25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE AUNDA TUME KUCHUNGUZA UDA

Na MWANDISHI WETU- DODOMA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, ameunda kamati ya watu watano ili kutafuta suluhu ya matumizi ya Sh bilioni 5.8 za uuzwaji wa hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda).

Taarifa hiyo imetolewa jana na Mbowe mwenyewe wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za upinzani bungeni mjini Dodoma.

Kwa mujibu wa Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kamati hiyo imeundwa baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na mameya, naibu mameya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na viongozi waandamizi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Katika kikao chetu hicho, tulikutana kujadili fedha hizo zilizoleta mvutano pamoja na kuangalia hali ya usafiri jijini Dar es Salaam.

Tumelitazama hili kwa upana na kwa kina zaidi, tumekubaliana kuunda kamati ya watu watano ambayo itakuwa ikiripoti kwangu, itakwenda kuandaa mpango mkakati wa namna ya kuboresha usafiri wa Dar es Salaam,” alisema Mbowe.

Alisema mapendekezo ya kamati hiyo yakikamilika ndani ya wiki moja au mbili, watayawasilisha serikalini na kwamba ana imani yatapokelewa.

“Dar es Salaam ni ya wote ingawa leo inaongozwa na Ukawa na sijui kesho itaongozwa na nani ndiyo maana tunapaswa kuweka kando siasa na kuangalia masilahi ya Taifa,” alisema Mbowe.

Mbowe aliwataja wajumbe wa kamati iliyoundwa kuwa ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia na Naibu Meya wa Ilala, Omar Kumbilamoto.

Hivi karibuni uliibuka mvutano kati ya Serikali na uongozi wa jiji hilo kuhusu kuidhinisha mabilioni hayo ya uuzwaji wa hisa asilimia 51 kati ya 100 kwa Kampuni ya Simon Group.

Jumamosi iliyopita, Baraza la Halmashauri ya jiji chini ya Mwita, walikutana na kushindwa kufikia mwafaka wa kuzipangia matumizi fedha hizo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni sawa na kubariki ufisadi wa uuzwaji wa hisa hizo ambazo wanaona ni kiasi kidogo.

Kikao hicho kilifanyika baada ya agizo la Rais Dk. John Magufuli alilolitoa Januari 27 mwaka huu, wakati akizindua mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam.

Katika agizo hilo, Rais Dk. Magufuli alitoa siku tano kwa uongozi wa jiji hilo kuhakikisha kiasi hicho cha fedha zilizolipwa na Simon Group  zinapangiwa matumizi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles