25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO MUHIMU YA KUKUMBUKWA AFCON

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


Didier drogbaMICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) juzi ilianza kwa kishindo kwa wenyeji Gabon kucheza dhidi ya Guinea-Bissau ambao wanashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza, toka mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1957.

Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo kumekuwa na matukio kadha wa kadha kuwahi kutokea.

Hata hivyo, kwa baadhi ya mashabiki, hii ni michuano ya kawaida ya soka, lakini Afcon kwa sasa ni michuano yenye ushindani mkali na yenye wachezaji nyota kama vile, Riyad Mahrez, Sadio Mane na Pierre-Emerick Aubameyang.

Licha ya michuano hii kuanza kutimua vumbi juzi, bado hatujachelewa kuangalia matukio muhimu ya furaha na ya kusikitisha pia ambayo hayasahauliki katika historia ya Afcon.

1994: Timu ya Taifa ya Zambia yafufuka

Aprili 27 mwaka 1993 timu ya taifa ya Zambia ilikuwa safarini kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia nchini Senegal, ndege iliyowabeba ilianguka na kutumbukia baharini mita 500 kutoka mji wa Libreville, Gabon. Wachezaji wote waliokuwa kwenye ndege hiyo walifariki.

Mwaka mmoja baadaye, Zambia ilijijenga vema na kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mataifa Bingwa Afrika 1994. Walifika fainali ingawa walitolewa na Nigeria kwa mabao 2-1.

2010: Basi la Togo lashambuliwa

Basi la timu ya taifa ya Togo lilishambuliwa na watu wenye silaha  wakati timu hiyo ilipokuwa ikirejea kambini Angola.

Tukio hilo lilitokea Januari 8 mwaka 2010 katika eneo liitwalo Candiba nchini Angola ambapo kundi linalojiita ‘Front for the Liberation of the Enclave of Candiba (FLEC)’, lilitajwa kuhusika na shambulio hilo.

Watu watatu waliuawa na wengine tisa kujeruhiwa. Nyota wa zamani wa Arsenal na Manchester City, Emmanuel Adebayor, ni miongoni mwa waliokuwa kwenye basi hilo.

2002/04: Jezi za maajabu za Cameroon

Mwaka 2002 katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika nchini Mali, timu ya taifa ya Cameroon walichukua Kombe la Afcon kwa kuifunga Senegal katika fainali kwa mikwaju ya penalti.

Lakini habari kubwa ya Cameroon ilikuwa ni kuhusu jezi zao, timu hiyo ilienda katika mashindano na jezi zilizokuwa katika mtindo wa singlendi (vesti) jezi ambazo baada ya mashindano Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) walizipiga marufuku.

Mwaka 2004 tena Wacameroon walitinga katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Tunisia wakiwa na jezi za ajabu zaidi zikiwa kwenye mtindo wa ‘Jump Suti’ yaani fulana na bukta zimeshikana, Fifa hawakukubali wakawakataza mara moja kuacha kutumia jezi hizo, safari hii Fifa wakiwapiga faini ya dola za Kimarekani 154,000 ambayo ililipwa na watengenezaji wa jezi hiyo kampuni ya Puma.

2006/12: Drogba ashinda amani Ivory Coast

Mshambuliaji wa Ivory Coast, Didier Drogba, alikuwa mahiri sana uwanjani kwa timu yake ya taifa na klabu wakati huo akicheza timu ya Chelsea na pia alitumia hadhi yake kufanikisha amani nchini mwake.

Wakati wa vita kati ya 2002 na 2007, alipiga magoti moja kwa moja kwenye runinga akiwa na wachezaji wenzake 2004 kuwahimiza waliokuwa wanapigana kuweka chini silaha.

Kipindi cha amani kilifuata. Mwaka 2008, alisisitiza mechi ya kufuzu Kombe la Taifa Bingwa Afrika ichezewe ngome ya zamani ya waasi Bouake kama wito kwa raia kuungana.

Mwaka 2006 na 2012, Drogba alisaidia taifa lake kufika fainali za Kombe la Mataifa Bingwa Afrika lakini wakashindwa kwa mikwaju ya penalti.

2015: Hofu ya ebola

Kupitia msemaji wao, Mohamed Ouzzine, Morocco walisema kutokana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hawataweza kuandaa mashindano hayo kutokana na kuenea kwa kasi virusi vya ebola, ugonjwa uliokuwa unasambaa kwa kasi Afrika Magharibi.

Baada ya Morocco kujitoa kuandaa mashindano hayo yalihamishiwa nchi ya Equatorial Guinea.

Aidha, kitendo cha Morocco kujitoa kuandaa Afcon, Shirikisho la Soka Africa (CAF) liliwapiga faini ya dola milioni tisa na kuwafungia kwa mashindano yaliyofuata ya Afcon adhabu ambayo Chama cha Soka cha Morocco kiliipinga.

2012: Zambia wabeba Afcon

Miaka 19 baada ya ajali ya ndege iliyoua wachezaji wao wote hatimaye Zambia wanalibeba Kombe la Afcon katika uwanja wa Stade d’Angonje.

Uwanja wa Stade uko mji wa Libreville ambao ndio ajali iliyoua wachezaji wa Zambia mwaka 1993 ilitokea.

Hatimaye Zambia walifanikiwa kuchukua kombe katika mji huo wakiipiga Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti.

Msisimko sana kuwahi kuuona kwani wachezaji wa Zambia wengi walibubujikwa na machozi, nahodha wa Chipolopolo, Joseph Musonda, aliumia dakika ya 11 tu ya mchezo huo na kushindwa kutembea.

Wakati mchezo huo unamalizika kocha wa timu hiyo alimbeba Musonda mikononi na kumpeleka hadi katikati ya uwanja aweze kushangilia ubingwa na wenzake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles