26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAMLAKA KIONGOZI MBIO ZA MWENGE YAZUA GUMZO

Na BENJAMIN MASESE- MWANZA

MAMLAKA na majukumu ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, yameonekana kuwachanganya watu wengi, wakiwamo watumishi wa umma.

Baadhi ya watu wakiwamo wasomi na wanasheria, wamesema kiongozi huyo hana mamlaka yoyote kisheria kukaripia watendaji wa Serikali isipokuwa kushauri tu.

Mkanganyiko huo wa majukumu umekuja siku chache baada ya kiongozi wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Amour Hamad Amour juzi kuwahoji hadharani viongozi wa Halmashauri ya Nyamagana jijini Mwanza kuhusu mradi wa maji ambao haujakamilika.

MTANZANIA ilizungumza na baadhi ya wananchi, wasomi na wachambuzi wa sera na mifumo, ambao wengi walionekana kutojua majukumu na mamlaka ya kiongozi wa mbio za mwenge.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sera na Utafiti ya Governance Links, Donald Kasongi, alisema majukumu ya kiongozi wa mbio za mwenge ni kuhamasisha shughuli za maendeleo, kuhimiza umoja ambao ndio nguzo kuu ya mwenge na kutoa kauli ya kukosoa au kusifia juu ya taarifa aliyopewa ya mradi wa maendeleo katika eneo husika.

Alisema kiongozi wa mbio za mwenge hana mamlaka ya kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa watumishi wa umma, kwa sababu hayupo katika Sekretarieti ya Maadili kwa viongozi wa umma, ispokuwa ana fursa ya kushauri tu.

“Unajua hadi kuwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, unakuwa umepitia katika mchunjo mrefu. Kuna watu wengi wanachaguliwa kisha wanaanza kuchujwa kwa kutafuta kigezo cha kumpata mtu ambaye anachukua sura ya Watanzania wote, yaani anaposimama anakuwa ni sura ya kitaifa,” alisema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Liberatha Damas, alisema hajui majukumu na mamlaka ya kiongozi wa mbio za mwenge, huku akibainisha kwamba tangu atoke shule za msingi hajawahi kufuatilia suala la mwenge.

“Kwa kweli tangu niondoke shule za msingi sijawahi hata kufuatilia huo mwenge, hata leo ukiniuliza upo wapi sijui kabisa na sijui majukumu na mamlaka aliyonayo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa,” alisema.

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake la Kivulini, Yassin Ally, alisema katika sheria za Tanzania kuna viongozi wa ajira na wale wa uteuzi, hivyo anaamini kiongozi wa mbio za mwenge ni mteule, hivyo itakuwa vigumu kutoa maelekezo ya kiutendaji kwa mtumishi wa umma ambaye kuna taratibu za kumwajibisha pale anapokosea.

Mtafiti wa mambo ya sera ambaye ni mwanasheria, Gasper Mwanaliela, alisema jukumu la kiongozi wa mbio za mwenge ni kutoa tamko, kupendekeza na kutoa taarifa serikalini ili wizara husika iweze kutafsiri matamko hayo na hatua za kiutendaji kuchukuliwa.

Alisema kiongozi wa mwenge hana mamlaka ya kumchukulia hatua mtumishi wa umma isipokuwa kukemea na kusisitiza kwamba baada ya ujio wa vyama vingi 1992 dhamana ya mwenge ilibaki chini ya Serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles