27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mamia wamzika Askofu Mushemba

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MWILI wa Askofu Dk. Samson Mushemba aliyewahi kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), umezikwa nje ya Kanisa Kuu la Bukoba Mjini, huku viongozi mbalimbali wakisema enzi za uhai wake alikuwa mfano wa kuigwa kutokana na utumishi wake kugusa maisha ya wengi.

Dk. Mushemba ambaye alifariki dunia Aprili 9, mwaka huu, wakati akipatiwa matibabu  Hospitali ya Ndolage Kamachumu, alizikwa jana katika kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, huku mazishi yake yakihudhuriwa na viongozi wa mbalimbali wa dini na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Akiongoza ibada ya mazishi, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Frederick Shoo, alisema Askofu Mushemba hakufanya kazi kwa ajili ya kanisa tu, bali kwa jamii nzima ya Watanzania.

“Alikuwa mtumishi wa kitaifa na dunia nzima, amegusa maisha ya wengi na amekuwa mfano wa kuigwa, ametuachia mengi ya kujifunza, ametunza heshima ya utumishi huu tuliokabidhiwa, heshima ya nchi yetu ya Tanzania na kanisa la Mungu. 

“Unaweza kuwa mtumishi, lakini ukawa si mfuasi wa Kristo katika tabia yako, matendo na mwenendo wako mzima. Mfuasi wa kweli wa Yesu anamtii bwana na mwokozi wake, anamfuata huyu Yesu kristo, alikuwa mtu mnyenyekevu, mtu mtii kwa bwana kama baba, mchungaji, askofu, mkuu wa kanisa na kiongozi akawa mtu wa maombi,” alisema Dk. Shoo.

Askofu Shoo pia alisoma salamu za mke wa mkubwa wa Kanisa hilo aliyemtangulia Dk. Mushemba, Askofu Sebastian Kolowa, Elifrida ambaye alisema kiongozi huyo alijaliwa kuwa na hekima na unyenyekevu katika maisha ya huduma.

“Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za msiba wa Askofu Dk. Samson Mushemba, hayati baba askofu alijaliwa hekima na unyenyekuvu katika maisha ya huduma takatifu. Hakujuinua, alikuwa baba mwenye upendo kwa wote, sote tumshukuru Mungu kwa maisha ya huduma ya Askofu Dk. Mushemba,”.

Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, Dk. Abednego Keshomshahara, alisema walishirikiana na Dk. Mushemba  kujenga jamii, kanisa na taifa kwa ujumla.

SALAMU ZA RAMBIRAMBI

Wakitoa salamu za rambirambi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alisema kazi mbalimbali zilizofanywa na Askofu Mushemba zaidi ya miaka 15 katika dayosisi hiyo na miaka 15 kama Mkuu wa KKKT zimewagusa Watanzania wengi.

“Watanzania wengi, nikiwemo mimi mwenyewe wanafaidi matunda ya kazi zake, Chuo cha Tumaini ilikuwa ni kazi ya baba Askofu Samson Mushemba. Ukienda KCMC Watanzania wengi wamepata huduma bora za afya, labda hawajui nani aliimarisha huduma katika hospitali ile. 

“Katika mkoa wetu wa Kagera, amefanya mengi, umoja uliopo miongoni mwa madhehebu mbalimbali katika mkoa huu, kuna uimara na ushirikiano mkubwa sana kati ya Serikali na viomghozi wa dini.

“Sikuwahi kufikiria chimbuko la haya ambayo yapo sasa wako watu walitangulia wakasimamia na kuweka misingi hiyo. Kwa yale aliyoyafanya katika hali ya kawaida si rahisi ‘ku – copy and paste’.

“Nilipata bahati ya kuwa naye karibu, lakini kwa siku ya leo (jana) jambo ninaloweza kujifunza ni kuwa na uwezo wa kukiri baada ya kukosea kama ambavyo yeye alikuwa na uwezo huo. La pili ni kuwa na uwezo wa kutolalamika, tuendelee kuwajibika na tuache kulalamika,” alisema.

Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Dk. Methodius Kilaini, alisema Dk. Mushemba alishiriki kuimarisha uhusiano mzuri baina ya makanisa. 

“Hapa Bukoba aliendeleza ushirikiano kati ya madhehebu mbalimbali na hata waislamu katika miradi mingi. Tunaahidi kuendeleza ushirikiano huo, baba Askofu Samson Mushemba kwa heri ya kuonana,” alisema Askofu Kilaini.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ambayo inajumuisha makanisa ya kiinjili zaidi ya 13, Askofu Alinikasa Cheyo, alisema Askofu Mushemba aliwahi kuwa makamu wa CCT na baadaye alikuwa mwenyekiti hivyo msiba huo umewagusa kipekee.

MTOTO WA MAREHEMU

Mtoto wa marehemu, Josephat Mushemba, alisema baba yao alipenda kuwa na uhusiano na watu wote na hata alipostaafu alichagua kuishi kijijini, huku akiwasaidia watu mbalimbali.

“Hakuwa na ubaguzi kwa watoto, hakuwa na ubaguzi wa dini, nyumba ya baba imekuwa ni nyumba ya watu wa dini zote, tuliishi na watu wa aina mbalimbali na kabila mbalimbali.

“Alikuwa tayari kuomba msamaha kwa watu wote hasa kwetu sisi watoto pale alipokuwa amekosea au kumkwaza yeyote, kwa mfano miaka 10 iliyopita alimpelekea ndugu yake kitenge sasa yule ndugu yake alichukia sana.

“Akasema (yaani ndugu husika) kwanini unaniletea kitenge akamrushia, baba hakusema chohote aliondoka na kukiacha. Baba alianza kulia akasema muende mumlete yule mama alipo nimuombe msamaha kabla sijafa

“Tulimuomba baba yetu mkubwa aende kumfuata yule mama kusudi amuombe msamaha, baba akasema mpelekeeni Sh 20,000 za chakula alizokuwa akidai,” alisema.

Josephat alisema pia baba yao hakuwa mtu wa malalamishi na hakuomba mtoto amsaidie.

“Mara nyingi ungechukua wiki moja bila kumpigia simu, baadaye ukampigia ukasema baba naomba unisamehe sikupiga simu muda mwingi, anasema lakini mbona umepiga leo haukupiga kesho, anasema hiyo haina shida…suala la kumsaidia kama hujajiongeza hautamsikia anakuomba,” alisema.

Alisema muda wote ambao walikuwa baba yao aliwatayarisha kwani alijua kwamba wakati wake umewadia.

“Alikuwa anasikia maumivu, alisema sidhani kama mnapaswa kunipeleka hospitali nirudisheni niende nikafie nyumbani, nafikiri wakati wangu umewadia, tulikataa sisi kama watoto,” alisema.

Alisema alipostaafu alipenda kwenda kuishi kijijini na walipomuuliza alisema anataka kwenda kuishi na watu wake wasio na uwezo awasadie mpaka nguvu zitakapoisha.  

“Wanafamilia tuliamua tukamjengea nyumba mjini na tukamuomba kwa kumpigia magoti, tukasema ukae hapa utakuwa unaenda na kijijini, lakini alisema mtajenga nyumba nzuri labda mnipe chumba cha nyumba nitakuwa nakuja nalala siku mbili narudi kijijini.

“Mimi sijui alikuwa mtu wa namna gani, ametufundisha mengi, zaidi kumtegemea Mungu katika maisha yetu, hakika tutamkosa na kwa kweli tutamkumbuka daima, atakuwa ni hazina inayudumu ndani ya maisha yetu,” alisema Josephat.

Askofu Mushemba  alizaliwa Juni 30, 1935 ameacha mjane, watoto saba, wajukuu 22 na kitukuu kimoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles