26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

MASWALI MAZITO MLIPUKO OFISI ZA MAWAKILI

Na MWANDISHI WETU – dar es salaam

TUKIO la ofisi za Kampuni ya uwakili ya IMMMA zilizoko Upanga, Dar es Salaam kulipuliwa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, limezongwa na maswali mengi.

Kitendo hicho kilichodaiwa kutokea usiku wa kuamkia jana kati ya saa 7:40-8:00, kimeacha sintofahamu si tu kwa mawakili wa kampuni ya IMMMA bali pia majirani wa eneo hilo.

Akizungumza eneo la tukio jana, Mkurugenzi Mtendaji wa IMMMA Advocates, Sadoc Magai, alisema bado hafahamu kilichotokea, na kwamba wanasubiri uchunguzi wa polisi.

Akielezea namna alivyopata taarifa, Magai alisema alipigiwa simu na kufika eneo la tukio jana saa 11 alfajiri.

“Saa 11 asubuhi tulikuja, tukakuta polisi wapo tayari hapa. Majirani wanasema tukio lilitokea saa 7 usiku. Jengo limekuwa ‘damaged’ (limeharibiwa), hatujui sababu, hatujui nini kimetokea, huko ndani kuta zimevunjika, milango ambayo ‘partition’ yake (imegawanywa) ni vioo imebomoka,” alisema Wakili Magai.

Magai alisema katika tukio hilo walielezwa na polisi kuwa walikuta madumu yenye petroli ambayo hawakuyataja idadi.

Kwa mujibu wa Magai, polisi pia waliwaarifu kuwa walinzi wao wawili wa Kampuni ya Knight Support waliokuwa wanalinda ofisi hizo siku ya tukio, nao walikutwa wametupwa eneo la Kawe wakiwa hawajitambui, mithili ya watu walioleweshwa dawa.

“Kulikuwa na madumu ya petroli yamezunguka huko ndani, Mkuu wa Polisi Ilala alikuwa hapa, sijajua chanzo. Polisi wanasema walinzi waliwakuta Kawe, hatujaongea nao bado ila wana-‘recover’ kwani walipewa dawa, walipelekwa Muhimbili,” alisema Magai.

Alisema bado hawajajua kilichoibwa kwa kuwa ofisi nyingine zilikuwa zimefungwa, huku fedha, kompyuta na simu zilizoachwa na wafanyakazi zikikutwa kama zilivyoachwa.

“Kompyuta zipo, vitu vingine kama simu, hela ambazo ‘staff’ waliacha zilikuwa juu kama zilivyoachwa,” alisema Magai.

Alisema katika tukio hilo ambalo mlango mkubwa wa kuingilia ofisini humo ulibomolewa kwa kitu hicho kinachosadikika kuwa ni mlipuko wa bomu, hakuna aliyejeruhiwa.

“Hakuna majeruhi zaidi ya athari za jengo, jengo hili lina ofisi za mawakili 25,” alisema Magai.

Akijibu swali la waandishi iwapo kuna wanayemuhisi kuhusika na tukio hilo, Magai alisema hakuna na kwamba anaviachia vyombo vya uchunguzi kufanya kazi yake.

“Hatuna ugomvi, sisi tunatetea, hatujui chanzo, tunaachia polisi, ni tukio limetokea na linaweza kutokea popote,” alisema Magai.

Ingawa alikataa kuhusisha tukio hilo na shughuli zao za uwakili, akisema kuwa kesi wanazozishughulikia ni zaidi ya 200, lakini miongoni mwa kampuni kubwa wanazozitetea katika kesi mbalimbali za madai ni ile ya uchimbaji madini ya Acacia.

Acacia ambayo inamilikiwa kwa kiwango kikubwa na Kampuni ya Barrick Gold Cooperation, ipo katika mazungumzo na Serikali kuhusu mzozo wa madini yaliyomo kwenye mchanga unaochimbwa katika migodi iliyowekeza hapa nchini.

Kesi nyingine iliyovuta hisia za watu inayotetewa na mmoja wa mawakili wa IMMMA, Fatma Karume, ni ile ya uchochezi inayomkabili Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.

Fatma ambaye aliibua mjadala kutokana na kumtetea Lissu, ni mtoto wa Rais wa zamani wa Zanzibar, Amani Karume.

“Hakuna uhusiano na kesi tunazozisimamia, sisi tunasimamia kesi nyingi za madini. Sisi ni mawakili wa Acacia tangu 2012 na hatutaki kuhisi, sitaki kuhisi, sisi ni ‘professionals’, tunaenda na utaratibu, tunaisubiri polisi. Msiseme kuwa wame-‘target’ mawakili, ni uongo,” alisema Magai.

Alisema uchunguzi huo wa polisi unahusisha pia kamera za ulinzi (CCTV) ambazo zilikuwa zimefungwa katika ofisi hizo.

 

JESHI LA POLISI

MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Lucas Mkondya, ambaye alisema taarifa zaidi zitatolewa baada ya uchunguzi.

“Hatuna uhakika kama ni bomu, ni mlipuko ulitokea na umesababisha uharibifu. Hatujajua, bado tunaendelea na uchunguzi, polisi bado tuko eneo la tukio. Hata hao askari siwezi kuwazungumzia hadi uchunguzi utakapokamilika,” alisema Kamanda Mkondya.

 

KAULI ZA MAJIRANI

Mmoja wa majirani anayeishi takribani mita 100 kutoka jengo hilo, alisema alisikia vishindo viwili majira ya saa 7:40 usiku.

“Nilisikia kishindo, lakini cha pili ndio kilikuwa kizito zaidi, pale nyuma utaona (akionyesha nyuma kulikoharibika) rangi zilibanduka na kuanguka chini,” alisema jirani huyo – raia wa kigeni, ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake.

Raymond Mrope ambaye ni mlinzi katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Immaculata Upanga, ambalo lipo karibu na ofisi hizo, alisema wao waliingia asubuhi kupokea lindo kutoka kwa wenzao, ambao waliwasimulia walichoshuhudia wakati tukio hilo likitekelezwa.

“Waliolala usiku wanasema watu watatu walifika wakiwa na gari mbili aina ya Land Cruiser, mmoja alisimama kwenye huu ‘mstimu’ (akionyesha nguzo ya umeme), mwingine getini na mwingine upande wa barabara, jamaa walikuwa ‘fasta’ (haraka), nasikia dakika chache walionekana wanaingiza gari kinyumenyume na kupakia maboksi,” alisema Mrope.

Wakati Mrope akisema hayo, majirani wa jengo la upande wa pili ambalo nalo limeharibika kwa kuvunjika vioo na ‘ceiling board’ kushuka, walishindwa kuzungumza vyema na gazeti hili.

 

NDANI YA OFISI

MTANZANIA Jumapili ambalo lilifika eneo la tukio, lilishuhudia magari mawili ya polisi yakiwa mwanzo mwa barabara ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa imefungwa kwa utepe wa rangi ya njano wenye maandishi “Usipite eneo la tukio”.

Awali polisi waliokuwa wametanda kila pembe ya eneo hilo, waliwazuia waandishi wa habari kuvuka utepe mwingine uliokuwa upande huo ambao uliondolewa saa 10:37 asubuhi.

MTANZANIA Jumapili lilishuhudia polisi zaidi ya 30 wakiwa eneo la tukio na magari ya polisi na binafsi zaidi ya 10, likiwamo lenye maandishi yanayosomeka ‘Crime Scene Investigation’.

Baada ya polisi kupungua, walifika askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) watatu walioingia ndani na kuzunguka eneo hilo huku wakizungumza na viongozi wa IMMMA.

 

HALI YA JENGO

Ingawa polisi hawakuruhusu waandishi kuingia ndani, mwandishi wa MTANZANIA Jumapili alishuhudia jengo hilo la IMMMA lenye ghorofa mbili likiwa limeharibika vibaya, hususani upande wa madirisha.

Jengo hilo lenye namba 357, vioo vya madirisha vilikuwa vimevunjika, huku ‘ceiling board’ zikionekana kubomoka na kuanguka chini.

Kwa sababu hiyo, nyaraka mbalimbali zilizokuwa kwenye makabati ndani ya ofisi hizo zilikuwa zikionekana kama ziko nje.

Mwandishi wa MTANZANIA Jumapili alifanikiwa kuchungulia kwa nyuma na kuona kitu kama ukungu wa moshi wa mafuta, huku gari moja ambalo kibao cha namba zake za usajili kikiwa kimeanguka chini, likionekana kuvunjika kioo cha nyuma.

Pamoja na kuangalia vyema, lakini ilishindikana kujua aina ya gari hilo wala namba hizo kusomeka vyema.

Upande wa mbele wa jengo ulionekana kuwa wazi kutokana na uharibifu, huku kukiwa na vioo vilivyovunjika na mashuhuda waliozunguka nyuma waliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kumeharibika vibaya zaidi.

Mlipuko huo haukuishia IMMMA, bali uliharibu pia jengo la jirani la Reliance Insurance Company (T) Ltd ambalo nyuma yake pia kuna makazi ya watu.

Mmoja wa wakazi wa jengo hilo, alisema waliona moto na moshi baada ya kishindo hicho na kusababisha watu kukimbia hovyo kwa taharuki.

“Tuacheni tupumzike, tumekimbia hovyo, tulichanganyikiwa, tuliona moto na moshi mkubwa baada ya kishindo,” alisema shuhuda huyo.

 

UTATA

Bado kuna utata juu ya kifaa kilichotumika kulipua ofisi hizo za kampuni kubwa ya uwakili hapa nchini.
Mtaalamu mmoja wa milipuko, aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa kama ni bomu limetumika kulipua eneo hilo, bado kwa kiasi kikubwa linaweza kuwa ni lile la ‘Defensive’ (kujihani).

“Mabomu yapo ya aina nne, kuna ‘Defensive’, hili ni la kujihami, wahalifu wengi wanapenda kulitumia kutokana na urahisi wake, ‘Offensive’ la kushambulia, hili ni hatari kidogo kwani linawaka moto kabla ya ku-‘burst’, halafu lipo ‘Stick and hand grenade’ na ‘RPG’. Hili RPG ni kali linashusha ghorofa lote, hivyo kwa vyovyote litakuwa limetumika Defensive,” alisema.

Akielezea sifa za bomu hilo, alisema lina uzito wa kilo mbili na nusu na mara nyingi likipigwa huathiri umbali wa mita 200.

Alisema lina pini na kwamba huwezi kulirusha pasipo kuichomoa.

Katika uchambuzi wake huo, mtaalamu huyo alisema kama bomu hilo limetumika, basi yanaweza kuwa yametumika mawili kwa sababu ya athari ambayo imeonekana katika eneo hilo.

Alisema ni mapema kujua pia kama wahalifu walitumia petroli kwani kama ndivyo pia wangesababisha moto mkubwa.

 

TUKIO LAIBUA MASWALI

Tukio hilo limeibua maswali makubwa manane kutoka kwa wadadisi wa mambo.

Ni akina nani waliotekeleza kitendo hicho cha kigaidi? Je, lengo la walipuaji hao ni nini? Ni aina gani mlipuko uliotumika kulipua ofisi hizo na kwa nini waliutumia?

Je, maboksi yanayodaiwa kuchukuliwa yalikuwa na nini? Kwanini iwe IMMMA? Na kwa nini walipuaji hawakuchukua kitu cha thamani kama kompyuta, simu au fedha kama lengo lao lilikuwa ni kujipatia kipato?

Je, ni kitu gani walichopewa walinzi hadi kulewa na waliwachukua vipi hadi Kawe? Je, polisi waliwatambua vipi kama walinzi hao waliokotwa Kawe ni wa Kampuni ya IMMMA? Rejea kauli ya Magai kwamba aliambiwa na polisi kwamba walinzi hao wamepelekwa Muhimbili na kwamba yeye alikuwa hajawaona.

 

MUHIMBILI

MTANZANIA Jumapili lilifika Hospitali ya Taifa Muhimbili ili kujua hali za walinzi hao, lakini halikuweza kupata ruhusa kutoka ofisi za uhusiano ambazo zilikuwa zimefungwa.

 

TLS

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, amelaani kitendo hicho akisema kuwashambulia mawakili wanapotekeleza majukumu yao ni kosa kubwa.

“Nakwenda kikao cha Baraza la Uongozi, hatujui ni kina nani, tutazungumza baada ya kikao,” alisema Lissu.

 

THRDC

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema kuwa wamesikitishwa na tukio hilo.

“Tunatambua kuwa wanasheria ni kundi kubwa katika makundi ya watetezi wa haki za binadamu hapa nchini na duniani kote.  Wanasheria husaidia wananchi kupata haki zao kwa njia za amani, pia ni watetezi wakubwa wa katiba na utawala wa sheria,” alisema Olengurumwa.

Alisema kitendo chochote kinachozua hofu katika kundi hilo madhara yake ni makubwa kwa taifa na katika mfumo wa utoaji haki.

 

CUF

Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kimelaani tukio hilo kupitia Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Mahusiano na Umma, Mbarala Maharagande.

Katika taarifa yake, Maharagande alisema chama hicho kinaungana na mawakili na wafanyakazi wote katika kipindi hicho kigumu cha uharibfu wa mali na vitendea kazi.

“Tunatambua mchango mkubwa wa Kampuni ya IMMMA na mawakili wake katika kutetea na kupigania haki, usawa, demokrasia na kufuatwa kwa utawala wa sheria katika nchi yetu,” alisema Maharagande.

Alisema IMMMA iliyoanzishwa mwaka 1997 ikiwa na washirika (Partners) saba na mawakili 15, mawakili wake wanamwakilisha Ally Salehe (Mbunge wa CUF – Jimbo la Malindi, Zanzibar) katika shauri la madai dhidi ya RITA na Bodi ya Lipumba (Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Ibrahim) na wenzake.

“IMMMA wanamtetea Lissu na ni mawakili washirika wa DLA Piper ya Uingereza wakiwa upande wa Kampuni ya Acacia Mining dhidi ya Serikali ya Tanzania katika sakata la makinikia linaloendelea hivi sasa nchini. Wakili Magai ni mweka hazina wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS),” alisema Maharagande.

Alisema Jeshi la Polisi lichukue hatua haraka mara baada ya uchunguzi na kutoa taarifa kwa umma nini chanzo cha mlipuko huo.

 

CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupitia Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, kilisema kinafahamu kuwa kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa mawakili wana haki ya kufanya kazi zao kwa uhuru na faragha wakati wa kutoa huduma zao kwa wateja na wananchi kwa ujumla.

Mrema alisema uvamizi huo unakiuka misingi ya sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za mawakili na kwamba vyombo vya dola vinapaswa kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahusika wanapelekwa kwenye vyombo vya sheria.

 

MATUKIO YA MILIPUKO

Hii si mara ya kwanza kutokea kwa milipuko nchini.

Tukio la hivi karibuni ni lile la bomu la petroli lililotokea nyumbani kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, Magomeni Ndugumbi, Dar es Salaam.

Jingine ni lile la Mei 5 mwaka 2013, katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti mkoani Arusha, ambako bomu lilirushwa na kusababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi 70.

Juni 14, mwaka huo huo, katika viwanja vya Soweto wakati wa mkutano wa kampeni za Chadema za uchaguzi mdogo wa kata nne za Themi, Elerai, Kaloleni na Kimandolu, watu wanne walifariki na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa naada ya kutokea mlipuko.

Matukio yanayofanana na hayo pia yamewahi kuripotiwa mara kwa mara kutokea visiwani Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles