MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
KOCHA wa Lipuli FC, Seleman Matola, amefichua siri ya kikosi chake kuendelea kukusanya pointi tatu katika Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.Lipuli imefanikiwa kukusanya pointi tisa kupitia michezo yake mitatu mfululizo ambayo ni dhidi ya Mbeya City iliposhinda mabao 2-0 ugenini, ikaizamisha Ruvu Shooting kabla ya kuitungua Biashara United.
Akizungumza na MTANZANIA, Matola alisema sare
waliyopata dhidi ya Simba Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, iliwaongezea
ujasiri wa kupambana wachezaji wake katika michezo iliyofuata na kufanikiwa
kushinda michezo hiyo mitatu mfululizo.
“Kwa sasa Lipuli tupo vizuri baada ya kupata
sare na Simba kuna nguvu mpya ambayo imeingia kwa wachezaji, kwa sasa
wanajiamini na kutumia uwezo wao wote wakiwa uwanjani hali inayosaidia kuweza
kupata matokeo hivyo bado moto hauzimwi kwa sasa.
“Tumejipanga kufanya vizuri katika michezo yetu yote tutakayocheza kwa
sasa, hilo linawezekana kwani mpira ni mchezo ambao hauwezi kuficha matokeo
yake yanapatikana uwanjani, mashabiki waendelee kutupa sapoti,” alisema
Matola.
Lipuli inakamata nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na
pointi 22, baada ya kushuka dimbani mara 17, ikishinda michezo mitano, sare
saba na kupoteza michezo mitano.