26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mabilioni yamwagwa mikopo elimu ya juu

Na ARODIA PETER -Dodoma

WANUFAIKA wa mikopo ya elimu ya juu wanatarajia kuongezeka baada ya Serikali kuongeza bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika mwaka wa fedha 2019/20.

Akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema Serikali inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 450 ambayo ni ongezeko la asilimia tano kulinganishwa na mwaka 2018/2019.

Profesa Ndalichako alisema Bodi ya Mikopo imepanga kutoa mikopo kwa wanafunzi 128,285 sawa na ongezeko la asilimia 4.5.

Alisema wanafunzi 45, 485 watakuwa wa mwaka wa kwanza ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.3 kulinganisha na wanafunzi 41,234 wa mwaka 2018/2019.

Mbali na hilo, alisema wanatarajia kukusanya Sh bilioni 221.5 kutoka kwa wanufaika ambao mikopo yao imeiva sawa na asilimia 40.5 kulinganishwa na lengo la mwaka 2018/2019.

Katika hotuba hiyo, pia Profesa Ndalichako alisema Taasisi ya Elimu Tanzania kwa mwaka 2019/2020 inatarajia kuandika muhtasari wa lugha ya Kichina kwa kidato cha tano na sita ambayo inafundishwa katika shule sita za Serikali.

“Taasisi ya Elimu pia inatarajia kuandaa mtaala wa muhtasari wa somo la Kiswahili kwa shule za msingi na sekondari za nchi ya Afrika Kusini na nchi nyingine zitakazowasilisha maombi ikiwamo Sudani Kusini ambapo ukuzaji wa lugha hiyo ni moja ya vipengele katika mkataba wa makubaliano uliosainiwa hivi karibuni kati ya nchi hiyo na Tanzania,” alisema.

MICHANGO YA WABUNGE

Wakichangia hotuba hiyo bungeni jana, baadhi ya wabunge walishauri yafanyike mabadiliko makubwa katika idara ya uandikaji wa vitabu na mitaala ya elimu ili kuondoa mkanganyiko uliopo.

Wa kwanza kuchangia hoja hiyo ni Mbunge wa Mlalo, Rashidi Shangazi (CCM) ambaye alisema sera ya elimu ya mwaka 2014 inaeleza kuwa elimu ya msingi itaishia darasa la sita. Hata hivyo suala hilo limeshindwa kutekelezeka na Serikali ipo kimya bila kulitolea ufafanuzi.

“Mheshimiwa mwenyekiti, sera ya elimu ya mwaka 2014 inaeleza wazi kwamba ‘standard seven’ (darasa la saba) itaishia darasa la sita, ni lini sera hii itatekelezwa kwa sababu mpaka sasa wanafunzi wetu wa standard seven wanakwenda shuleni kuota jua, sasa sijui watakuwa wanasoma mitaala ipi?”  alihoji Shangazi.

Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo (CCM) alitishia kuondoa shilingi endapo hatapata majibu ya kuridhisha kuhusu makosa yaliyofanywa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TET) kupitisha vitabu vyenye makosa na kusababisha hasara kwa wamiliki wa shule binafsi.

“Mwaka juzi vitabu vilivyokuwa vimetolewa na TET viliondolewa na Serikali kwa sababu vilikuwa na makosa, lakini wakati uamuzi huo unachukuliwa tayari wamiliki wa shule binafsi tulikwishanunua vitabu hivyo.

“Sasa nataka waziri anieleze kama wamiliki binafsi watarudishiwa hizo gharama zao walizokwishaingia kwa sababu hayakuwa makosa yao,” alisema Mulugo na kuongeza:

“Ninaiomba Serikali kukaa meza moja na wamiliki wa shule binafsi ili wawashauri namna ya kwenda, kwa mfano hakuna vitabu vilivyoandikwa lugha ya Kiingereza kwa darasa la tatu, lakini pia wamiliki hawa wameendelea kutozwa kodi za mabango, vifaa vya zimamoto ambazo zilikwishafutwa na waziri, lakini halmashauri wameendelea kuzidai, ninaomba Serikali mtupe waraka ili kuepuka kadhia hii.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles