Patricia Kimelemeta na Grace Shitundu
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetoa ufafanuzi kuhusu ununuzi wa mashine za Biometric Voter Registration (BVR) ambazo zitatumika kwa ajili ya kuwaandikisha upya wapiga kura kuanzia Septemba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba, alisema kuwa mashine hizo zimenunuliwa kwa Dola za Marekani 89,094,407 na kampuni ambayo ilishinda zabuni kwa mujibu wa sheria.
Alisema zabuni ya awali ya ununuzi wa mashine hiyo ilitangazwa Januari, 2013 ambapo kampuni sita zilijitokeza na kuomba kazi hiyo ya ununuzi wa mashine hizo.
“Januari 2013 tulitangaza zabuni ya ununuzi wa mashine ya BVR ambapo kwa mujibu wa sheria za manunuzi, zabuni hiyo inaiva baada ya siku 45 ndipo zilipojitokeza kampuni sita,” alisema Malaba.
Alisema baada ya kushindanishwa, muunganiko wa kampuni tatu za M/S SCI Tanzania, INVU IT Solution ya India na The Jazz Matrix Corporation ya Australia zilishinda zabuni hiyo.
Malaba alisema baada ya kampuni hizo kushinda zabuni, kampuni ya M/S Safran Morpho ilikata rufaa ya mshindi wa zabuni hiyo.
Alisema katika manunuzi ya awamu ya pili waliamua kuziita kampuni zote na kuangalia mashine zao kwa sababu muda ulikuwa umekwenda kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa na NEC.
Alisema kutokana na hali hiyo waliwaita wataalamu wa Tehama kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ili kuangalia ubora wa mashine hizo.
Alisema sheria ya manunuzi inawaruhusu kutumia njia hiyo kwa kutumia mfumo wa ‘single sourcing’.
“Baada ya wataalamu kujiridhisha na mashine zilizoonyeshwa, bodi ya zabuni ya tume iliteua kampuni ya Lithotech Export ili ifanye mchakato wa mashine hiyo. Kutokana na hali hiyo NEC ilinunua mashine hizo kwa dola za Marekani 98,094,407 pamoja na gharama za vifaa vingine vinavyofungwa kwenye mashine hiyo.
“Katika mchakato huu tumenunua mashine 10,500 ambazo zitatumika katika uandikishaji wa wapiga kura katika maeneo mbalimbali ya nchi,” alisema Malaba.
Mkurugenzi huyo wa NEC alisema kutokana na hali hiyo ya ununuzi wa mashine hizo, tume yake ilifuata taratibu za kisheria pamoja na kampuni kushindana kwa zabuni zilizotangazwa kwa mujibu wa utaratibu, sheria na kanuni za manunuzi.
Sakata la ununuzi wa mashine hizo liliibuliwa mwishoni mwa mwaka jana na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ambaye aliitaka ufanywe uchunguzi kuhusu zabuni ya ununuzi wake.
Ni vema kuwa na teknolojia mpya katika uchaguzi ujao, lakini cha msingi, je wadau wengine kama vile vyama vingine vya kisiasa walishirikishwa katika mchakato wa ununuaji mashine hizo. Kaktika siasa za vyama vingi, jambo kama hili ni lazima liwe wazi hasa kutokana na malalamiko yaliyopo kwamba chama tawala wanaiba kura ,hawashindi kihalali. Ukitaka kumaliza majungu na fitina, ni lazima uwe jasiri kuweka mambo yako wazi, lakini bado kuna agenda za siri unaofanywa na NEC katika uendeshaji wa shughuli zake. Watanzania tunaendelea kuwa na wasi wasi na uhuru na uchaguzi ulio haki katika chaguzi zijazo. CCM wanajua wanachofanya, na Nec bado wanashikilia ndoa yao na serikali ya CCM. Dawa ni moja kuunda Tume huru ya uchaguzi ambayo haitakuwa ya kuteuliwa na Rais. Mpaka tume huru iwepo madarakani, bado uchaguzi hautakuwa huru na wa haki. Tunakuza demokrasia au tunaendelea kuibomoa?