NAIROBI, KENYA
MASENETA wa mrengo wa muungano wa Jubilee wamewataka wenzao wa Cord kuachana na mpango wa maandamano ambayo wameyaitisha nchi nzima.
Cord walitangaza kuitisha maandamano hayo kuanzia Januari 4 mwakani kupinga mageuzi tata yaliyofanywa na Serikali kuhusu sheria za uchaguzi.
Maseneta Stephen Sang’ (Nandi), Aaron Cheruiyot (Kericho), Kimani Wamatangi (Kiambu), Mutahi Kagwe (Nyeri) na Beatrice Elachi (maalumu), walisema Cord inapaswa kuheshimu hatua ya Seneti ya kuwasilisha suala hilo kwa Kamati ya Sheria kwa kupokea maoni kutoka kwa wananchi na wadau wengine.
“Kwa sababu Seneti imeongozwa na hekima na busara kurejesha suala hili kwa umma ili kupata mwafaka, tunaomba wenzetu wa Cord wasitishe maandamano ili kutoa nafasi ya majadiliano kuhusu sheria hii,” alisema Sang’.
Aidha Wamatangi alitoa wito kwa wanachama wa Cord, hasa vinara Raila Odinga, Kalonzo Musyoka na Moses Wetang’ula kufika kwenye vikao vya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta Amos Wako watoe maoni yao.
“Bila shaka mapendekezo yao, pamoja na ya Wakenya wengine yatajumuishwa kwenye ripoti ambayo itawasilishwa katika Bunge hili kwenye kikao maalumu hapo Januari 4.
“Hakuna haja kwa watu kuandamana kiasi cha kupandisha joto la kisiasa wakati huu muhimu Wakenya wakijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu ujao. Spika wetu ametoa mwelekeo mzuri na sote twapaswa kuufuata ili taifa hili liwe thabiti,” alisema Seneta huyo wa Kiambu.
Hata hivyo, Ofisa Mkuu Mtendaji wa Ofisi Kuu ya Cord, Norman Magaya, alisema vinara wa Cord walitarajia kukutana jana kujadiliana na kuamua iwapo waahirishe maandamano au la.
“Uongozi wa Cord utakutana kutokana na yaliyojiri katika Bunge la Seneti ijapokuwa hayawezi kubadili msimamo wetu wa kupinga marekebisho yaliyofanywa katika sheria hiyo,” alisema Magaya.