29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mashine za EFDs kujadiliwa kimataifa

Mashine za EFD
Mashine za EFD

RUTH MNKENI NA RAPHAEL NOLESCUS (TUDARCO), DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema Mkutano Mkuu wa Kodi utasaidia kujadili changamoto za mashine za kielektroniki za EFDs na jinsi ya kuzitatua.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade, alisema mkutano huo unaojumuisha nchi mbalimbali una lengo la kujadili namna ya kuimarisha taasisi za kodi nchi za Afrika.

Alisema mashine za EFDs zipo kwa mujibu wa sheria, hivyo mamlaka hiyo itaendelea kuzisimamia hadi sheria itakapokuwa na mabadiliko.

“Sheria ya sasa inasisitiza matumizi ya mashine za EFDs, hivyo ni wajibu wa TRA kuendelea kusimamia matumizi yake pamoja na kwamba kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza,” alisema Bade.

Hata hivyo, alisema kwamba mkutano huo utasaidia kuwajengea uwezo watumishi katika taasisi za kodi, kubadilishana uzoefu wa ukusanyaji wa kodi katika sekta mbalimbali pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za biashara za kimataifa na uwekezaji katika nchi za Afrika.

Aidha alisema mada zitakazozungumziwa ni pamoja na uongozi katika ajenda ya kodi kimataifa, kuzingatia uweledi, kanuni na misingi bora ya utawala na usimamizi wa kodi.

“Kaulimbiu ya mkutano huu ni kujadili namna ya kuimarisha taasisi za kodi Afrika, kujenga uwezo wa watumishi katika taasisi za kodi, kubadilishana uzoefu wa ukusanyaji kodi pamoja na kubadilishana taarifa muhimu za biashara za kimataifa na uwekezaji katika nchi za Afrika,” alisema Bade.

Aidha alisema mgeni rasmi katika mkutano huo utakaoanza Septemba 15 hadi 19, atakuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Alisema mkutano huo utajumuisha nchi 37 ambazo ni pamoja na Benin, Botswana, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Chad, Kenya, Uganda, Rwanda, Namibia, Nigeria, Misri, Liberia, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Tanzania na nyinginezo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles