21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

MAUWASA yawahakikishia wananchi kupata maji safi na salama

Na Samwel Mwanga ,Maswa

Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imewahakikishia wananchi ambao ni watumiaji wa maji ya Bwawa la New Sola lililoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo kuwa ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Bwawa hilo ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji wa Maswa na vijiji 11.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mauwasa,Mhandisi Mathias Nandi kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa chujio la kuchujia maji katika mitambo ya kusukuma maji iliyoko katika bwawa hilo.

Sehemu iliyowekwa pampu za kusukuma maji kutoka katika bwawa la New Sola lililoko wilaya Maswa mkoani Simiyu kwenda kwenye chujio la maji kabla ya maji hayo kusukumwa kwa wananchi(Picha Na Samwel Mwanga)

Amesema kuwa serikali ilitoka kiasi cha fedha Sh bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa chujio hilo ambo kwa sasa limekwisha kukamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutumika na hivyo kuwahakikishia watumiaji wa maji hao kuwa ni safi na salama.

Amesema kuwa katika ujenzi huo kuna maabara ambayo kazi yake kubwa ni kutibu maji na kuua vijidudu vyote vinavyotoka katika bwawa kabla ya kusafirishwa kwenda kwa watumiaji wa maji.

“Ujenzi huu wa chujio pia kuna maabara kubwa ambayo inatumika kwa ajili ya kuhakikisha inaua vijidudu vyote vinavyopenya kwenye maji kutoka bwawani na kuingia kwenye chujio hivyo vyote huuawa kwa dawa ya Clorine kabla ya kusafirishwa kwenda kwa watumiaji wa maji na kwa ufupi maabara hiyo ndiyo kutibu maji yetu,”amesema.

Amesema kuwa kabla ya ujenzi wa chujio hilo walikuwa wakisukuma maji ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa na tope na hivyo kuzua malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wananchi.

“Kabla ya kukamilika kwa ujenzi wa chujio hilo ulipata changamoto kutoka kwa wananchi wanaotumia maji yetu kulikuwa na malalamiko mengi kuwa yana kiwango kikubwa cha tope na hilo lilikuwa wazi kwa kuwa hatukuwa na chujio ila kwa sasa maji yetu ni maangavu na malalamiko hayapo tena wananchi wanafurahia huduma yetu”amesema.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya Mauwasa,Paulina Ntagaye amesema kuwa wataendelea kuisimamia menejimenti ya Mamlaka hiyo ili iweze kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia maji safi na salama na kuwaomba wananchi kuwafichua watu wote wanaohujumu miundo mbinu ya maji ya Mauwasa.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa wananchi wa wilaya hiyo hususani wa mji wa Maswa na vijiji 11 wanaotumia maji ya bwawa hilo kuona thamani ya bwawa la New Sola hivyo wana kila sababu ya kuhakikisha wanalilinda na kulitunza.

Amesema kuwa kwa sasa Mauwasa inatakiwa kuweka nguvu kubwa katika kulilinda bwawa hilo na lenye raslimali ya maji na serikali ya wilaya hiyo imewahakikishia kuwawekea mazingira mazuri ya utendaji wa kazi zao.

“Uongozi wa Mauwasa lilindeni bwawa la New Sola kwa gharama zote sisi kama serikali ya wilaya tutawatengenezea mazingira mazuri ya utendaji wenu wa kazi pia niombe wananchi hasa wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka bwawa hili kushirikiana na Mauwasa kulilinda kwa faida ya wote kwani hatuna chanzo mbadala cha maji iwapo hicho kikitoweka,”amesema.

Bwawa la New Sola linalomilikiwa na Mauwasa linawahudumia wakazi wapatao 120,000 wa mji wa Maswa na vijiji 11 vilivyoko katika wilaya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles