Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mawakili wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DSM), ‘aliyepotea’ Abdul Nondo, wamejikuta katika wakati mgumu na kukimbilia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusubiri huenda mwanafunzi huyo atafikishwa katika mahakama hiyo.
Wiki iliyopita, Mawakili hao wa Mtandao wa watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC) kwa kushirikiana, Mtandao wa Wanafunzi (TSNP) na Kituo cha Haki za Binamu walipeleka maombi Mahakama Kuu kuitaka itoe amri kwa Jeshi la Polisi kumpeleka Nondo mahakamani au kumpa dhamana wakati shauri la msingi likiwa linaendelea.
Mmoja wa mawakili wa Nondo, Jones Sendodo ameiambia Mtanzania Digital kuwa leo Jumanne Machi 20, wamekwenda Kikuu cha Polisi (Central), ambako mwanafunzi huyo anashikiliwa na kupata wakati mgumu baada ya kuambiwa mwanafunzi huyo hayupo katika kituoni hapo.
“Tumekwenda kituoni hapo kumwangalia na kukamilisha baadhi ya taratibu lakini Central wamesema hayupo kwa hiyo tunakwenda kutega Kisutu tunafikiria labda wanaweza wakamleta hapa, wanasema hawajui alipo.
“Tumejaribu kuwasiliana na Mambosasa (Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam) hapokei simu na ofisini hayupo, tunafikiria watamleta hapa,” amesema Sendodo.