Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MALIPO kuhusu mkopo kwa Tanzania kupitia benki ya Standard ambao benki hiyo iliutoa kupitia benki ya Stanbic yanazidi kupingwa na Watanzania, huku wasomi maarufu na wanasiasa wakiunga mkono hatua hiyo.
Wanaopinga malipo hayo ni pamoja na wabunge, wanasiasa na wasomi wa kada mbalimbali ambao wameungana na Watanzania 1,750 wa ndani na nje wakitaka suala hilo lichunguzwe upya na mkopo huo ufutwe.
Miongoni mwa waliounga mkono hatua hiyo ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM).
Bashe, wakati akihojiwana kituo kimoja cha radio juzi, alisema anaunga mkono hatua ya Rais Dk. John Magufuli, kuirudisha nchi kwenye mstari na kuzuia kila aina ya wizi unaofanyika nchini.
Alisema anaamini suala la mkopo huo pia litaungwa mkono na viongozi wote wa Serikali kwa vile kama hatua hiyo haitachukuliwa kuna hatari ya nchi kulipa mkopo wenye shaka.
“Ni lazima katika hili Watanzania wote tuungane na uchunguzi ufanyike upya badala ya kulipa deni hili lenye shaka. Vinginevyo nchi yetu itageuka shamba la bibi la kila mtu kufanya analoweza huku Watanzania maskini wakiendelea kuumia,” alisema Bashe.
Wengine waliounga mkono hatua hiyo kwa kusaini hoja ya kufanyika uchunguzi ni Profesa Issa Shivji na Profesa Ibrahim Lipumba.
Pia wamo Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Makongoro Nyerere na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kasesela ambao nao wamesaini hati hiyo ya kutaka suala hilo lichunguzwe.
Katika suala hilo ambalo sasa linachunguzwa na vyombo vya Tanzania, benki ya Stanbic iliikopesha serikali dola za Marekani milioni 600 (Sh Sh trilioni 1.2), mkopo wenye riba ya asilimia sita inayolipwa kwa miaka minne.
Mkopo huo ulichunguzwa na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Uingereza (SFO) na kuonekana ulikuwa na mazingira ya rushwa ingawa wanaotuhumiwa hadi sasa ni viongozi wa serikali ya Tanzania na wafanyakazi wa benki ya Stanbic.