azam FC nafasi ya tatu.

Akizungumza Dar es Salaam juzi mara baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Mgambo Shooting katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Mayanja alisema haoni sababu ya kuiogopa Yanga wakati kuna mechi nyingine ngumu zinazowakabili kwenye ligi hiyo.

“Ni kweli tumepata mafanikio makubwa na kuweza kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ambapo tunawakaribia Yanga kileleni, lakini huu si muda mwafaka wa kuwajadili sana mahasimu wetu kwani muda utakapofika nitafanya hivyo,” alisema.

Kocha huyo raia wa Uganda ambaye nyota yake inaonekana kung’ara zaidi akiwa Simba, alisema hawatakubali kupunguzwa kasi watakapocheza ugenini katika mechi zijazo, badala yake watahakikisha mashambulizi wanayofanya wakicheza uwanja wa nyumbani yanaendelea.

“Jambo kubwa la msingi mbele yetu ni kuhakikisha mapambano yanaendelea katika mechi zijazo za ugenini, nitawapa maelekezo sahihi wachezaji wangu ili waweze kutambua mambo wanayotakiwa kufanya wakiwa uwanjani,” alisema.

Hata hivyo, Mayanja aliwaomba mashabiki wa Simba kuendelee kutoa sapoti yao ili kusaidia maendeleo ya timu hiyo, ambayo imeanza kuimarika kwa kufanya vizuri na kuingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa msimu huu.

Simba inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumamosi hii kuchuana vikali na Kagera Sugar, ambao watakuwa wenyeji wao katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi, Tabora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles