27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mashamba kuhakikiwa

  • Lukuvi asema kulikuwa na dalili za upendeleo yalipofutwa 15 likiwemo la Sumaye

Munir Shemweta, Kilosa

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imesema itafanya uhakiki wa mashamba yote yaliyopo Kilosa Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kubaini yale yasiyoendelezwa ili yapendekezwe kufutwa kwa Rais.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu uamuzi wa kuyafuta mashamba 15 likiwamo la Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, ufanywe Agosti 2017.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na  Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alibainisha hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Mvumi wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, alipokwenda kutatua migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo.

Alisema uamuzi wa Wizara yake kuamua kufanya uhakiki wa mashamba yote yaliyopo katika wilaya hiyo, unatokana na kubaini kuwepo dalili za upendeleo wakati wa kupendekeza mashamba 15 yaliyofutwa na Rais.

Kwa mujibu wa Lukuvi, Wilaya ya Kilosa ina jumla ya mashamba 183 na yote yatafanyiwa uhakiki na timu ya wataalamu 15 kutoka wizarani kwa lengo la kubaini mashamba yasiyoendelezwa na kuwasilisha mapendekezo kwake kwa lengo la kuyatolea uamuzi.

Katika hilo alisema mashamba yaliyofutwa ni machache ukilinganisha na hali halisi.

“Wataalamu  wetu wana uwezo wa kufanya kazi kwa weledi bila kumwogopa mtu na wamekuja kukagua mashamba yote hivyo muwape ushirikiano,” alisema Lukuvi.

Alisema Wilaya ya Kilosa inaongoza  kwa migogoro ya ardhi na wizara yake inataka kumaliza migogoro hiyo na kuwataka wananchi wa Kilosa kuwapa ushirikiano wataalamu hao wakati wa zoezi la uhakiki.

Mapema Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira katika Halmashauri ya Kilosa, Ibrahim Mndembo, alisema jumla ya mashamba 15 yamebatilishwa miliki zake katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa mujibu wa Mndembo, mashamba yenye mgogoro na wananchi katika Wilaya ya Kilosa ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza dhidi ya wananchi wa Mabane, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai dhidi ya wananchi wa Ilonga na shamba la Mauzi Estate Malangali.

Agosti 2017, Lukuvi aliutangazia umma kuwa Rais Dk. John Magufuli, amefuta umiliki wa mashamba 14 makubwa yenye ukubwa wa heka 14,341 yaliyokuwa yakimilikiwa na watu mbalimbali wilaya ya Mvomero na Kilosa, mkoani Morogoro.

Alisema hatua hiyo ilitokana na wamiliki wa mashamba hayo kushindwa kuyaendeleza licha ya kutakiwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, ikiwamo kuandikiwa barua kwa mujibu wa sheria.

Miongoni mwa mashamba yaliyofutiwa umiliki ni pamoja na la Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na mkewe Esther lenye ukubwa wa ekari 473.

Mengine ni la Kampuni ya Noble Agriculture Enterprises Limited ambalo mmiliki wake alitambulika kwa jina la Gitu Patel aliyekuwa akimiliki mashamba manne yenye ukubwa wa ekari 2,661.

Waziri Lukuvi alisema mashamba hayo yalifutiwa umiliki kutokana na kushindwa kulipiwa kodi za Serikali kama walivyotakiwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles