30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Polisi wamkamata kigogo wa CUF Z’bar

Hamad Masoud HamadNA SARAH MOSSI, ZANZIBAR

JESHI la Polisi Visiwani Zanzibar  linamshikilia Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, wa Chama cha Wananchi (CUF), Hamad Masoud Hamad, kwa tuhuma za kutoa kauli za uchochezi kuelekea kwenye uchaguzi wa marudio,   Machi 20 mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam, jana alithibisha kushikiliwa kwa kiongozi huyo kwa ajili ya mahojiano.

Alisema ni  kutokana na kauli alizozitoa  akiwa Kisiwani Pemba hivi karibuni.

“Ndiyo tumemkamata alfajiri ya leo (jana) na tunamuhoji  kutokana na kauli zake na mambo yanayoendelea hivi sasa ya ulipuaji mabomu sehemu mbalimbali.

“Tumeamua kumfuata nyumbani kwake alfajiri kwa sababu  kwa siku tatu tulikuwa tukimtafuta hapatikani,” alisema Kamanda Mkadam.

Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu kadhaa kwa mahojiano.

Alipoulizwa idadi ya watu wanaowashikilia alisema   ni kubwa na kila siku wanaongezeka.

Hata hivyo, Kamanda Mkadam,  alishindwa kueleza   kauli zinazodaiwa kutolewa na kiongozi huyo wa CUF, ambazo ni za uchochezi.

Taarifa zinasema   Masoud akiwa mjini Unguja hivi karibuni, alitoa kauli   akililaumu Jeshi la Polisi kuegemea upande mmoja katika kufanya kazi.

Alisema jeshi hilo limekuwa likiwakamata wafuasi wa CUF pekee wakituhumiwa kujihusisha na matukio ya ulipuaji mabomu sehemu mbalimbali mjini hapa.

Inadaiwa Masoud pia aliwatuhumu polisi kwa kusababisha wananchi kadhaa kisiwani Pemba kukimbilia nchi jirani za Kenya na Somali kutokana na matukio ya kuwapiga na kuwashambulia wananchi wanaodaiwa ni wafuasi wa CUF.

Akizungumzia   kukamatwa kwa Masoud, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema tukio la kukamatwa kwa kiongozi mwenzao wanalifuatilia kwa karibu.

“Ndiyo tuko njiani tunaelekea Madema, hatujui sababu za kumkamata, ndiyo tunakwenda kuwasikiliza,” alisema Mazrui.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, alisema vyombo vya dola vimejipanga kuhakikisha hakuna tukio la kuvunja amani siku ya kupiga kura na baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa marudio.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi   Jumapili kwa ajili ya kwenda kupiga kura.

Akizungumza na waandishi wa habari   mjini Unguja jana, alisema ni lazima wananchi watumie haki yao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa marudio.

Kitwanga alisema matukio ya ulipuaji mabomu katika sehemu mbalimbali yamelenga kuwatisha wananchi wasijitokeze kupiga kura  siku ya uchaguzi huo.

“Anayetaka kwenda kupiga kura Jumapili kwa ajili ya kuchagua viongozi aende na ulinzi wake upo lakini kwa mtu ambaye hayupo tayari kupiga kura basi akae nyumbani na asitumie nafasi yake kukera wenzake kwa kuwazuia,” alisema.

Wananchi wa Zanzibar wanatarajiwa kupiga kura Jumapili Machi 20  baada ya uchaguzi wa wa Oktoba 25  mwaka jana kufutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha kwa sababu mbalimbali.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,391FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles