LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewataka watu wenye taarifa kuhusu tukio la kutekwa kwa raia wa Kenya, Raphael Ongangi, waziwasilishe zifanyiwe kazi.
Raia huyo anayeishi nchini, anadaiwa kutekwa tangu Juni 24 na hadi sasa hajulikani alipo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema taarifa za sehemu ambazo Ongangi alipelekwa tangu alipotekwa zilizotolewa na Zitto ni taarifa za mitandao na wao hawafanyii kazi mambo ya mitandao.
“Hizo habari za mitandao kila mmoja anatoa anavyofikiria, cha msingi ambacho sisi tungeweza kukiona cha maana kama kuna jambo lolote lipelekwe kituo cha polisi, ofisi yangu ipo, kama kuna mtu ana taarifa alete, lakini hizo na sisi tunazisikiliza kama unavyozisikiliza wewe,” alisema Mambosasa.
Jana, Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, aliiomba Serikali kulipa uzito unaostahiki suala la kutekwa kwa Ongangi.
Zitto alisema Ongangi alikuwa akifanya naye kazi kama msaidizi wake tangu mwaka 2009 hadi 2016.
Hata hivyo, alisema hana taarifa zozote dhidi yake kwani hafanyi kazi naye kwa miaka mitatu sasa.
“Tangu mwaka 2009 mpaka mwaka 2016 Raphael amekuwa akifanya kazi nami akiwa msaidizi wangu, hata baada ya kuamua kufanya biashara za usafirishaji, aliendelea kuwa mtu wa karibu yangu mpaka alipotekwa Juni 24.
“Tunaambiwa watekaji wanataka taarifa zangu kutoka kwa Raphael, napenda kuwajulisha kuwa Raphael hafanyi kazi nami kwa miaka mitatu sasa, kwa hiyo hana analojua,” alisema Zitto.
Kwa mujibu wa Zitto siku aliyotekwa Ongangi maeneo ya Oysterbay, Dar es Salaam alikuwa na mke wake Veronica wakitokea shuleni kwa mtoto wao kushiriki kikao cha wazazi.
“Raphael amefunga ndoa na Mtanzania Veronica Kundya, ana watoto wadogo wawili ambao wiki moja sasa hawajui baba yao yupo wapi. Wamuache ajiunge na familia yake,” alisema.