22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Ngozi, kinyesi cha ng’ombe vyatumika mbadala wa pedi

AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM

UKOSEFU wa taulo za kike hasa maeneo ya vijiji vya mikoa ya wafugaji umewafanya wasichana kutumia udongo, ngozi na vinyesi vya wanyama kama vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi.


Akizungumza Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya siku mbili ya masuala ya hedhi salama, Mtaalamu wa Maji na Usafi wa Mazingira na Mwezeshaji Mwandamizi katika Masuala ya Hedhi Salama, Dhania Mbaga, alisema utafiti uliofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali la SNV, unaonyesha kuwa changamoto wanazokumbana nazo wasichana na akina mama waliopo maeneo ya vijijini kipindi cha hedhi ni kubwa kiasi cha kutumia vitu ambavyo si salama.


Alisema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kujihifadhia zikiwemo taulo za kike kipindi cha hedhi jambo linalosababisha baadhi ya makabila na jamii ya kifugaji kutumia vifaa visivyo salama mara tu baada ya msichana kuvunja ungo.


“Mabinti na akina mama wanaoishi huko vijijini wanapata shida wanapoingia hedhi kwa sababu vifaa vinavyotumika si rafiki, sisi tumezunguka mikoani na kufanya tafiti, wapo watu ambao wanapoingia katika hedhi wanatumia ngozi, udongo pamoja na vinyesi vikavu jambo linalosababisha kuwafanya kupata maumivu makubwa na kushindwa kuwa huru,” alisema Mbaga.


Alisema vifaa hivyo vinavyotumika mbali na kuwaumiza lakini pia vinashindwa kufyonza damu vizuri na kuwafanya kuwa katika hali ya uchafu na pia wanaposhindwa kuvifanyia usafi ipasavyo mtumiaji anaporudia kukitumia anakuwa na uwezekano wa kupata maradhi.
Alisema kwa mujibu wa SNV, wilaya zilizofanyiwa utafiti ni pamoja na Babati, Siha, Chato, Magu, Sengerema, Njombe na Mufindi.


Naye Mkufunzi kutoka Taasisi ya I4ID, Halima Lila, alisema vifaa vya kujihifadhia kipindi cha hedhi ni muhimu kwa wanawake kwa sababu wanapokosa wanapata shida ya kujisitiri na kushindwa kufanya shughuli zao.
Alisema tatizo la kukosekana kwa taulo za kike katika maeneo ya vijijini linatokana na wahusika kutofikisha bidhaa hiyo katika maeneo hayo na hata wakifikisha inauzwa kwa bei ya juu licha ya Serikali kuiondolea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).


“Serikali isitoe VAT kwa kuwa bado taulo za kike zinauzwa bei ile ile ya awali, kikubwa iangalie inafanya nini katika kusaidia jamii kupata vifaa hivyo kwa urahisi zaidi hasa maeneo ya vijijini,” alisema Lila.


Kwa upande wake, Mkufunzi wa Masuala ya Hedhi Salama, Robert Kitundu, alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa waandishi wa habari kwa lengo la kutoa fursa ya uelewa wa namna watakavyoandika habari juu ya masuala ya hedhi salama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles