NA FERDNANDA MBAMILA-DAR ES SALAAM
SERIKALI kupitia Taasisi isiyo rasmi nchini ya Women in Mining Netwok Tanzania (AFWIMNTZ), imetoa msaada wa majiko 238 na kilo 40 za vitofali vya makaa ya mawe katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Taasisi hiyo ambayo makao yake makuu ni Kimara Bucha jijini Dar es Salaam, ni taasisi inayotengeneza majiko sanifu na maalumu kwa matumizi ya nishati ya vitofali vya makaa ya mawe.
Ofisa Misitu katika Ofisi ya Makamu wa Raisi Idara ya Mazingira, Timothe Mande, anasema kutokana na takwimu za awali nchini, zaidi ya tani laki 3 za misitu hutumika kila mwaka na kuna ongezeko ambalo linategemewa kufikia hadi tani laki 4 mpaka laki 5 kutokana na matumizi ya kuni na mkaa nchini.
Anasema zaidi ya asilimia 30 ya wananchi haswa wa vijijini hutegemea zaidi matumizi ya kuni na mkaa katika shughuli mbalimbali za kila siku.
Lengo mahususi la mradi huu ni kwamba wajasiriamali hao wanatengeneza majiko maalumu ya makaa ya mawe ili kurahisisha mapishi haswa kwa mama ntilie nchini kwa kuanza na Manispaa ya Kinondoni.
Kwani baada ya kuanza kutumika kwa majiko hayo, imewarahisisha kwa kiasi kikubwa kwani hapo awali walikuwa wananunua mkaa wa kawada kwa kiasi cha Sh 6,000 kwa kipimo cha debe, lakini kwa sasa wananunua kiasi cha Sh 3,000 kwa makaa ya mawe.
“Endapo tutalinda vyanzo vyetu vya asili kama misitu na vichaka, tutakuwa tumenusuru majanga na maafa mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yangeweza kutokea hapo baadaye,” anasema Mande.
Anasema ingawa kuna athari za kawaida zinazosababishwa na binadamu na kutokana na ukataji wa misitu na kwa na uchomaji ovyo wa vichaka.
Hata hivyo, aliipongeza sana Taasisi ya African Women kwa kubuni mradi kama huo ambao umekuwa ni mwanga kwa jamii ya Tanzania kwa ujumla.
Naye Katibu Mtendaji wa Taasisi hiyo, Mary Mbeyela, anasema katika manispaa ya Kinondoni ambapo ina jumla ya kata 20 za wilaya hiyo na 14 za Manispaa ya Ubungo, zimeweza kunufaika na zoezi hilo.
Anasema zaidi ya majiko 170 yenye uwezo wa kupokea kitofali kimoja cha mkaa huo yameweza kutolewa katika ngazi ya Kaya 68 kwa mama lishe na baba lishe, ambayo yana uwezo wa kubeba vitofali vitatu hadi vinne kwa wakati mmoja.
“Hata hivyo, majiko yaliyogawiwa tayari kwa baba lishe na mama lishe, kila jiko moja lina thamani ya Sh 40,000 wakati yale yatakayotolewa kwa ngazi ya Kaya yana thamani ya Sh 15,000 kwa kila jiko moja,” anasema Mary.
Anasema lengo kuu la uzinduzi huo ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ya makaa ya mawe kwa kuanzia katika nafasi ya kaya hadi manispaa kwa mama lishe na baba lishe pamoja na wakaanga chipsi na mishkaki.
Kwani kabla ya kufikia hatua hii ya kutoa msaada wa majiko na makaa ya mawe kwa wananchi hao, taasisi hii ilifanya majaribio ya mkaa huo wa matofali ya mkaa ya mawe ambao ni wa tofauti zaidi.
“ Kuna baadhi ya taasisi mbalimbali mfano Gereza la Segerea mnamo mwaka 2012 lilitoa msaada pia , Shule ya Sinza maalumu chini ya mamlaka ya Manispaa ya Kinondoni mwaka 2013 na kwenye majiko ya bwalo la chakula katika hostel ya wanafunzi ya MTC katika Chuo Kikuu cha Sayansi cha Afya Muhimbili,” anasema Mary.
Anasema taasisi imejikita zaidi katika utengenezaji wa majiko sanifu ambayo ni maalumu kwa matumizi kwa nishati ya vitofali vya makaa ya mawe, vinavyotokana na vumbi linalopatikana baada ya makaa ya mawe kusafishwa.
“Utengenezaji wa majiko hayo pamoja na vitofali vya makaa ya mawe , vimefadhiliwa na mfumo wa misitu Tanzania, ambao uko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili kusaidia ukataji ovyo wa misituna, uoto wa asili hapa nchini,” anasema Mery.
Anasema baada ya zoezi la uzinduzi huo ambalo limewahusisha watendaji wa kata na Serikali za mitaa zilizotajwa, watakuwa na jukumu la kuwatafuta wananchi wanaouza mkaa wa kuni ili kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kutumia nishati mbadala na kisha watawauzia kwa bei ya jumla majiko na vitofali kwa ajili ya kuwauzia wateja wao.