30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Balozi Adadi apania kuirudisha Muheza kwenye chati

Mbunge wa Jimbo la Muheza, Balozi Adadi Rajabu akipiga mpira kuashiria ufunguzi wa Ligi ya Wilaya  ya Muheza ambayo yeye ni mdhamini jana.

OSCAR ASSENGA, MUHEZA

MBUNGE wa Muheza, Adadi Rajabu, amesema ndoto yake ni kuhakikisha wilaya hiyo inakuwa na timu itakayokuwa tishio katika soka hapa nchini.

Akizungumza jana mjini hapa wakati wa uzinduzi wa ligi ya soka Wilaya ya Muheza ambayo yeye ameifadhili, Balozi Adadi, alisema anaamini vipo vipaji  wilayani humo ambavyo kama vitaendelezwa vitakuja kuwa na faida kwa taifa siku za mbeleni.

“Kama unavyojua madhumuni makubwa ni kuibua vipaji Muheza, hapo zamani tulikuwa tunatisha kwenye soka bahati mbaya hatukuweza kufika mbali kupitia Muheza Shooting na Muheza United ambazo tuliona zinaweza kutupeleka huko, lakini kipindi hiki tuna ndoto kubwa za kufikia huko,” alisema Balozi Rajabu.

Mbunge huyo alisema anaamini kupitia mashindano hayo vitaibuliwa vipaji vikubwa vitakavyokuja kupata mafanikio kama ilivyo kwa mshambuliaji wa timu ya KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao wameitangaza nchi kupitia soka.

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Muheza, Mohamed Moyo ambaye alishiriki uzinduzi wa ligi hiyo, aliwataka viongozi wa Serikali Wilaya ya Muheza kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanahifadhiwa, ili kuwawezesha vijana kuonyesha vipaji vyao ambavyo vitakuwa ni hazina kwa Taifa kwa siku zijazo.

Alisema hawatakubali maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanatolewa kwa wawekezaji.

“Kwa kweli sisi kama Chama Cha Mapinduzi (CCM), hatutakubali kuona maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya michezo yanavamiwa na wawekezaji na kuwakosesha fursa vijana kushiriki michezo, tuhakikishe tunadhibiti hali hiyo,” alisema Moyo.

Aliwataka wachezaji watakaoshiriki ligi hiyo kutambua kwamba, hawawezi  kufikia malengo yao iwapo wataingiza ushirikina katika michezo, badala yake waongeze juhudi katika mazoezi.

“Tunamshukuru mbunge wetu jinsi anavyotekeleza ilani ya 2015-2020, wakati anagombea aliahidi kusimamia masuala ya michezo, kitendo anachofanya ni utekelezaji wa ilani hiyo kwa sababu anasisitiza michezo kwa vijana,” alisema.

Mshindi wa kwanza katika  mashindano hayo atapata Sh 500,000, kombe na jezi seti moja, mshindi wa pili Sh 300,000 na mbuzi, mshindi wa tatu Sh 100,000 na mbuzi, wakati zawadi nyingine zitatolewa kwa mfungaji bora, kipa bora, mchezaji bora na mwamuzi bora wa mashindano.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,688FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles