ROMA, ITALIA
MATAIFA yenye nguvu duniani yamekutana mjini hapa jana kujadili mustakabali wa Shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi wa Palestina (UNRWA).
UNRWA linalokabiliwa na changamoto kubwa baada ya Marekani kusitisha ufadhili wa mamilioni ya dola.
Kamishna Mkuu wa shirika hilo, Pierre Krahenbuhl amesema wana fedha za kutosha kuendeshea shule na kusimamia utoaji wa huduma za afya hadi Mei mwaka huu.
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umeahidi kutoa dola milioni 60 pekee kwa shirika hilo mwaka huu, ikilinganishwa na dola milioni 360 mwaka uliopita.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanazitaka nchi za Ulaya kuingilia kati kuziba pengo lililopo, lakini wanaendelea kuchangisha fedha katika mataifa ya Ghuba.