28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kanakamfumu amchana Pluijm

Hans-van-der-Pluijm*Aeleza asipobadilika timu itaondolewa mapema kimataifa

NA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Joseph Kanakamfumu, amemshauri Kocha Mkuu wa timu ya Yanga, Hans van der Pluijm kubadili mfumo wa timu yake mapema ili kupata uhakika wa ushindi kila mchezo katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa.

Ushauri huo kwa Pluijm umekuja baada ya timu hiyo kuanza kupokea kichapo cha bao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili dhidi ya Coastal Union na sare ya 2-2 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya.

Kanakamfumu aliweka wazi kama asipobadilika na kukubali kubadili mfumo anaotumia, atakuwa kwenye wakati mgumu au kuondolewa mapema kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika licha ya kuwa na timu nzuri.

Akizungumza na MTANZANIA, Kanakamfumu alisema  kocha huyo atakuwa na wakati mgumu kupata ushindi katika kila mchezo atakaocheza endapo ataendelea kutumia mfumo wa 4-2-3.

Alisema mabadiliko atakayokubali kuyafanya yataisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika inayotarajiwa kuanza Februari 13 mwaka huu siku chache kuanzia sasa.

“Bado Yanga ni timu ya kawaida ingawa imefanya usajili mkubwa ukilinganisha na timu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu, hivyo wana wajibu wa kufanya marekebisho kabla ya kuanza michezo migumu ya Klabu Bingwa Afrika,” alisema Kanakamfumu.

 

“Pluijm amezoeleka kuichezesha Yanga kwenye ligi mfumo ambao unatumia sana washambuliaji kuliko viungo, hali ambayo inamgharimu katika baadhi ya michezo.

“Mfumo huo ndio ulisababisha timu hiyo kufungwa na Coastal Union wiki iliyopita, wakati anaweza kuchezesha mfumo  wa 4-4-2 ambao ulimpa ushindi katika mchezo dhidi ya Simba katika mzunguko wa kwanza,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Polisi Dodoma, alisema endapo kocha huyo hatoweza kubadilika anaweza kupata matokeo mabaya zaidi kwenye michezo ijayo.

“Tangu Nadir Harub (Cannavaro) awe majeruhi safu ya ulinzi imepoteza umakini kitu ambacho kinafanya kuwe dhaifu eneo la nyuma kutokana na uchache wa viungo.

“Unapochezesha mfumo huo ni muhimu kuwa na mshambuliaji mwenye kiwango kizuri cha ufungaji, ili kufanya upatikanaji wa mabao uwe mwepesi, lakini ikiwa tofauti litakuwa jambo la kubahatisha kama anavyofanya Pluijm,” alisema.

Aliongeza kwamba, ni nadra kwa kocha yeyote duniani kuchezesha mfumo ambao unatoa fursa chache za utengenezaji wa pasi za mwisho ambazo zinatumika kupata mabao.

“Kabla ya Haruna Niyonzima kurudi dimbani, awali Pluijm alikuwa akiwatumia Thaban Kamusoko kama namba nane huku Mbuyu Twite akiwa namba sita, idadi ambayo ni ndogo ya viungo ukilinganisha na washambuliaji,” alisema.

Alieleza kuna wakati timu hiyo inalazimika kucheza mipira mirefu kutokana na udhaifu wa mfumo unaotumika ambao unaowanyima wachezaji kuchezea mpira wa burudani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles