22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Mongela aibukia Chadema

Kada wa CCM, Balozi Getrude Mongella, akisalimiana na mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Hawa Mwaifunga (kulia), wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix
Kada wa CCM, Balozi Getrude Mongella, akisalimiana na mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA), Hawa Mwaifunga (kulia), wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa baraza hilo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Fidelis Felix

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Gertrude Mongela, ameibukia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAWACHA), na kueleza kwamba wanawake wanatakiwa kushirikiana bila ya kujali vyama vyao.

Akihutubia katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, jana, Mongela aliyepata kuwa Mbunge wa Ukerewe kwa muda mrefu kwa tiketi ya CCM, aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa wahakikishe wanajua kwamba wanawake hawatakiwi kubaguana.

“Hata nilipokuwa Beijing nilikuwa nikiwaeleza mara nyingi wanawake kuwa ni kitu kimoja na hatupaswi kubaguana pasipo kuangalia taasisi uliyotoka,” alisema.

Mongela alisema kuwa katika mapambano yake alijali zaidi kuona nchi za Afrika zinaondoa dhuluma na kuwapa haki wanawake wote.

“Wanawake wanatakiwa kuungana kupigania haki zao kwa sababu hakuna leba za wanawake wa Chadema wala leba za wanawake wa CCM,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliwataka wanawake wenye ndoto ya kuwania Bawacha kwa nia ya kupata Ubunge wa Viti Maalumu waondoe fikra hizo.

Pia aliwashukia wale wenye nia ya kuingia Bawacha kwa nia ya maslahi binafsi, kwamba watambue kuwa nafasi hiyo haitakuwapo.

Mbowe alikemea tabia aliyosema imejengeka kwa wanawake wengi waliobweteka kwa kusubiri kupewa viti maalumu na kuacha kwenda majimboni kugombea.

“Wanawake wamekuwa na ulemavu wa kudumu wa kutaka viti maalumu na si kushindana majimboni, na wasifikirie unyonge wa kupewa na badala yake wapambane majimboni.

“Siri ya ushindi wa nafasi mnazowania isiwe rushwa na badala yake iwe ubora, mikakati na tabia njema kwani chama hakitaendelezwa kwa majungu fitina na kubezana,” alisema Mbowe.

BAVICHA

Katika hatua nyingine Patrobas Paschal, amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Chadema (Bavicha).

Mwenyekiti huyo amechaguliwa katika uchaguzi uliofanyika juzi usiku katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, kunakoendelea Uchaguzi Mkuu wa Chama hicho taifa.

Akitangaza matokeo hayo jana, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa, ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi wa vijana, Hashim Issa, alisema Patrobas alishinda kwa kupata kura 173 dhidi ya mpinzani wake Upendo Peneza aliyepata kura 70.

Hata hivyo, uchaguzi huo ulifanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza Peneza aliibuka kidedea kwa kupata kura 68 na Patrobas kuambulia kura 61.

Msimamizi huyo wa uchaguzi alifafanua kuwa kufanyika kwa uchaguzi wa awamu ya pili ni baada ya mshindi kutopata asilimia 50 ya kura.

Issa alisema nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara iliyokuwa ikiwaniwa na wagombea 11, ilichukuliwa na Patrick Ole Sosopi aliyepata ushindi kwa kura 128 dhidi ya mpinzani wake Jesca Kiskwa aliyepata kura 110.

Alisema kwa upande wa Zanzibar, katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliyokuwa na wagombea watano, Zeudi Abdallah ametangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 126 dhidi ya Shabani Omary Shabani aliyeambulia kura 69.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles