LONDON, ENGLAND
KLABU ya Manchester United imekataa pauni bilioni 3 za hisa kutoka kwa mtoto wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kwa madai kuwa klabu hiyo haiuzwi.
Bin Salman, ambaye anatoka katika familia ya Mfalme wa Saudia Arabia, inayomiliki utajiri wa pauni bilioni 850, anataka kununua hisa za pauni bilioni tatu ili kuimiliki klabu hiyo.
Mwana wa Mfalme huyo ni miongoni mwa matajiri wakubwa duniani, amedaiwa kuwa na nia ya kuinunua klabu hiyo moja kwa moja.
Lakini jitihada zake hizo zinaonekana kugonga mwamba kwa familia ya Glazer, licha hisa za klabu hiyo kuongezeka tangu mpango wake ulipogundulika.
Thamani ya Manchester United kwa sasa inakaribia kuwa pauni milioni 2.7, lakini  itauzwa kwa pauni bilioni nne.
Kwa mujibu wa gazeti la The Sun, Bin Salman, hivi karibuni anatarajia kukutana na mmiliki wa klabu ya Manchester United,  Avram Glazer, nchini Saudi Arabia.
Bin Salman alisema anatamani kuwa mpinzani mkubwa wa jirani yake, mmiliki wa Manchester City, Sheikh Mansour katika miaka 10 ijayo.
Hata hivyo, licha ya hali halisi iliyopo ndani ya klabu hiyo, inaonekana kubaki katika mikono ya familia ya Glazers, ambayo inamiliki asilimia 97 za hisa ya tangu Mei mwaka 2005.
Ikiwa chini ya Glazers, Manchester United, imeshinda mataji matano ya Ligi Kuu England, ambayo ni mengi kuliko klabu yoyote kwa kipindi cha miaka 13.
Klabu hiyo pia imenyakua Kombe la FA, Kombe la Ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini Glazer kwa sasa anaonekana kutofautiana na wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, wakidai wameelemewa na madeni tangu tajiri huyo aichukue.
Klabu hiyo katika majira ya joto yaliyopita ilishindwa kumpa fedha kocha Jose Mourinho kusajili wachezaji anaowataka.
Manchester United ilishindwa kumsajili beki wa kati, ingawa Mourinho alikuwa akihitaji kusajili sura mpya ili kukiongezea nguvu kikosi chake.
Kocha huyo, ambaye kwa sasa yupo katika presha ya kufukuzwa, alikuwa akimhitaji beki wa Leicester, Harry Maguire, Bayern Munich, Jerome Boating au Toby Alderweireld kutoka Tottenham.
Kutokana na sababu hizo, Manchester  United imekuwa na mwanzo mbaya tangu kuanza msimu mpya wa Ligi Kuu England.