26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MAWAKILI WA LEMA WAOMBA KESI IHAMISHIWE MAHAKAMA KUU

Na JANETH MUSHI
-ARUSHA 


MAWAKILI wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), katika kesi ya kutoa lugha ya kumkashifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wameomba kesi hiyo ihamishiwe Mahakama Kuu ili ifafanue makosa ya kisheria yaliyomo kwenye hati ya mashtaka.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana, Hakimu wa mahakama hiyo, Nestory Baro, alisema mawakili hao, John Mallya na Sheck Mfinanga, walitoa ombi hilo wakati walipokuwa wakiwasilisha hoja zao za pingamizi, wakipinga hati ya mashtaka.

Katika kesi hiyo namba 351 ya mwaka jana, Lema na mkewe, Neema Lema, wanashtakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno uliokuwa na nia ya kumuudhi Gambo, ambapo Januari 18 mwaka huu, mawakili hao waliwasilisha notisi ya  pingamizi hilo kwa madai hati ya mashtaka ina mapungufu ya kisheria.

Akiwasilisha hoja hizo jana, Wakili Mallya alisema washtakiwa hao wameshtakiwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010, wakati hati ya mashtaka inayowashtaki ina makosa makubwa ya kisheria kwani shtaka wanaloshtakiwa nalo halipo kwenye sheria hiyo.

Mallya aliieleza mahakama hiyo kuwa kutokana na makosa hayo ya kisheria, hati hiyo inazua maswali magumu kisheria ili kuendelea nayo na kuwa Sheria ya Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai (CPA), inaeleza namna ya kuandika hati ya mashtaka inayotakiwa kuwa na taarifa za kutosha kuwafanya washtakiwa kuelewa wanachoshtakiwa nacho mahakamani.

“Tunaomba kama inafaa mahakama yako ihamishe kesi hii mahakama kuu, kuna maswali ambayo si ya kawaida ambayo yapo kwenye hati ili mahakama kuu ipate fursa ya kuzungumza na kutoa tafsiri katika kila jambo ambalo tunaona ni geni katika taratibu zetu za kisheria, ikiwezekana kuondoa shauri hili mahakamani,” alisema Mallya.

Mallya alisema sheria ambayo Lema na mkewe wanashtakiwa nayo haizungumzii chochote kuhusu watu wanapotumiana ujumbe mfupi wa maandishi, kwa kuwa mawasiliano binafsi ya mtu na mtu hayapaswi kuingiliwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema walipaswa kueleza ujumbe waliotuma umemfanya nini aliyetumiwa kwani makosa ni mengi.

Huku akinukuu vifungu mbalimbali vya sheria na kesi mbalimbali ambazo zimewahi kutolewa uamuzi, Mallya alitaja hoja ya pili kuwa ni mawakili wa Jamhuri kuweka ushahidi kwenye hati ya mashtaka suala ambalo halikubaliki kisheria na kuwa walipaswa kuandika katika hati hiyo ujumbe huo mfupi ulifanya nini kwa aliyetumiwa na si kuiweka yote kama walivyofanya.

“Sheria inaelekeza namna ya kuandika hati ya mashtaka ila ukiangalia hati hii haifai kabisa kuwa mahakamani, alitakiwa aseme meseji hiyo ilimtisha au ilifanya nini na si kuonyesha ujumbe unaodaiwa kuwepo kwenye meseji hiyo,” alisema Mallya.

Alifafanua kuwa katika sheria ya ushahidi inasema ni mazingira tata mke na mume kutoa ushahidi dhidi ya mwenzake na kuwa ikifika hatua ya kuwa wana kesi ya kujibu wanaweza kukataa kutoa ushahidi suala ambalo ni gumu kisheria.

“Mke na mume kwa mujibu wa sheria ni mashahidi tata kwani mke anaweza kuogopa kutoa ushahidi dhidi ya mumewe akihofia kupewa talaka, ndiyo maana tunataka tuende mahakama kuu ili Bakita waje watueleze maana ya neno shoga, kwani mwingine akiitwa shoga hana shida lakini mwingine akiitwa atarusha ngumi,” alisema Mallya.

Alitaja sababu nyingine ya pingamizi hilo kuwa ni kwenye hati hiyo ya mashtaka kuwa Mrisho Gambo amepewa cheo cha ukuu wa mkoa, wakati simu anayotumia ni yake binafsi na imesajiliwa kwa jina lake binafsi si cheo hicho wakati kwenye hati ya mashtaka mtu haruhusiwi kuweka wadhifa.

“Kama ni hivyo katika hati ya mashtaka wangemwandika Lema kuwa ni Mbunge wa Arusha Mjini na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, kwani Gambo anaweza kuhamishwa wakati wowote na sheria haibagui na pia haiwezekani watu wawili kutumia simu moja kutuma ujumbe mmoja na kwa wakati mmoja,” alisema Mallya.

Akijibu hoja za pingamizi hizo, Wakili wa Serikali, Rose Sule, huku akinukuu vifungu mbalimbali vya sheria alisema kuwa hoja ya hati ya mashtaka iko sahihi kisheria na haina mapungufu yoyote kwani hati imekuwa wazi na watuhumiwa wameelezwa wanakabiliwa na kosa gani.

Alisema katika hati hiyo ya mashtaka imeeleza kuwa kazi ya Lema ni mwanasiasa na wadhifa wake ni ubunge na kuwa baadhi ya hoja za mawakili hao wa Lema ni hoja za utetezi.

“Maelezo mengine waliyoyatoa hapa ni bora wasubiri kwenye utetezi kwani katika hati ya mashtaka mtuhumiwa wa kwanza (Lema) na kazi yake imetajwa ni mwanasiasa na wadhifa wake umetajwa ni ubunge,” alisema Sule.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Mfinanga alisema maelezo ya wakili wa Serikali hayashawishi mahakama kwa sababu hayana mamlaka yoyote kisheria yanayosapoti hoja zake hivyo kuiomba mahakama hiyo ipuuze hoja hizo kwani kuna makosa makubwa na ya wazi.

Hakimu Baro aliahirisha kesi hiyo na Februari 10 mwaka huu, atatoa uamuzi mdogo wa pingamizi hizo.

Lema bado anashikiliwa katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kukosa dhamana katika kesi namba 440 na 441 za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli ambapo alikamatwa Novemba 2, mwaka jana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles