25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI YANAHITAJI MBINU MPYA


NI siri iliyo wazi kwamba Ukimwi bado ni tishio kubwa kwa maisha ya watu nchini na dunia nzima kwa ujumla.  Sababu kubwa ni kwamba hadi sasa ugonjwa huo haujapata tiba wala chanjo inayoeleweka licha ya juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na wanasayansi na watafiti.

Vilevile ingawa hatua kadha wa kadha zimekuwa zikichukuliwa zikiwamo kampeni za kila wakati na utoaji wa elimu kuhusu jinsi ya kuukabili ugonjwa huo, hali bado si ya kutia matumaini kwa kiasi kikubwa.

Ni kweli kwamba dawa za kupunguza makali ya ugonjwa zimekwisha kugundulika na zimekuwa zikitumiwa kwa miaka mingi na watu wenye vijidudu vya ugonjwa huo (VVU) kwa utaratibu maalumu.  Hizo na nyingine, ni mbinu, mipango na taratibu ambazo zinapaswa kuendelezwa na kuwekwa  mkazo zaidi.

Hata hivyo, inaonekana, ni wakati sasa wa kuwapo msukumo mpya wa kukabiliana na Ukimwi kwa kuzingatia ripoti mbalimbali za utafiti ambazo zimekuwa zikitolewa.

Mfano ni ripoti iliyotolewa kwa wahariri wa habari mjini Bagamoyo juzi iliyohusu matokeo ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ugonjwa huo kwa mwaka 2016/17, utafiti uliofanywa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukiwmi (TACAIDS).

Kwa mujibu wa utafiti huo watu wanaopeana talaka wanaonoza kwa kuwa na maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha Ukimwi kwa asilimia 11 ikilinganishwa na maambkizi kwa watu walioko katika ndoa ambayo  yamefikia asilimia 4.8.

Hili ni suala ambalo halina budi liangaliwe kwa uzito wake kulinda maisha ya watu wanaotalikiana. Kwa maana kwamba kwa nini watu idadi ya watu hao kupata VVU iwe kubwa kiasi hicho?

Pengine inabidi itafutwe njia ya kudumu na inayoeleweka ya kuwafikia watu hao waweze kuepukana na maambukizi mapya ya VVU.

Mfano mwingine ni habari zilizopatikana mkoani Simiyu hivi majuzi kwamba watu wapatao 10,000 ambao wamekuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya Ukimwi wameacha kutumia dawa hizo na hawajulikani waliko!

Hii nayo ni hali ambayo siyo nzuri kwa sababu ilitarajiwa watu hao waendelee kutumia dawa hizo na siyo ‘kupotea’ ikizingatiwa zinatolewa bure,  kwa utaratibu maalumu na unaoeleweka.

Swali ni kwamba kitu gani kimetokea hadi wakaamua kuacha   kutumia dawa hizo na hata ‘kupotea?’

Hiyo ni mifano michache tu ambayo inadhihirisha kwamba pengine kuna haja ya kubadili mbinu na taratibu za kupambana na Ukimwi.  Kwamba mbinu ambazo zimekuwa zikitumika hadi sasa  hazitoshelezi na hazina budi kuangaliwa upya.

Ni ukweli usiopingika kwamba kila kukicha binadamu anazidi kukabiliwa na matatizo au changamoto mpya ambazo hana budi kutafuta njia ya kupambana nazo.

Kama tulivyokwisha kusema, wakati umefika kwa wadau wote wakiwamo watafiti, wataalamu, maofisa, viongozi na watendaji kuziangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza ili mapambano dhidi ya Ukimwi yaweze kuleta matunda yanayotarajiwa ikizingatiwa kuwa hadi sasa hakuna tiba wala chanjo ya ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles