25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Malumbano madiwani CCM halmashauri yamkera JPM

Na ANDREW MSECHU                             

RAIS Dk. John Magufuli amewataka viongozi wa CCM na wale wa halmashauri kuacha malumbano kwa kuwa tabia hiyo inasababisha kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

Akizungumza katika mkutano wake na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo mkoani Mbeya jana, Rais Magufuli alisema ana taarifa za kuendelea kuwepo malumbano ya kisirisiri baina ya madiwani na viongozi wa halmashauri hiyo kuhusu miradi ya maendeleo.

“Viongozi wa halmashauri na wa CCM waache malumbano ya kisirisiri. Nasikia mara diwani huyu, mara huku, mara mradi huu, mara nani, nataka nizungumze hili kwa uwazi, nalisema hili kwa sababu msema kweli mpenzi wa Mungu,” alisema.

Alieleza kuwa ana taarifa kuhusu mabishano ya ujenzi wa kituo cha afya na kumtaka Diwani wa Kata ya Lufilyo, Lucas Mwamafupa (CCM) aeleze kuhusu mvutano huo.

Katika maelezo yake, diwani huyo alisema kwa mujibu wa Ilani ya CCM, kila kata inatakiwa iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati, lakini zipo nyingine zinajengwa hospitali zaidi ya moja zenye hadhi ya vituo vya afya wakati nyingine hazina.

Hata hivyo, alisema ni taasisi binafsi ndizo zinazojenga vituo vya afya kwenye kata ambazo tayari kuna kituo cha afya cha Serikali.

Kutokana na maelezo hayo, Rais Magufuli aliagiza taasisi hizo binafsi ziachwe zijenge kadiri ziwezavyo katika maeneo wanayoona yanafaa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema kama kuna mgogoro ni wa madiwani wenyewe kwa sababu suala hilo liko chini ya Baraza la Madiwani ambalo lina uwezo wa kuamua mambo ya maendeleo.

Awali, akizungumza katika uzinduzi wa kiwanda cha kusindika maparachichi Rungwe, Rais Magufuli aliwataka wawekezaji kuangalia namna ya kuboresha masilahi ya wafanyakazi wao na kutoa bei nzuri kwa wakulima, wakati Serikali ikiendelea kuangalia namna ya kuwaboreshea mazingira ya uwekezaji.

“Kweli Serikali inatambua kuwa wawekezaji wamekuwa wakisumbuliwa kutokana na utaratibu wa marejesho ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani), lakini nao mnatakiwa kuhakikisha mnasaidia kuinua maisha ya wafanyakazi wenu na wakulima,” alisema.

Alisema Serikali imekuwa ikifuatilia kwa karibu suala hilo la marejesho ya VAT kutokana na ununuzi wa vifaa vya uzalishaji vinavyoingizwa na wawekezaji, ambalo liko kwa muijbu wa sheria, lakini liliingia dosari kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kufanya udanganyifu.

“Suala hili liliingia dosari baada ya kubaini kwamba kuna baadhi ya watu walikuwa wakitumia hiyo kama njia ya kufanya udanganyifu. Utakuta mtu ananunua kifaa kwa shilingi milioni tano anaandika milioni hamsini. Ananunua kifaa milioni hamsini anaandika milioni mia tano, kwa hiyo Serikali ilikuwa inajikuta inapoteza fedha nyingi.

“Tumeliwa sana kwenye suala hili la ‘refund’ ya VAT. Ila viongozi wapo, tunawahakikishia wawekezaji kuwa wapeleke malalamiko yao na itakuwa rahisi sana kulipwa kama hakutakuwa na suala la kuongeza gharama. Leteni hayo madai yenu, ila msiongeze, ikiwezekana mpunguze.  

“Wakati Serikali inashughulikia kumaliza matatizo yenu, na nyie hebu angalieni kidogo kuhusu bei ya mazao ya wakulima, hata wafanyakazi wenu muangalie mishahara yao, iwe mizuri ili nao pia wanufaike, hivyo ndivyo mambo yanavyokwenda,” alisema.

Alisisitiza kuwa hiyo itasaidia pia kujenga uchumi wa wakulima na wa wafanyakazi ambao pia watatakiwa siku moja nao waweze kuanzisha viwanda vyao katika maeneo hayo na kuchangia kuinua uchumi wa nchi.

Akiwa katika uzinduzi huo, Rais Magufuli alionesha kukerwa na malalamiko ya wanafunzi katika Shule ya Msingi Ilembe iliyopo katika eneo hilo, ambao walidai kuwa shule hiyo haina umeme wala mashine ya kudurufia.

Kahusu malalamiko hayo, Rais Magufuli alimwagiza mhandisi wa umeme katika Wilaya ya Rungwe kuhakikisha anafikisha umeme shuleni hapo ndani ya siku 10 na alichangia Sh milioni moja, ambayo aliagiza Sh 500,000 itumike kufunga mfumo shuleni hapo na Sh 500,000 itumike kwa uwezeshaji wa umeme kufika shuleni hapo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitoa Sh milioni moja na kumkabidhi mwalimu mkuu wa shule hiyo kwa ajili ya kuongezea kwenye ununuzi wa mashine ya kudurufia akiwa na uhakika kuwa ipo fedha ambayo ilikuwa ikiendela kukusanywa kununua mashine hiyo.

Akiwa katika mji wa Busokelo Rais Magufuli alieleza kufurahishwa kwake baada ya kukutana na Profesa Mark Mwandosya ambaye amewahi kuwa mbunge wa Ruangwa na Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu na ya Nne.

Alisema wakati akiwa Waziri wa Miundombinu na Profesa Mwandosya akiwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia mazingira, alikuwa akimsumbua sana kuhusu ujenzi wa barabara ya Busokelo ambayo jana alizindua kilometa 10 kati ya 81 na kwamba atahakikisha inajengwa yote kwa kiwango cha lami.

“Profesa Mwandosya alikuwa akinisumbua sana kuhusu hii barabara, tukawa tunachora ananiambia ni kilometa 75, lakini kumbe ni kilometa 81 na hizo nyingine alikuwa haniambii, ila alikuwa anataka tu anionyeshe umuhimu wa hii barabara. Sasa tumeianza na ninashukuru kwamba mimi ndiye niliyeizindua mwenyewe. Tunaendelea kujenga barabara iliyobaki,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles