25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Madiwani watakiwa kumaliza kero sugu Serengeti

Na Malima Lubasha, Serengeti

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Nurdin Babu ametoa wito kwa madiwani wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanatumia muda wao kutatua kero sugu wilayani humo hususan katika huduma ya Elimu, Afya, Wizi wa Ng’ombe, Barabara na Ardhi ambazo zimedumu kwa muda mrefu.

Babu aliyasema hayo juzi baada ya madiwani kuapishwa na kukabidhiwa halmashauri ili waanze kutekeleza majukumu yao akiwataka kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine kupokea kero za wananchi, kusikiliza na kuzitatua.

Alisema hadi sasa halmashauri inakabiliwa na changamoto nyingi lakini ni vyema wahakikishe wanaanza na ujenzi wa vyumba 18 vya madarasa vinavyohitajika katika shule za sekondari kabla ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza waliofaulu ni ambao ni 5,706 sambamba na kumaliza shule za msingi upungufu ni madarasa 166 kwa upande wa shule za msingi.

Alisema taarifa inaonyesha jumla ya shule za msingi 119 na sekondari 34 wilayani humo zina idadi kubwa ya wanafunzi huku baadhi yao wanakaa chini na madarasa mengine hayana sakafu hivyo madiwani wanatakiwa kwenda kushirikiana na maofisa tarafa,watendaji wa kata vijiji,wenyeviti wa vijiji kutatua kero hiyo.

Pia aliwataka viongozi hao kutatua migogoro ya ardhi ya muda mrefu katika vijiji na kata zao ambapo aliwahimiza kutenga siku ya kupokea na kusikiliza kero za wananchi zinazowakabili katika maeneo pamoja kuweka mikakati ya shughuli za maendeleo kama walivyoahidi wakati wa kampeni.

Aidha Babu, alikemea vitendo vya wizi wa mifugo wilayani humo unaoendela kufanyika katika vijiji bila vingozi kuchukua hatua na kusisitiza kila mfugaji, mwananchi na viongozi kuweka utaratibu wa kufanya ulinzi usiku ikiwa ni pamoja na kufanya doria usiku na mchana kubaini wezi na kuonya watu kuacha kujichukulia sheria  mkononi badala yake waache sheria ifuate mkondo wake. 

Babu pia aliwataka madiwani hao kujenga tabia ya kuheshimiana, kushirikiana na kupendana muda wote wa miaka mitano katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya halmashauri kwani wote wanajenga nyumba moja ambayo ni wilaya ya Serengeti hivyo haina haja ya kuendekeza migogoro.

Awali Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti Jacob Bega, aliwataka madiwani hao kusimamia mapato na matumizi ya  fedha za Halmashauri na kubuni vyanzo vingine vya mapato ili iweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Bega aliwataka madiwani hao kupita vijijini kuwaelemisha wananchi umuhimu wa hifadhi ya Serengeti ili waweze kutambua sheria zilizopo ambapo itasaidia kuacha kuingia hifadhini kuondoa uwindaji haramu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles