30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mawakili wavutana kesi ya Wenje, Mabula

mabulaNa Judith Nyange, Mwanza

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mwanza chini ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Sumbawanga, Kakusulo Sambo, imeanza kusikiliza kesi namba 4/2015 iliyofunguliwa na Ezekiel Wenje (Chadema) kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la Nyamagana dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo, Stanslaus Mabula (CCM), msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo iliyoanza jana, mawakili wa wajibu maombi wa pili na wa tatu (Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria wa Serikali), Siti Mkemwa na Ajuaye Bilishanga, wameiomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi hayo kwa gharama sababu yamewasilishwa chini ya kifungu cha sheria ambacho si sahihi.

“Mahakama hii haina uwezo wa kusikiliza maombi haya kwa sababu yameletwa chini ya sheria namba 189 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002. Katika sheria zetu za ukomo hatuna sheria namba 189, badala yake tuna sheria namba 89,” alisema Mkemwa.

Kwa upande wake, mawakili wa mjibu maombi wa kwanza (Mbunge Mabula), Costantine Mtalemwa na Faustine Malongo, walisema wanaunga mkono hoja zilizotolewa na wakili Mkemwa na kuongeza kuwa waleta maombi walipaswa kutumia kifungu namba 93 kinachotoa mamlaka kwa mahakama kuongeza muda wa kutekeleza matakwa ya kisheria na si kutumia sheria ya ukomo.

Akijibu hoja za pingamizi, mawakili wa mleta maombi (Ezekiel Wenje), Deya Outa na Elias Hezron, walikubaliana na Mtalemwa na Mkemwa kuwa hakuna sheria ya ukomo namba 189 na kosa hilo limetokana na makosa ya kiuandishi, na sheria hiyo kwa usahihi ni namba 89.

Outa aliiomba mahakama hiyo kupuuzia makosa madogo madogo ya kiuandishi, hasa kama hayana athari na tofauti na kifungu kilichotajwa, pia wameomba pingamizi mbili zilizowasilishwa na mjibu maombi wa pili, wa tatu na wa nne zitupiliwe mbali kwa gharama.

Hata hivyo, Outa pia aliwasilisha maombi namba nane ya mwaka 2016 chini ya sheria ya ukomo kifungu 14 (1), kiapo chake na cha mleta maombi kinachoomba kuongezewa muda na kusema ni lini na wapi atakapokuwapo mleta maombi namba moja (Wenje) ili mjibu maombi wa kwanza, wa pili na tatu waweze kukagua fomu namba 21 D zilizotumika katika uchaguzi.

Wakili Mkemwa na Bilishanga, wameiomba mahakama isishawishiwe na hoja ya makosa ya kiuandishi na maombi hayo yatupiliwe mbali kwa gharama kutokana na hoja ya mleta maombi pamoja na viapo vyao kutokuwa na mashiko pamoja na kukosewa kwa kifungu cha sheria kilichotumika.

Mtelemwa alidai ili muda uliotolewa uweze kuongezwa, lazima sababu za msingi za kuchelewa kwa kila siku zielezwe na si kusubiri huruma ya mahakama, pia maombi hayo yameambatanishwa na viapo visivyo vya ukweli na vinakinzana.

Naye wakili Outa aliwasilisha maombi namba 22 ya mwaka 2016 kuiomba mahakama itoe ruhusa ili aweze kupeleka maswali kwa mjibu maombi wa kwanza na wa pili kwa sababu wana nyaraka ambayo ni fomu 21B iliyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Alisema kama ombi hilo halitaruhusiwa, atalazimika kuita mashahidi 693 kutoka katika kila kituo kilichotumika kupiga kura katika  Jimbo la Nyamagana kutoa ushahidi.

Kutokana na hoja hizo, Jaji Sambao aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 3, mwaka huu ambapo alisema mahakama hiyo itatoa uamuzi wa hoja za pingamizi pamoja na maombi yote yaliyowasilishwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles