32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

VILIO, SIMANZI BOMOA BOMOA KIMARA

NA WAANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

UBOMOAJI wa nyumba zaidi ya 1,300 unaoendelea kuanzia Kimara hadi Kiluvya, Dar es Salaam kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro, umeacha vilio na simanzi kwa mamia ya wananchi, wakiwamo wamiliki wa nyumba, wapangaji, wafanyabiashara, misikiti na makanisa.

Bomoa bomoa hiyo inayoendelea kufanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, inatarajiwa kuzikumba nyumba zilizopo mita 121.5 kutoka katikati ya barabara.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya waliokumbwa na bomoa bomoa hiyo, wameeleza machungu wanayopitia katika kipindi hiki ambacho nyumba zao zimebomolewa.

Mwalimu mstaafu, Juma Ngonyani, alisema amepata hasara ya Sh milioni 150 baada ya kubomolewa baa yake ya Kibamba CCM iliyokuwa tegemeo lake.

Alisema alijinyima kwa miaka 40 kuwekeza katika biashara ambayo ingemsaidia akiwa amestaafu kazi, lakini Serikali imemrudisha nyuma baada ya kubomoa baa yake.

“TANROADS walifika hapa wakiwa na polisi wakatuamuru kutoa vitu vyetu huku wakitutishia, tulitoa ndipo wakaanza kubomoa,” alisema Ngonyani.

Alisema anaumia sana kuona nguvu zake nyingi alizofanya kazi akiwa kijana zikipotea huku akiwa hana msaada wowote.

“Sheria tuliyoikuta kipindi tunahamia hapa hifadhi ya Barabara ya Morogoro ni mita 60 kila upande katika sheria ya mwaka 1967, lakini sheria ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009 zimetukuta, hivyo Serikali ingeweka utaratibu wa kutuondoa na si kutumia nguvu,” alisema.

Mfanyabiashara wa duka Kibamba, Hilda Mkenda, akizungumza huku akilia, alisema amechanganyikiwa kwa kuwa alikuwa amechukua mkopo katika taasisi za kifedha ili kuendeleza biashara yake.

“Tutakuwa wageni wa nani, tuliwaachia mita 60 bado wanatufuata na huku tena, nina mkopo nitalipaje mimi?” alisema Hilda.

Kwa upande wake Imamu wa Msikiti wa Nuur uliopo Kibamba, Ustadhi Mashaka Shaaban, alisema pamoja na kuwa maendeleo yana changamoto zake, lakini Serikali iwahurumie wananchi wake wakiwamo wazee na wajane.

“Msikiti upo hapa tangu mwaka 1970, tangu ulipokuwa umejengwa kwa udongo hadi leo hii unavyouona ni ‘block’, hapa hatuna sehemu ya kwenda kuabudia kwa kuwa Serikali haijatoa eneo wala fidia,” alisema Ustadhi Shaaban.

Hata hivyo, tingatinga linalobomoa nyumba hizo, jana lilishindwa kuendelea na kazi baada ya kuharibika eneo la Mbezi kwa Msuguri saa 9.00 alasiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles