29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Malinzi aongoza wadau maziko ya Mwenyekiti Azam

Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa timu ya Azam FC, Said Mohamed Abeid kuelekea katika Makaburi ya Kisutu kwa mazishi, Dar es Salaam jana.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa timu ya Azam FC, Said Mohamed Abeid kuelekea katika Makaburi ya Kisutu kwa mazishi, Dar es Salaam jana.

Na MOHAMED MHARIZO-DAR ES SALAAM

RAIS wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi, amewaongoza wadau mbalimbali wa soka katika maziko ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Azam FC, Said Mohammed Abeid.

Marehemu amezikwa jana katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka.

Kabla ya kuzikwa, marehemu aliswaliwa katika msikiti wa Maamour uliopo Upanga. Baadhi ya waliohudhuria maziko hayo ya kiongozi huyo ambaye pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ni pamoja na Makamu wa Rais TFF, Wallace Karia, Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Celestine na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Kigoma, Msafiri Mgoyi.

Wengine ni Rais wa zamani TFF, Leodegar Tenga, Mkurugenzi wa zamani wa ufundi na wa sasa, Sunday Kayuni na Said Madadi, Makamu Mwenyekiti Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na wengine wengi.

Rais Malinzi amemwelezea marehemu kuwa ametoa mchango mkubwa katika soka na wamefanya naye kazi Kamati ya Utendaji na alisimamia ukweli.

“Suala la msingi ni kumwombea dua ili aweze kupumzika kwa amani, ila tunatambua mchango wake mkubwa,” alisema.

Wakati huo huo Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa), kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti huyo.

Taarifa iliyotumwa na Katibu wa Chama hicho, Samir Mhando, ilieleza kuwa atakumbukwa na waandishi wa habari za michezo kutokana na ukaribu wake na wanahabari na alikuwa na ushirikiano wa kutosha pale alipoombwa kufanya hivyo.

“Alikuwa kiungo kikubwa kwa Taswa kufanikisha matukio mbalimbali ya udhamini,

tunatoa pole kwa familia ya marehemu, klabu ya Azam na wanamichezo wote hapa nchini katika kuomboleza kifo cha Mzee Said, huku tukiwatakia moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles