29.9 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Ushahidi kesi ya Zitto waendelea kutolewa

PATRICIA KIMELEMETA- DAR ES SALAAM

SHAHIDI wa nne wa upande wa Jamhuri ambaye ni mpelelezi katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, Inspekta Salum Masoud, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Zitto Kabwe, alimkabidhi taarifa ya vyombo vya habari (Press-Release) wakati alipokuwa akimhoji.

Shahidi huyo alieleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na hatua ya ushahidi.

Kesi hiyo ya uchochezi namba 37/2018 inayomkabili Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo,  iliendelea mahakamani hapo jana ambapo upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon na Janneth Magoho, wakati upande wa utetezi umeongozwa na Wakili Peter Kibatala, Dickson Matata na Steven Mwakibolwa.

Wakili Katuga alimwongoza shahidi huyo mahakamani hapo ili aweze kutoa ushahidi wake na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo:-

Wakili Katuga: Shahidi tunaomba uieleze mahakama unafanya kazi wapi na upo hapo kama nani na majukumu yako ni yapi?

Shahidi: Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni, nipo kama msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kinondoni na majukumu yangu ni kusimamia askari wa chini yangu pia  nashughulika na makosa ya jinai na makosa ya mtandaoni.

Wakili Katuga: Upo hapo kwa muda gani?

Shahidi: Tangu Julai, mwaka jana.

Wakili Katuga: Hiyo ofisi ipo wapi?

Shahidi: Ipo katika Kituo cha Polisi Oysterbay kilichopo Mkoa wa Kipolisi Kinondoni.

Wakili Katuga: Oktoba 31, mwaka jana mchana unakumbuka ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa eneo langu la kazi Kituo cha Polisi Oysterbay, nikiwa hapo nilikuwa kwenye shughuli zangu za kiupelelezi alikuja Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi akiwa na Zitto kwa sababu Ofisi ya Msaidizi ipo karibu na Mkuu wa Upelelezi, nilimwona aliingia naye ofisini kwake kwa mahojiano.

Wakili Katuga: Wewe ulijua kwanini Zitto Kabwe yupo hapo na kwa ajili ya nini?

Shahidi: Alikuja kwa ajili ya tuhuma zinazomkabili za uchochezi dhidi ya Serikali, maneno ambayo aliyatoa Oktoba 28, mwaka jana.

Wakili Katuga: Nini kimeendelea?

Shahidi: Nikiwa kama mpelelezi hilo jambo nilikuwa nalifahamu na alikiri kweli kuwa huo mkutano aliufanya basi nikamwomba (Press-Release) ya huo mkutano wake aliofanya na waandishi wa habari.

Hakimu Shahidi: Hapo wakati unamuuliza baada ya mahojiano na RCO au uliingilia kati?

Shahidi: Baada ya kumalizana na RCO nikaomba (Press-Release).

Wakili Katuga: Zitto yupo hapa mahakamani?

Shahidi: Yupo.

Wakili Katuga: Ni yupi?

Shahidi: Ni yule pale aliyekaa kizimbani.

Wakili Katuga: Kwa ridhaa yako hakimu tunamwomba shahidi akamwonyeshe Zitto.

Shahidi alikwenda kumshika bega Zitto aliyesimama baada ya kuona shahidi anakwenda upande wake na mahojiano yakaendelea.

Wakili Katuga: Ni mahojiano ya aina gani yalifanyika kati ya huyu msaidizi wa RCO na Zitto?

Shahidi: Kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari.

Wakili Katuga: Ulikuwa unasikiliza hayo mahojiano?

Shahidi: Nilikuwa nasikiliza.

Wakili Katuga: Na ulimwomba (Press-Release) baada ya Zitto kufanya kitu gani?

Shahidi: Baada ya kukiri kuwa alifanya mkutano.

Wakili Katuga: Baada ya kumwomba hiyo (Press-Release) alijibu nini?

Shahidi: Alijibu haina shida kwa kuwa pale hakuwa nayo alimwagiza kijana wake aje nayo.

Wakili Katuga: Tunaomba uieleze mahakama kama ilitokea ikapatikana?

Shahidi: Baada ya muda kidogo huyo kijana alikuja na hiyo press release na kumkabidhi Zitto.

Wakili Katuga: Wewe kama wewe uliweza kujua hiyo nyaraka imefuatwa wapi?

Shahidi: Hapana sikuweza kujua ila Zitto baada ya kuipitia alisema ndio yenyewe.

Wakili Katuga: Tunaomba ieleze mahakama ilichukua muda gani?

Shahidi: Nilipomwomba haikuchukua muda sana.

Wakili Katuga: Unaweza kukumbuka?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Wakili Katuga: Ulikabidhiwa lini?

Shahidi: Siku hiyo hiyo ya tarehe 31 baada ya hapo nilimwambia aisaini.

Wakili Katuga: Ilikuwa wapi?

Shahidi: Kituoni Oysterbay.

Wakili Katuga: Baada ya hapo?

Shahidi: Mimi baada ya kuipitia nikamwomba aisaini kuwa amenikabidhi hiyo na mimi nikasaini kwa kuwa tulikuwa askari wengi nikamwomba mmoja aje awe shahidi.

Wakili Katuga: Unaweza kumkumbuka huyu mwenzako?

Shahidi: Ndio Gabriel Katengu. Baada ya hapo nikamkabidhi incharge wa upelelezi Albart.

Wakili Katuga: Hiyo unayoita hati ya makabidhiano ya hiyo Press Release?

Shahidi: Ndio, kuna saini yangu na saini ya Zitto.

Wakili Katuga: Kwa ridhaa ya mahakama angalia hiyo nyaraka.

Wakili Katuga: Tunaomba iangalie na kuieleza mahakama kuwa hiyo ndiyo hati ya makabidhiano uliyoitaja?

Shahidi: Ndiyo kuna saini yangu kuna saini ya Zitto.

Wakili Katuga: Tunaomba ieleze mahakama hiyo nyaraka unataka waifanye nini?

Shahidi: Naiomba mahakama hii ipokee nyaraka hii kama sehemu ya kielelezo.

Wakili Katuga: Hiyo Press-Release utaikumbuka?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Katuga: Utaikumbukaje?

Shahidi: Ina kurasa sita, ina nembo ya chama cha ACT na mwishoni kuna saini ya Zitto, ilikuwa na kichwa cha habari ‘Serikali imevuruga zao la korosho, imeshindwa kulinda ustawi na usalama wa raia’.

Wakili Katuga: Tunaomba uieleze mahakama hizo kurasa zilikuwa za namna gani?

Shahidi: Ilikuwa ina kurasa nyeupe na maandishi meusi.

Wakili Katuga: Ridhaa ya mahakama angalia nyaraka hii?

Shahidi ameiangalia (Press-Release).

Wakili Katuga: Hiyo ni nini shahidi?

Shahidi: Hiyo ndiyo nyaraka aliyonikabidhi Zitto.

Wakili Katuga: Unataka mahakama iifanye nini?

Shahidi: Iiridhie na iichukue kama kielelezo.

Wakili Katuga: Shahidi naomba isome hiyo nyaraka.

Awali, Zitto alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka matatu ya uchochezi anayodaiwa kuyatenda Oktoba 28, mwaka jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya ACT Wazalendo.

Hata hivyo, Hakimu Shaidi, aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 18 na 19, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles