Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
MANISPAA ya Ilala imeanzisha utaratibu wa kutoa uji kwa wazazi pindi wanapokuwa leba ili kudhibiti uingizwaji wa dawa za mitishamba ambazo zimekuwa zikitumiwa na wanawake wengi kuharakisha uchungu.
Dawa hizo zimetajwa kusababisha madhara kwa akina mama kama vile kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua, mtoto kuzaliwa akiwa amechoka na wakati mwingine mama na mtoto huweza kupoteza maisha.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Dk. Victorina Ludovick, alisema matumizi ya dawa za asili na za hospitali yanaweza kusababisha mwingiliano au ukinzani wa dawa na kusababisha madhara kwa mtumiaji.
“Vifo vya kina mama vimepungua, tunaweza kukaa hata miezi miwili bila kupata kifo, lakini changamoto tuliyo nayo sasa ni ya vifo vya watoto wachanga, wastani wa watoto wawili hadi watatu wanafariki dunia kwa wiki na watoto wengi wanafariki kati ya siku moja hadi saba.
“Ni hali ambayo hatuifurahii sana kwa sababu hakuna mama ambaye anapenda afike hospitalini halafu arudi nyumbani bila mtoto, inaumiza na kusononesha sana. Tumeanzisha utaratibu wa kutoa uji, mama akishaingia leba tu haturuhusu vimiminika vingine viingie hata kama ni maji ya kunywa lazima chupa iwe imefungwa,” alisema Dk. Ludovick.
Akitoa mfano alisema mama anaweza kufika hospitali akiwa ameshakunywa dawa za mitishamba na inapotokea akachomwa sindano za uchungu hali hiyo inaweza kusababisha dawa moja isifanye kazi au nyingine iwe na nguvu na kuleta madhara.
“Unakuta mama anahangaika sana bila mafanikio na wakati mwingine anatokwa na damu nyingi, ukimuuliza hasemi hadi anapoona hali imekuwa mbaya, wanawapa shida wahudumu wetu,” alisema.
Alitaja sababu nyingine zinazosababisha vifo hivyo kuwa ni mama kuchelewa kufika hospitali, shinikizo la damu kuwa juu na kupungukiwa damu.
Alisema pia wameanzisha huduma za kibingwa za Mkoba katika maeneo ya pembezoni mwa mji ambayo yamekuwa yakitembelewa kila baada ya wiki mbili.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni Msongola, Mvuti, Zingziwa, Chanika, Buyuni, Majohe, Pugu, Kinyerezi, Kitunda na Kivule.
“Haya ni maeneo ambayo yana watu wengi lakini mengine hayafikiki na unaweza kukuta hospitali iko mbali hivyo usipowafuata huwezi kujua kinachoendelea,” alisema.