23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

LUGUMI MAMBO MAZITO

*Serikali yasema kama anaidai afuate taratibu, TRA yasema imempa nafasi kulipa deni, taarifa zasambaa kuwa amekamatwa

 

NA MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

 

Mambo kwa mfanyabiashara Said Lugumi, yamezidi kuwa magumu baada ya Serikali kusema kama anaidai afuate taratibu na si kutolipa kodi, huku taarifa za kukamatwa kwake jana zikisambaa.

Taarifa hizo zinakuja ikiwa ni siku moja tangu kusambaa kwa taarifa za nyumba zake tatu kutarajiwa kupigwa mnada Septemba 9, kutokana na deni la Sh bilioni 14 la kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono, Scholastica Kevela, alisema juzi kuwa mnada huo pia utahusisha mashine tatu za kutengeneza mabati.

 

WIZARA YA FEDHA

Msemaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ben Mwaipaja, akizungumza na gazeti hili juu ya taarifa za Lugumi kuidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 300, hakukubali wala kukataa, lakini akasisitiza kuwa anapaswa kufuata sheria na taratibu zilizopo kisheria.

“Inawezekana kweli Serikali inadaiwa, lakini si sababu ya yeye kushindwa kulipa deni linalomkabili eti kisa anadaiwa… kuna taratibu, kanuni na sheria anapaswa kuzifuata juu ya suala lake.

“Kwa hali ilipofikia, anapaswa kuwa mwenye kuangalia kwa makini taratibu za madai yake, kwa sababu tunaamini hata TRA hadi inafikia uamuzi ule, ilifuata sheria zote za nchi,” alisema Mwaipaja.

Alisema kwa siku tisa alizopewa tangu kutolewa kwa tangazo hili, zinamtosha kujipanga vizuri kushughulikia suala lake.

“Amepwa siku tisa na TRA, anaweza kuzitumia kujipanga kulipa deni lake… haya ni mambo ya kisheria,” alisema.

 

TRA YASEMA

Kwa upande wake TRA, ilisema licha ya kutangaza kupiga mnada mali za Lugumi, bado ana nafasi ya kuzikomboa kabla ya siku ya mnada kufika.

Jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alilieleza gazeti hili kuwa kabla ya kutangaza kuuza mali hizo kwa mnada, hatua mbalimbali zilishachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kumtafuta Lugumi ili kujua namna atakavyolipa jambo ambalo halikufanikiwa.

“Ukiona tumefika hatua ya kupiga mnada jua tumepita kwenye hatua zote za awali, ikiwa ni pamoja na kufanya naye mazungumzo na kuangalia hata kama atalipa kwa awamu ili tuandikishiane mkataba.

“Pia hizo nyumba utaona hata tangu tumeziweka utepe ni zaidi ya miezi miwili, hiyo yote ilikuwa ni nafasi ya kuweza kulipa na bado ana nafasi ya kulipa hilo deni mpaka siku ya mwisho ya mnada, ila akikaa kimya mpaka inalia kengele ya tatu, tutakuwa hatuna tena namna,” alisema Kayombo.

Gazeti hili pia lilitaka ufafanuzi juu ya taarifa kwamba Lugumi ameiandikia TRA barua kadhaa, akiwaeleza kuwa anaidai Serikali zaidi ya Sh bilioni 300, hivyo wasubiri akilipwa na yeye atalipa, jambo ambalo Kayombo alisema hata kama ni kweli, suala hilo haliwanyimi nafasi ya kudai mapato ya nyuma.

“Siwezi kusema kama ni kweli ama si kweli kwamba aliandika barua, kwa sababu hilo hadi nifuatilie, lakini hata kama hilo lipo, bado halituzuii kudai kodi ya mapato yake,” alisema Kayombo.

Alipoulizwa kodi wanayodai imetokana na mapato gani, Kayombo alisema hawezi kusema zaidi kwa sababu suala hilo ni kati ya TRA na mteja wao.

“Hili la nyumba nalisema kwa sababu limeshakuwa hadharani, lakini mambo mengine ya mapato yake hayo yalitokana na nini ama ni kiasi gani anadaiwa, hilo siwezi kusema,” alisema Kayombo.

 

TAARIFA ZA KUKAMATWA

Katika hatua nyingine, taarifa zinasema Lugumi anashikiliwa na vyombo vya dola kwa mahojiano jijii Dar es Salaam.

Chanzo chetu kimesema kuwa mfanyabiashara huyo alishikiliwa kuanzia jana saa 10 jioni.

“Kaka huyu jamaa anashikiliwa na vyombo vya dola tangu leo saa kumi (jana), hatujui ni kwa sababu gani, fuatilieni mnaweza kujua undani wake,” kilisema chanzo chetu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alipoulizwa suala hilo, alisema hana taarifa na kumtaka mwandishi wetu kuwasiliana na ofisi ya  Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz.

Alipotafutwa Boaz kupitia simu yake ya mkononi, haikuwa hewani na hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi haukujibiwa.

mwisho

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. M2 kama unadaiwa lipa kwanza den unalodaiwa kisha na wewe udai haki yako maana waweza kukuta unapoteza v2 kwa kudai kuwa na wewe unadai hvyo timza xehemu yako kwanza ndpo uanze upande mwingne wa madai yako.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles