25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Maximo aifanya Yanga kama Stars

Marcio Maximo
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo

Na Abducado Emmanuel, Dar es Salaam

KOCHA mpya wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo, ameanza kwa kasi kibarua hicho kwa kuwatahadharisha wachezaji wenye utovu wa nidhamu kuacha tabia hiyo, huku akipanga kuwakata mishahara wachezaji wote watakaokiuka masharti hayo.

Maximo ambaye miaka minne iliyopita alikuwa akiinoa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, akisisitiza nidhamu leo ataanza rasmi programu yake ya kuinoa timu hiyo kwenye ufukwe wa Bahari ya Coco jijini Dar es Salaam tayari akiwa amesaini mkataba wa miaka miwili wa kuinoa Yanga sambamba na msaidizi wake, Leonardo Neiva.

Mbrazil huyo alifanya kikao na wachezaji wa timu hiyo kilichofanyika jana asubuhi kwenye Makao Makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam, ili kuwapa mikakati na masharti yake kabla ya kuanza rasmi programu ya mazoezi yake.

Habari za ndani toka kwenye kikao hicho zilieleza kuwa, Maximo amewataka wachezaji wote kuwa na umoja na nidhamu kwa ajili ya kufikia mafanikio kwa pamoja, huku akitoa sharti la wachezaji wote kuacha uzembe na vitendo vya utovu wa nidhamu.

“Suala la utovu wa nidhamu kalisisitiza sana, akidai hataweza kumvumilia mchezaji atakayekuwa na tabia hiyo na kwa atakayekiuka atapewa adhabu ya kukatwa mshahara kwa sababu atakuwa ameenda kinyume na misingi na taratibu alizowawekea kupitia kikao hicho.

“Pia amewataka wachezaji kuwa na umoja na kupendana ndani na nje ya uwanja, kwani mafanikio bila umoja hayataweza kufikiwa, pamoja na hayo amewataka wachezaji kuonesha asilimia 100 ya viwango uwanjani kwa manufaa ya timu,” kilieleza chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Mara baada ya kukabidhiwa mikoba hiyo, Maximo alieleza kuwa wiki hii atawapa mazoezi magumu wachezaji wake ya kuwajengea stamina pamoja na ya ufundi uwanjani, ataanza kutoa mbinu zake watakaporejea wachezaji wa timu hiyo waliopo timu za Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles