26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAZIRI WA JPM WAIBUA MASWALI

MTZ jmosi new july.inddNa Waandishi Wetu

 BARAZA la Mawaziri la Rais John Magufuli alilolitangaza juzi limezua maswali mengi, kutokana na kile kinachoelezwa kujaa makosa mengi ya kimantiki na kiufundi.

Wasomi na watu wa kada mbalimbali ambao wameutazama muundo pamoja na aina ya watu walioteuliwa kuunda Baraza hilo la Mawaziri wameyataja mambo sita ambayo yanaonekana kujenga taswira ya kuwako kwa nyufa katika baraza hilo.

Mambo hayo ni pamoja na uteuzi kutozingatia suala la Muungano, uwiano wa mikoa, mawaziri wasio na makandokando na usawa wa kijinsia.

Mengine ni utashi uliotumika kuunganisha wizara  na hatua ya Rais kuacha baadhi ya nafasi za wizara wazi, lakini pia akichukua mawaziri nje ya wabunge wake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hoja hizo zimekuja wakati ambapo tayari Rais Magufuli ametangaza Baraza lake la Mawaziri lenye Wizara 18, mawaziri 19, manaibu mawaziri 15, huku nne kati ya hizo akiziacha wazi.

Wizara hizo nne alizoziacha wazi huku akiwa tayari amezipatia manaibu waziri ni Wizara ya Fedha na Mipango (Naibu ni Dk. Ashatu Kijaji), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Mhandisi Edwin Ngonyani), Wizara ya Maliasili na Utalii, (Mhandisi Ramo Makani), Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi (Stella Manyanya).

Pamoja na kwamba Magufuli alitoa sababu za kuacha wazi wizara hizo, akisema ni kutokana na unyeti wake na hivyo kushindwa kupata mawaziri kamili, lakini jambo hilo ni miongoni mwa mambo yaliyoibua maswali.

 

SUALA LA MUUNGANO

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaeleza kuwa ili kuendelea kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao umedumu kwa miaka 51 sasa, uteuzi wa Baraza la Mawaziri ulipaswa kuzingatia hoja hiyo ipasavyo.

Hata hivyo, wanasema uteuzi wa baraza hilo haukuzingatia au haukulipa uzito unaotakiwa suala la Zanzibar kwa kuwa kati ya mawaziri 30 walioteuliwa hadi sasa, Wazanzibari ni wawili tu.

Mawaziri hao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa.

Duru zaidi zinabainisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mambo ya Ndani pamoja na ile ya Ofisi ya Makamu wa Rais ambazo zinashughulikia masuala ya Muungano zilipaswa kupewa watu wenye upeo na masuala ya Muungano ili waweze kutatua kero za Muungano huo.

UWIANO WA MIKOA

Suala la uwiano wa mikoa ni miongoni mwa mambo ambayo yanajadiliwa sana na baadhi ya wachambuzi, hasa ikizingatiwa kuwa kihistoria uteuzi wa mawaziri umekuwa ukizingatia hilo.

Hata hivyo, katika uteuzi alioufanya Magufuli suala hilo hakulizingatia kutokana na hatua yake ya kuteua mawaziri wanne kutoka mkoa mmoja huku mingine ikiwa haina hata mmoja.

Mfano mmojawapo unaotolewa na wachambuzi hao ni Mkoa wa Ruvuma, uliotoa mawaziri wanne, ambao ni Jenister Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi na Vijana, Ajira na Walemavu), Edwin Ngonyani (Naibu Waziri Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Ramos Makani ( Naibu Waziri Maliasili na Utalii) na Stella Manyanya (Naibu Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi).

Hoja kama hiyo inaelekezwa pia Mkoa wa Dodoma, ambako wameteuliwa watatu katika baraza hilo ambao ni Anthony Mavunde (Naibu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi na Vijana, Ajira na Walemavu), Ashatu Kijaji (Naibu Waziri Fedha na Mipango), George Simbachawene (Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI).

Katika hilo, baadhi ya mikoa ambayo haina mwakilishi katika baraza hilo ni pamoja na Shinyanga, Kigoma, Kilimanjaro na Rukwa.

 

KUUMBUA CCM

Hatua ya Rais Magufuli kuacha wazi baadhi ya nafasi za wizara, lakini pia akichukua mawaziri nje ya wabunge wake wa CCM, nako kumezua maswali mengi.

Baadhi wanaona kuwa huenda Magufuli haridhishwi na sifa za aina ya wabunge walio ndani ya chama chake wanaozidi 200.

Kauli hiyo wanaipa mkazo kwa kutumia hoja kwamba licha ya Rais kutumia zaidi ya mwezi mmoja kuangalia anayefaa kuingia kwenye baraza lake, lakini bado ameshindwa kukamilisha uteuzi huo kwa kupata wenye sifa za kuongoza Wizara nne alizoziacha wazi.

Hoja hiyo pia inatiwa nguvu na Magufuli mwenyewe, kutokana na hatua yake nyingine ya kuteua wabunge wawili kutoka nje ya wabunge wa CCM na kuwapa uwaziri katika serikali yake.

Wabunge aliowateua na kuwafanya mawaziri ni pamoja na Dk. Possy Abdallah, ambaye amekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi na Vijana, Ajira na Walemavu pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga.

Mwendelezo huo wa kuteua watendaji nje ya wabunge wa CCM ulijitokeza pia bungeni wakati wa mchakato wa kumpata Naibu Spika, ambako Magufuli alimteua Dk. Tulia Mwansasu kuwa Mbunge, akitokea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambako alikuwa naibu mwanasheria.

Katika muktadha huo, MTANZANIA Jumamosi lilimuuliza Msemaji wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, juu ya sababu zilizomsababisha Rais ashindwe kukamilisha uteuzi wa mawaziri wa baraza lake alilounda ambapo alijibu kwa kusema rais bado hajapata watu watakaokamilisha nafasi hizo zilizobaki, kwamba atakapowapata atawataja.

“Jana (juzi) waandishi walimuuliza swali kama hilo akajibu bado hajawapata na siku akiwapata atawatangaza,” alisema Msigwa.

Na alipoulizwa juu ya sababu ya Wizara ya Tamisemi kuhamishiwa Ofisi ya Rais, Msigwa alijibu kwa kusema kuwa Rais Magufuli aliamua kufanya hivyo ili kutimiza lengo lake la kuunda baraza dogo la mawaziri pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.

Akitanabahisha mgawanyo wa majukumu kupitia Wizara hiyo mpya ambayo ipo chini ya Ofisi ya Rais, Msigwa alisema Waziri George Simbachawene ataongoza Tamisemi na Angela Kairuki ataongoza Utumishi na Utawala Bora.

 

Mawaziri wenye makandokando

Pamoja na kwamba yeye mwenyewe Magufuli aliahidi kutochukua watu wenye makandokando katika serikili yake, hata hivyo, hatua yake ya kumteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk Harrison Mwakyembe  kuwa Waziri wa  Katiba na Sheria na Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, imezua hisia hasi.

Pamoja na kwamba wapo wanaoona viongozi hao licha ya makandokando yao huenda wakahimili kasi ya Magufuli, hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wameonyeshwa kushangazwa na hatua hiyo ya Rais.

Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, tayari amekaririwa akionyesha kushangazwa na kitendo cha Magufuli kumteua Profesa Muhongo, mtu ambaye alikumbwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 za Esrow, iliyomlazimu kujiuzulu wadhifa wake wa Waziri wa Nishati na Madini wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Lissu alisema uteuzi huo wa Muhongo ni sawa na kulitukana Bunge na Watanzania na kwamba ataendeleza suala hilo la Escrow bungeni kutokana na kwamba hata mwaka mmoja haujakwisha tangu Prof. Muhongo alipojiuzulu kwa kashfa hiyo kubwa.

Itakumbukwa kuwa wakati Profesa Muhongo akijiuzulu alidai kuwa hakufanya kosa lolote kwa kuwa fedha hizo za Escrow hazikuwa za serikali, hoja iliyopigwa na baadhi ya wanasiasa, hususan waasisi wa hoja hiyo kama akina David Kafulila na Zitto Kabwe, ambao walidai kuwa katika fedha hizo ilikuwemo kodi ya serikali ambayo haikuwa imelipwa.

Mbali na hoja hiyo ya Escrow, Muhongo pia amekuwa akitajwa kuwa na kauli za kukera na kukatisha tamaa wafanyabiashara wa ndani, hasa kwenye uwekezaji wa gesi na madini kwa madai kuwa hawana uwezo huo na kwamba uwezo wao ni kuwekeza kwenye juisi na matunda.

Mbali na Profesa Muhongo, mwingine ambaye uteuzi wake umezua maswali ni Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Harrison Mwakyembe.

Wanaoshangaa uteuzi wa Mwakyembe wanasema Rais Magufuli hakupaswa kumteua kwa kuwa ni yeye ndiye aliyehusika na uteuzi wa  Bodi ya Wakurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, ambayo Magufuli yeye mwenyewe ameivunja kutokana na upotevu wa makontena zaidi ya 2,500.

Watu hao wanasema kama Magufuli aliweza kuivunja bodi hiyo kutokana na madudu yaliyoyakuta bandarini, pia alipaswa kumwajibisha Mwakyembe  kwa kushindwa kushughulikia ufisadi uliokuwa ukitendeka katika mamlaka hiyo kwa kuwa alikuwa Waziri wa Uchukuzi wakati hayo yakitokea.

Si hilo tu, Mwakyembe pia anahusishwa na kashfa ya ununuzi wa mabehewa chakavu ya Shirika la Reli (TRL).

Katika orodha hiyo ya watu wenye makandokando pia jina la Mwigulu Nchemba linatajwa kwenye uzembe uliopelekea uchotwaji wa fedha za Escrow.

 

Mwigulu, ambaye wakati wa serikali ya Kikwete alikuwa Naibu Waziri wa Fedha lakini sasa amepewa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, baadhi wanaona alipaswa kuunganishwa na maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) waliotimuliwa kwa kuikosesha serikali mapato, kwa kuwa wakati madudu hayo yakitokea alikuwa naibu waziri mwenye dhamana.

 

USAWA WA KIJINSIA

Suala la usawa wa kijinsia nalo limeibua maswali kutoka kwa wachambuzi hawa wanaolitazama Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.

Wapo wanaoona kwamba hakulizingatia na hivyo kulitupilia mbali azimio la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) linaloelekeza usawa wa kijinsia angalau tunakoelekea ifikie asilimia 50 kwa 50 katika ngazi za kutoa maamuzi kisiasa.

Hata hivyo, katika Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli mawaziri wanawake ni watatu tu, huku wanaume wakiwa 12, manaibu watano huku wanaume wakiwa 10.

 

MRUNDIKANO WA WIZARA

Licha ya baadhi kumpongeza kwa kuunda Baraza dogo la Mawaziri, lakini bado wapo wanaoona kwamba baadhi ya wizara zilizounganishwa zinaweza kugeuka na kuwa mzigo mkubwa kwa serikali.

Mfano wa wizara hizo ni pamoja na ile ambayo hadi sasa haijapata waziri  ambayo ni Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ambayo baadhi ya wadadisi wanaeleza kuwa waziri huyo atakuwa na rundo la taasisi, bodi na mashirika ambayo yanahitaji umakini na uangalizi mkubwa ili kuweza kuleta mapinduzi ya kimaendeleo kama alivyoahidi Magufuli mwenyewe.

Taasisi na mamlaka hizo ni  kama Mamlaka ya Bandari (TPA), Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Majengo (TBA), TEMESA, RFB, ERB, CRB, Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA),  Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Shirika la Reli (TRL), TAZARA na nyingine.

Wizara nyingine zinazoonekana kurundikwa ni Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora), Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu).

Wasemavyo wachumi kuhusu baraza dogo

Profesa Semboja

Profesa wa uchumi kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Haji Semboja, anasema kuundwa kwa baraza dogo la mawaziri hakumaanishi kunapunguza gharama za uendeshaji wa Serikali.

Alisema faida ya baraza la mawaziri itatokana na ufanisi watakaoufanya mawaziri wenyewe kwa kuongezea pato la Taifa mara tatu ya kiwango kinachokusanywa kwa sasa.

“Siwezi kuamini kama baraza dogo la mawaziri linaweza kuleta athari chanya kwa uchumi wa nchi, kikubwa ni kwamba hao walioteuliwa wanatakiwa waonyeshe ufanisi wao kwa kusukuma mbele gurudumu la uchumi wa nchi, unajua haya mambo yamegawanyika sehemu mbili, unaweza kuunda baraza dogo la mawaziri na lisiwe na tija na pia ukaunda baraza kubwa na likaleta mafanikio…

“Kuunda baraza la mawaziri ni sawa na kuweka mtaji kwenye biashara, kwamba ugharamike ili unufaike. Tanzania ya leo inahitaji baraza la mawaziri litakalojenga uchumi mara tatu ya mapato yanayokusanywa sasa,” alisema Profesa Semboja.

Profesa Lipumba

Kwa upande wake, Profesa  Ibrahim Lipumba alisema kuwa dhamira ya rais ya kuunda baraza dogo la mawaziri ni mrengo mzuri wa kupunguza matumizi ya serikali.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alitoa angalizo kwa kusema matunda ya baraza dogo la mawaziri hayatatokana na miujiza, bali yatatokana na utekelezaji wa mipango ya kuinua uchumi ambayo rais amekusudia kuifanya.

“Uzuri wa kuwa na baraza dogo la mawaziri ni rahisi kulisimamia kwa kufuatilia kila nyendo, unachokiagiza kwa manufaa ya wananchi lazima kitoe matokeo chanya, lakini tofauti na hivyo unaweza kuwa na baraza dogo lisilokuwa na tija kwa nchi,” alisema Profesa Lipumba.

Kuhusu hoja ya rais kushindwa kukamilisha baraza lake la mawaziri kwa kuacha wazi viti vinne, Profesa Lipumba alisema kuwa uamuzi huo huenda umetokana na kutokukamilika kwa uchaguzi wa wabunge kwenye baadhi ya majimbo.

“Rais hajaacha nafasi hizo nne kwa makusudi, kumbuka kuna majimbo takribani manane hayajafanya uchaguzi wa wabunge, hivyo inawezekana akaziba viti hivyo baada ya chaguzi zote kumalizika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles