Na Christopher Msekena
Kutoka pande za Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, mwimbaji wa gospel anayekuja kwa kasi kwenye muziki huo, Collins Efe, ameweka wazi kuwa wimbo Thank You, umebeba ushuhuda wake wa ugonjwa corona ulivyomtesa, Mei, mwaka huu.
Collins ameliambia MtanzaniaDigital kuwa kila mtu anapaswa kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyompigania mwaka 2020 ila kwa upande wake alipitia wakati mgumu baada ya kupata corona wakati mkewe akiwa na ujauzito pamoja na mtoto wao wa kwanza, Alma.
“Nilipata maumivu makali ya kifua kwa wiki mbili mnamo Mei 5, mwaka huu na baada ya kupima nilikutwa na corona na ukiangalia mke wangu alikuwa mjamzito wa wiki 38 na tuna binti wa miaka miwili anaitwa Alma na nikiwa kama baba ilitakiwa nijitenge na kuhudumia familia mpaka nilipopona ulikuwa wakati mgumu lakini Mungu alinivusha na mke wangu akajifungua salama mtoto wetu wa pili (Quarantining when baby Zoe came and how she came in such trying time could only be GOD) hivyo nina kila sababu ya kusema asante kwake na mashabiki dunia kote naomba waungane na mimi kushukuru kupitia wimbo huu ambao upo kwenye chaneli yangu ya YouTube,” amesema Collins.