24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MA-DC WAWILI HATARINI KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Upendo Mosha- Hai

WAKUU wa wilaya wawili, wako hatarini kufikishwa mahakamani baada ya kudaiwa kukiuka maadili ya kazi zao.

Mmoja ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa Kilimanjaro, Gelasius Byakanwa, anayedaiwa kumwamuru Mwalimu wa Shule ya Sekondari Lerai, iliyopo Kata ya Bondeni, wilayani humo, kupiga ‘pushapu’ mbele ya wanafunzi wake.

Mwingine ni Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mkoa wa Dodoma, Simon Odunga, anayedaiwa kumpiga na kumjeruhi mkazi wa Kijiji cha Kambiyanyasa, Chindika Pingwa (57), ambaye ni mzazi wa mtoto anayedaiwa kuvunja kioo cha gari la kiongozi huyo, wakati wakicheza na wenzake.

Tukio la wilayani Hai lilitokea Agosti 11 mwaka huu shuleni hapo baada ya mwalimu huyo, Erasto Mhagama, kushindwa kujibu maswali aliyoulizwa na mkuu huyo wa wilaya.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwalimu Mhagama, alisema wakati analazimishwa kufanya hivyo, walikuwapo pia walimu wenzake baada ya mkuu huyo wa wilaya kufika shuleni hapo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi.

“Baada ya mkuu huyo wa wilaya kufika shuleni kwetu na kupokewa na makamu mkuu wa shule yetu, aliomba kufanya kikao kifupi na walimu.

“Wakati wa kikao hicho, alituuliza maswali mbalimbali yakiwamo nini kirefu cha IGP, CDF, CUF na CAF na maswali mengine mengi.

“Alipofika kwangu, aliniuliza Wilaya ya Hai ina shule ngapi nami nikamjibu sijui kwa sababu sina takwimu.

“Niliposema sijui, alinikaripia kwa maneno makali ya kejeli na kunitaka nisishiriki tena katika mjadala wa kikao hicho alichokuwa akikiongoza yeye.

“Baadaye, aliniita pembeni, nje ya kikao na kunitaka nichague adhabu mbili ambazo ni kukaa mahabusu kwa saa sita au kupiga pushapu 20 hadharani.

“Nilimwambia siwezi kupiga pushapu kwa sababu nina matatizo ya kiafya, lakini alionekana kukasirika kwa sababu aliniambia hayo hayamhusu.

“Kwa hiyo, alipiga simu polisi na baada ya muda mfupi, gari la polisi wa Kituo cha Bomang’ombe, lilifika na kunibeba na kunipeleka mahabausu ya kituo hicho, majira ya saa nane mchana hadi saa mbili usiku nilipotolewa.

“Nilipotolewa mahabusu nilikuwa nimechanganyikiwa kidogo, lakini nilijikaza kiume na kurudi nyumbani kwangu.

“Kwa kuwa nilidhalilishwa mbele ya walimu na wanafunzi wangu, naomba mamlaka husika zichukue hatua dhidi ya mkuu huyo wa wilaya ili kulinda haki na masilahi ya walimu,” alisema mwalimu huyo.

Katibu wa Chama cha Walimu, Mkoa wa Kilimanjaro (CWT), Digna Nyaki,  alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema halileti taswira nzuri katika jamii.

Kutokana na hali hiyo, alisema CWT imemtaka mkuu huyo wa wilaya aombe radhi dhidi ya tukio hilo ndani ya siku 30 kuanzia jana kabla hajafikishwa katika vyombo vya sheria.

“Ni kweli tukio hilo lipo na lilifanywa na DC Ijumaa ya wiki iliyopita katika Shule ya Sekondari Lerai. Tumejiridhisha kwa hilo baada ya kupata taarifa na kutembelea shule hiyo na kuzungumza na walimu ambapo walikiri mkuu huyo wa wilaya kufanya tendo hilo.

“Kwa hiyo, tunampa siku 30 aombe radhi na kama hatafanya hivyo, tutampeleka mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema Nyaki.

“Tutamfikisha mahakamani kwa sababu hii siyo mara yake ya kwanza kufanya vitendo vya udhalilishaji kwani awali alifanya hivyo kwa walimu wa Shule ya Sekondari Boma.

“Kwa kifupi, tumeshapata malalamiko mengi kutoka kwa walimu wa Hai wakimlalamikia, kwamba amezoea kufanya hivyo kwani hata mwaka jana, alimsweka ndani mwalimu mwingine kwa sababu zisizokuwa na msingi.

“Kibaya zaidi, amekuwa akitoa vitisho mbalimbali, kwamba hakuna mtu anayeweza kumfanya chochote na kuna taarifa zinasema amesababisha walimu wetu wawili waache kazi na hadi sasa tunafuatilia mambo hayo.

“Mpaka sasa tumepata taarifa za ndani kwamba kuna walimu wawili wameacha kazi kutokana na uzalilishaji unaofanywa na DC kwa sasa tupo katika ufuatiliaji zaidi tutatoa taarifa rasmi, lakini hatua inayofuata sasa tutapeleka malalamiko yetu kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwhira,” alisema.

Alisema vitendo vya uzalilishaji vinavyofanywa na DC huyo vimekuwa vikififisha juhudi na jitihada za walimu katika kuongeza ufaulu kwa wanafunzi na kwamba havipaswi kufumbiwa macho bali hatua stahiki za kinidhamu zitachukuliwa ili kukomesha tabia hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA juu ya tukio hilo, mkuu huyo wa wilaya, alikana kumpigisha pushapu mwalimu huyo ingawa alikiri kufika shuleni hapo akiwa katika ziara ya kikazi.

“Sikumpigisha pushapu wala kichura ila kilichotokea ni kwamba wakati namuuliza maswali huyo mwalimu alinijibu kwa ujeuri.

“Kinachoonekana hapa ni kwamba kuna watu wanapinga jitihada zangu za kuleta maendeleo ndiyo maana wameanza kugeuzageuza maneno,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Wakati kiongozi huyo wa wilaya akikanusha tukio hilo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issa, alithibitisha mkuu huyo wa wilaya kumweka ndani mwalimu huyo kwa saa sita.

“Hilo tukio lipo na nimeambiwa mkuu wa wilaya alimweka ndani mwalimu kwa saa sita baada ya kushindwa kujibu swali alilomuuliza.

“Kwa hiyo, nadhani itabidi nitoe maelekezo kwa viongozi wetu ili wajue ni makosa gani ya kuwaweka watu ndani kwa sababu kiongozi anaruhusiwa kumweka mtu ndani pindi anapohatarisha amani na si vinginevyo,” alisema Kamanda Issa.

Katika tukio jingine, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mkoa wa Dodoma, Simon Odunga, ametakiwa kumwomba radhi, Chindika Pingwa (57), baada ya kudaiwa kumpiga na kumuumiza.

Hivi karibuni, Odunga alimcharaza  viboko mkazi huyo wa Kijiji cha Kambiyanyasa, wilayani Chemba kwa madai kuwa mtoto wake alivunja kioo cha gari lake lenye namba za usajili STL 669.

Katika tukio hilo lililotokea wiki iliyopita, watoto hao walitajwa kuwa ni Baraka Chindika, Majala Chindika, Jacskon Stephano na Paschal Daud.

Akizungumza na MTANZANIA juzi katika Kitongoji cha Mlongia, Kijiji cha Kambiyanyasa, Pingwa alisema amelazimika kulifikisha suala hilo katika vyombo vya sheria kwa sababu mkuu huyo wa wilaya alimdhalilisha.

“Alinidhalilisha kupita kiasi kwa sababu siku ya tukio alinipiga na kuni kichwani nikiwa nimelazwa kwenye gari la polisi, huku nikiwa nimefungwa pingu.

“Kwa kuwa naamini hakunitendea haki, namtaka aniombe radhi haraka, vinginevyo nitalazimika kumfikisha mahakamani.

“Kosa la kuvunja kioo lilifanywa na mtoto, iweje mimi nipigwe kwa kosa ambalo sikulifanya?, namtaka aniombe radhi.

“Pia, naiomba Serikali iwaangalie viongozi wake wanafanyaje kazi kwani wanaweza kusababisha madhara kwa wananchi wasiokuwa na hatia,” alisema Pingwa.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mlongia, Marius Roman, alisikitishwa na kitendo alichofanya mkuu huyo wa wilaya na kusema kiongozi huyo amekuwa na matukio mengi ambayo yanasababisha baadhi ya wananchi wakose imani naye,” alisema Roman.

Kwa upande wake mkuu huyo wa wilaya alipoulizwa siku ya tukio, alikiri kufanya kitendo hicho na kusema kuwa baadhi ya watu wa kijiji hicho wamekuwa na tabia ya kuweka mawe barabarani pamoja na kupiga magari mawe.

Alisema watahakikisha tabia hiyo inakomeshwa, kwani vitendo hivyo ni hatari kwa wasafiri na jamii kwa ujumla.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles