Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Zanzibar imetajwa kuwa kichochoro cha wafanyabishara wa dawa za kulevya waliokimbia kutoka Tanzania Bara, kutokana na udhibiti mkali unaofanywa na Mamlaka ya Kudhiti Dawa la kulevya nchini.
Hayo yameelezwa bungeni leo Jumanne Aprili 3, na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Antony Mavunde, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwantumu Dau Haji (CCM) ambaye alihoji ni kwanini Zanzibar imekuwa mlango wa kupitishia dawa za kulevya.
Akijibu swali hilo Mavunde amesema kutokana na kuongezeka kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya, imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa matumizi ya dawa hizo nchini.
“Udhibiti huo umesababisha Zanzibar kuanza kuwa kichochoro kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya waliokimbia kutoka Bara lakini naomba nilieleze bunge kuwa vikao vinafanyika ili kuweka mfumo thabiti wa kupambana na dawa hizo visiwani Zanzibar,” amesema.
Aidha, akitilia mkazo suala hilo, Waziri wa wizara hiyo, Jenista Mhagama amebainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi chache za Afrika zenye sheria nzuri ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
“Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa nchi za Afrika zitakazokuja kujifunza namna ambavyo tulivyofanikiwa kwenye mapambano hayo,” amesema Jenista.