25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mamlaka za mikoa zitangaze fursa za uwekezaji

Na Ismail Ngayonga



SERIKALI  ya Awamu ya Tano imeingia katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/17 – 2020/21, unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu.

Uamuzi wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na endelevu na hivyo kuchangia katika kukuza Pato la Taifa, kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira, kuzalisha na kukuza teknolojia zinazohitajika na kuzalisha bidhaa bora kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi.

Ili kufikia malengo hayo, ardhi ni miongoni mwa rasilimali muhimu iliyowekewa mikakati maalumu na Serikali katika kufikia azma ya uchumi wa viwanda katika kuikwamua jamii na wimbi la umasikini, ikiwa ni pamoja na kuwa na rasilimali ya kutosha kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Miongoni mwa mikakati hiyo ya Serikali ni pamoja na kuhamasisha mamlaka za usimamizi wa ardhi nchini ikiwemo halmashauri za vijiji, wilaya na miji kupunguza michakato ya utoaji hati za umiliki wa ardhi kwa wawekezaji ili kuweka mazingira bora ya ujenzi wa viwanda katika mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa nchini.

Taarifa ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inaonyesha kuwa mamlaka za Serikali za mitaa kupitia mikoa na wilaya, zimeendelea kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, ambapo jumla ya mikoa 13 imewasilisha taarifa ya utengaji wa maeneo hayo.

Mikoa hiyo ni pamoja na Mkoa wa Kigoma ekari 451.46, Kilimanjaro ekari 53,033.16, Simiyu (807.06), Shinyanga (33,637.63), Tanga (33,788.62); Mbeya ekari (6,618.83); Pwani (63,065.2), Dodoma (54,614.16), Singida (15,442), Mwanza (11,204.3), Njombe (15,662.29), Lindi (8,790.52) na Geita (472) na viwanja 144.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, anasema hadi kufikia Mei mwaka huu, mipango kabambe ya miji 18 inayoandaliwa imetenga jumla ya ekari 127,942.96 kwa ajili ya matumizi ya viwanda.

Waziri Lukuvi anasema kupitia mwongozo ulioandaliwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Upangaji, tayari  Halmashauri ya Wilaya Kibaha imepanga eneo lenye jumla ya hekta 1,563 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vikubwa 124 na viwanda vidogo 23.

“Wizara imetenga eneo la ardhi ya akiba lenye ukubwa wa hekta 89.9, maeneo ya biashara hekta 40.6 na ardhi ya kilimo cha biashara yenye ukubwa wa hekta 334 zilizopatikana kutokana hekta 2,383 kubatilishwa  milki yake kutokana na ukiukwaji wa masharti ya uendelezaji,” anasema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi anasema Serikali imebatilisha milki za mashamba yenye ukubwa wa ekari 9,636.19 katika wilaya za Lushoto, Busega, Bukoba na Arumeru na kutoa maelekezo kwa mamlaka za upangaji ikiwemo halmashauri za vijiji, wilaya na miji kuzingatia utengaji wa maeneo hayo kwa ajili ya viwanda, kilimo na ardhi ya akiba.

Anaongeza kuwa katika kutekeleza azma hii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, inaendelea kuandaa mpango wa kuendeleza ardhi katika eneo la Mbwamaji lenye ukubwa wa ekari 711 kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya uwekezaji.

Akifafanua zaidi, Waziri Lukuvi anasema Serikali pia imeboresha huduma mbalimbali katika sekta ya ardhi ikiwemo kupunguza muda wa kuandaa na kusajili hati ambapo kwa sasa mwekezaji anaweza kupata hati ndani ya muda wa siku 30, endapo atakuwa amekidhi vigezo na masharti ya umilikishaji.

Aidha, Waziri Lukuvi anasema pia mifumo ya kutoa huduma za ardhi kwa njia za kielektroniki imeimarishwa, ambapo muda wa upatikanaji wa taarifa za hati na nyaraka nyingine zilizosajiliwa umepungua kutoka siku saba hadi tatu.

Ujenzi wa viwanda unaanza kwa kutambua eneo la kujenga viwanda ambalo ubainishwaji wake na uwekaji wa miundombinu wezeshi na saidizi unahusisha mamlaka mbalimbali, hivyo mafanikio ya dhima ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ni matokeo ya ushirikiano na jitihada za wizara zote na Serikali kwa upande mmoja na sekta binafsi kwa upande mwingine.

Kimsingi Tanzania haina shida ya ardhi lakini ili kupata ukamilifu wa matumizi ya miundombinu, Serikali haina budi kupunguza michakato ya utoaji ardhi ikiwemo mihula ya umiliki iliyoidhinishwa kisheria kwa miaka 33, 66, 99 kupitia hati miliki za kimila.

Ujenzi wa viwanda unaanza kwa kutambua eneo la kujenga viwanda ambalo ubainishwaji wake na uwekaji wa miundombinu wezeshi na saidizi unahusisha mamlaka mbalimbali, hivyo mafanikio ya dhima ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ni matokeo ya ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles