24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Muhongo akacha makabidhiano ya ofisi

prof muhongoNa Waandishi Wetu, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wamekacha makabidhiano ya ofisi hatua iliyofanya mawaziri wapya kukabidhiwa ofisi na watendaji.
Mialiko iliyokuwa imetolewa, ilisema mawaziri hao wangekabidhi ofisi kwa wateule wapya, William Lukuvi, aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na George Simbachawene wa Nishati na Madini.
Kutokana na kutotokea kwa Profesa Muhongo, ilimlazimu Simbachawene akabidhiwe ofisi na wakabidhiwe ofisi na watendaji wa wizara husika.
Baada ya Lukuvi kukabidhiwa ofisi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Alphayo Kidata, alieleleza mikakati yake huku akisema namna wizara hiyo ilivyokuwa ya moto.
Alisema anaifahamu vizuri wizara hiyo kutokana na kuwapo kwa mtandao wa watendaji wanaoshirikiana na matajiri kutapeli wananchi.
Alizungumzia alivyoshughulikia migogoro ya ardhi alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba aliweza kusambaratisha mtandao wa ufisadi wa ardhi kwa kuhamisha watendaji wote wa manispaa tatu zinazounda jiji hilo.
Alisema wananchi wamejenga dhana kwamba wizara hiyo inaongozwa na watu waliojaa dhuluma wakishirikiana na watu wenye fedha, ambao huwanyanyasa wanyonge na masikini.
Lukuvi alisema anafahamu vema kinachoendelea, hivyo atahakikisha anauondoa mtandao huo.
“Naingia katika wizara hii nikiwa na akili timamu, ninajua humu ndani kuna moto, najua migogoro ya ardhi inasababishwa na watendaji, huu ni ujumbe rasmi nawapa, nawachukia sana watu wasiotoa haki na kufanya dhuluma kwa wananchi,” alisema Lukuvi.
Alisema ataanza kuzunguka mikoani kusikiliza kero za wananchi juu ya migogoro ya ardhi kwa sababu anajua masikini wengi hawana uwezo wa kwenda Dar es Salaam kueleza shida zao.
Lukuvi alisema anafahamu ufinyu wa bajeti uliopo serikalini, lakini akasema utatuzi wa migogoro ya ardhi unahitaji uamuzi zaidi kuliko fedha.
Tibaijuka nimetoka kwa bahati mbaya
Akizungumza wakati wa kukabidhi ofisi yake, aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Anna Tibaijuka, alisema alichaguliwa kwa bahati nzuri kuongoza wizara hiyo, lakini ameondoka kwa bahati mbaya.
Alisema mambo aliyoyaacha ni vizuri wakayaendeleza ikiwemo kushughulikia migogoro wakazi wa jiji la Dar es Salaam wa wa maeneo ya Chasimba, Kigamboni na kwingineko.
SIMBACHAWENE AMWACHIA MUNGU
Kwa upande wake, Simbachawene, amewashangaa watu wanaohoji kuhusu uwezo wake na kusema suala hilo anamwachia Mungu.
“Hiyo ni mitazamo ya watu. Mtu kama hakupendi huwezi kumlazimisha akupende, kama anakutilia shaka huwezi kumlazimisha asikutilie shaka…Mungu amempa kila mtu karama yake. Acheni nitumie fursa hii kuonyesha kile alichonipa na acheni Mungu afanye kazi yake,” alisema Simbachawene.
“Hatukuja kuendesha wizara, tumekuja kusimamia. Wizara ina waendeshaji tayari ambao tena hawabadiliki, sisi tumekuja na tutawaacha, hao ndio tunaowasimamia na kuhakikisha mambo yanakwenda kama inavyotakiwa, hivyo sisi ni kama washereheshaji tu,” alisema Simbachawene ambaye aliambatana na naibu wake Charles Mwijage.
Kuhusu usiri wa mikataba ya gesi, alisema: “Sasa tupeni siku chache ili tuangalie huo usiri unaosemwa ni upi na tutakuja na majibu yake.”
Kabla ya uteuzi huo, Simbachawene alikuwa Naibu Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles