28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mama aua watoto wake, awafukia ndani ya nyumba

IMG-20150126-WA0001NA THOMAS MURUGWA, TABORA
JESHI la Polisi linawashikilia watu wawili wakazi wa Manispaa ya Tabora kwa tuhuma za kuwanyonga watoto wawili hadi kufa, kisha kuwafukia ndani ya nyumba waliyokuwa wanaishi.
Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kufanyika juzi saa moja jioni katika eneo la Chechem Manispaa ya Tabora walikokuwa wakiishi watuhumiwa wa mauaji hayo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Juma Bwire, amethibitisha jana kutokea kwa mauaji hayo ya kikatili na kuwataja watuhumiwa kuwa ni mama mzazi wa watoto hao, Zuhura Masoud (25) na baba yake Shaban Ramadhan (75) wakazi wa Kata ya Chemchem mjini Tabora.
Aliwataja watoto hao waliouawa ni Mwamvua Mrisho (4) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Sudi, anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi 4.
“Baada ya mama huyo kutekeleza unyama huo, aliwafunga kwa kuwavingirisha mifuko ya sandarusi kisha kuwafukia chini, mmoja sebuleni na mwingine chumbani kwake.
“Tulipata taarifa tukazifanyia kazi kwa weledi wetu na kubaini ukweli wa mauaji hayo. Huyu mwanamke na baba yake mzazi mzee Ramadhani tunawashikilia kwa mahojiano zaidi.
“Tunazo taarifa kwamba hawa watu walikuwa wakigombea nyumba kati yao, na inawezekana ugomvi huo labda ndiyo chanzo halisi cha mama huyo kuamua kuchukua uamuzi mgumu kama huo wa mauaji ya kinyama kwa wanawe wawili,” alisema Kamanda Bwire.
Alisema polisi mkoani hapa wanaendelea kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini chanzo halisi cha mauaji hayo, na baadaye watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles