27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Sumaye: Mimi ni tumaini la Watanzania

Frederick Sumaye
Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye

Na Sitta Tuma, Mwanza

WAZIRI Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, amesema yeye ni tumaini la Watanzania na mpambanaji wa vita dhidi ya maovu.

Kutokana na hali hiyo, amesema ni jemadari hodari aliyeungana na askari wapiganaji hodari wa vita ambao wataleta ushindi usio na shaka.

Kauli hiyo aliitoa jijini Mwanza jana, katika hotuba yake ya uzinduzi wa taasisi ya Vijana ya Tanzania Youth (TYDC), ambako alipinga hatua ya baadhi ya wanasiasa kununua wapiga kura kwenye uchaguzi na kufanikisha kitendo hicho ni sawa na uroho wa madaraka.

Alisema hali hiyo ni hatari, kwani wanasiasa wa aina hiyo wanapaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu, wanaweza kulisambaratisha Taifa.

Sumaye ni mmoja wa makada sita wa CCM waliopewa onyo kutokana na kile kilichoelezwa kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya uzinduzi wa taasisi hiyo, Sumaye alisema yupo tayari kugombea urais iwapo ataombwa kufanya hivyo.

Akijibu maswali kwa waandishi wa habari, alisema dhamira yake katika kujitosa kuwania urais ipo, lakini pale atakapoombwa kugombea.

“Nikiombwa kugombea urais nitagombea, hilo wala halina tatizo…na mjue kutangaza nia siyo kosa kwa mujibu wa kanuni za CCM, ila kosa ni kufanya kampeni kabla ya muda, wakati rais anapomaliza muda wake wagombea wengi hujitokeza kuwania nafasi hiyo, sasa hata mimi nikiombwa nitagombea,” alisema Sumaye.

Sumaye, anayetajwa kuwa miongoni mwa wanasiasa ndani ya CCM wanaotaka kuwania urais mwaka 2015, akizungumza katika uzinduzi huo wa TYDC, alisema kuna watu wamekuwa wakitumia nguvu ya fedha kusaka madaraka na kuwafananisha na watu wafupi wanalazimisha kupanda juu ya stuli ili waonekane mbele ya jamii kwa kutumia nguvu kubwa ya fedha.

Alisema watu hao ni hatari iwapo wakichaguliwa na kushuka juu ya stuli kwa vile hawataonekana tena kuwasaidia wananchi na kubainisha wamekuwa wakiwatumia vijana vibaya ili kukidhi malengo yao binafsi, yakiwemo ya kisiasa.

Katika kongamano hilo, Sumaye alitangaza kuwa mlezi wa vijana nchini na kuwaahidi maisha ya matumaini kwa miaka ijayo.

“Mimi nataka niwe mlezi wa vijana wa Tanzania nzima ili wawe na maisha ya matumaini. Ninyi vijana mtu akiwaleteeni hela chukueni kuleni halafu mnamchagua mwingine. Yaani hata Sumaye akileta msikatae hela, chukueni kuleni msimchague, maana mtu anayetumia nguvu ya fedha kusaka madaraka ya Serikali za Mitaa, udiwani, ubunge na hata urais huyo hafai na ni dhaifu,” alisema Sumaye, huku akieleza hakuja kwenye kongamano hilo kwa sababu za kisiasa.

Aliwaasa vijana wote, hususan waliopo masomoni wasidanganyike wala kutegemea kupata ajira za ofisini na kwamba wasiopata ajira wasikubali kutumiwa kisiasa, vijana watakaotumiwa watakuwa wamejiunga katika kundi la wala rushwa na wapokea rushwa, watakuwa wamejiunga kwenye kundi la mafisadi na la maangamizi kwa taifa.

Alisema kwamba vijana ni jeshi muhimu la taifa kwa maslahi ya taifa na wananchi wake na siyo jeshi la kuleta maafa katika jamii, hivyo atakuwa mlezi wa vijana kwa mambo yote na sifa anayoipenda ni mtu kuwa mzalendo wa kweli, kusimamia haki ya umma na siyo maslahi binafsi.

Alisema kwamba, hivi sasa Watanzania wanaelekea kwenye uchaguzi na fedha nyingi zinatembezwa kwa vijana ili watoa rushwa wachaguliwe katika nafasi wanazoomba na kudai siku hizi kumeibuka mtindo wa watoa fedha kuitwa wakarimu na wasiotoa kuhonga wao huitwa wachoyo.

“Mliponitaka niwe mlezi wenu nilikubali kwa sababu mimi ni mpambanaji wa vita dhidi ya matatizo na maovu hayo ambayo TYDC imeyaweka kama malengo yake makuu.

“Hivyo niliona nimepata wapiganaji wenzangu katika vita hii na kwa bahati nzuri wapiganaji wenyewe ni vijana ambao ni wengi, ni wenye nguvu na ndio wenye uchungu na nchi yao. Mimi ninawaahidi kuwa mmempata jemadari hodari wa kuongoza vita hii na yeye jemadari amepata askari mashujaa wa kupigana vita hiyo,” alisema.

Alisema muunganiko huo wa wawili wa jemadari hodari na askari wapiganaji hodari wa vita utaleta ushindi usio na shaka.

“Kama unavyoambiwa wewe na wenzako wengine wasiokuwa na mahesabu nao huambiwa vivyo hivyo. Lakini la msingi ujue kuwa kama mtu anatumia njia hizo za mkato kutaka kuingia madarakani, huyo mtu hajiamini na wala hana uhakika na uwezo wake wa kumudu hayo madaraka anayoyatafuta, vinginevyo asingehangaika kuhonga watu,” alisema Sumaye.

Awali akimkaribisha Sumaye kuzungumza na halaiki ya vijana zaidi ya 300, Mwenyekiti wa TYDC, Lengai Thomas Ole Sabaya, alionekana wazi kumpigia ‘debe’ Sumaye katika harakati zake za kisiasa, kwa kusema wakati wa utawala wake na Mkapa fedha ya Tanzania ilikuwa na thamani kuliko ilivyo leo hii.

Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

Februari 18, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Kamati Ndogo ya Udhibiti na Nidhamu katika kikao chake ilipendekeza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa makada wake ambao wameanza kampeni ya kuwania urais wa mwaka 2015.

Uamuzi huo wa kamati hiyo ya maadili ulibarikiwa na Kamati Kuu (CC) ya CCM, iliyokutana Februari 17, mwaka huu mjini Dodoma, chini ya Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete.

Makada waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa tuhuma za kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati ni January Makamba, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Steven Wassira pamoja na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Katika adhabu hiyo, makada hao walizuiwa kujihusisha na masuala ya kisiasa ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku mwenendo wao wa kisiasa ukifuatiliwa chini ya uangalizi mkali katika kipindi chote cha kutumikia adhabu hiyo.

Kabla ya adhabu hiyo, makada hao waliitwa na kuhojiwa na Kamati Ndogo ya Maadili ambayo iliwatia hatiani kwa kutumia Kitabu cha Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6 (7)(i).

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kimsingi ingefaa kiongozi yeyote aliyewahi kushika madaraka makubwa serikalini hasa Waziri Mkuu, Waziri wa Fedha,Waziri wa Elimu na Waziri wa Maliasili wasipewe nafasi ya kugombea kwa kuwa nafasi hizi ni nyeti sana na wakati wa kipindi chao hawakumshauri Rais ipasavyo. Hawa wanoitwa vijana si vijana – wamekwishavuka ukomo wa ujana, ni vyema wahamasishwe kugombea. Haiwezekani mtu aliyekuwa kwenye uongozi miaka kumi iliyopita alete mabadiliko yoyote. Hizi tamaaa zitaimaliza nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles