24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RC Malima azitaka halmashauri kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma

Na Clara Matimo, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ameziagiza halmashauri mkoani humo kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma yanayolenga kuwakumbusha kutimiza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuleta ufanisi wa kutoa huduma kwa wananchi.

Pia, ameuomba uongozi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, kutoa mafunzo ya sheria ya mgawanyo wa mamlaka kwa viongozi wa umma mkoani humo ili kuwaepusha kutoelewana kati ya mkuu wa wilaya na mkurugenzi au mwenyekiti wa halmashauri pamoja na mkurugenzi jambo ambalo husababisha miradi kuchelewa kukamilika.

Malima ameyasema hayo leo Mei 5, mkoani humo alipokuwa akifungua mafunzo ya maadili kwa viongozi wa umma wa mkoa huo yaliyolenga kuwakumbusha viongozi na wakuu wa taasisi za umma mkoani humo kuzingatia kanuni, sheria na taratibu wakati wa kutekeleza majukumu yao, kujiepusha na masuala yote yanayoweza kuwaingiza kwenye mgongano wa maslahi na kuzingatia suala la uwajibikaji wa pamoja.

Amesema maadili kwa watumishi wa umma ni nguzo muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo, hasa kwa taasisi zinazotekeleza miradi ambayo lengo lake ni kuwanufaisha wananchi na kwamba suala la uwajibikaji wa pamoja ni muhimu katika kuwaletea wananchi maendeleo ya haraka.

“Mfano Mwauwasa, TARURA, RUWASA, TANESCO na REA mnapokosa uadilifu mkakoroga mradi anayetukanwa na wananchi ni Rais na Chama Cha Mapinduzi wakati lengo la serikali ni kuinua maisha ya wananchi kiuchumi naomba niwe muwazi ndani ya mkoa wa Mwanza sitawavumilia watumishi wasio waadilifu,” amesema Malima na kuongeza:

“Kumekuwa na mmomonyoka mkubwa wa ukiukwaji maadili kwa baadhi ya watumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao ikiwemo miradi ya maendeleo hali inayosababisha itekelezwe chini ya kiwango ikiwa haina thamani halisi ya fedha, suala la mgongano wa maslahi kwa viongozi wa umma katika utumishi wa umma limekuwa likiathiri sana ufanisi kwenye utendaji wa majukumu ya serikali,” amesema.

Upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia maadili uadilifu na kuwa wazalendo huku wakiwajibika ili kukidhi matarajio ya wananchi kwa serikali yao katika kuwaletea maendeleo.

Baadhi ya Viongozi wa umma mkoani Mwanza wakiwa kwenye mafunzo ya maadili ya viongozi wa umma.

Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, Godson Kweka, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mada tatu ambazo ni sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambapo watakumbushana misingi ya maadili ya umma kama ilivyoainishwa kwenye sheria hiyo, mgongano wa maslahi na uwajibikaji wa pamoja katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, Kweka amewataka watumishi wa umma wa mikoa ya kanda ya ziwa kuheshimu viapo vyao vya ahadi ya uadilifu walivyoapa kwa nyakati tofauti walipopewa dhamana ya nafasi walizonazo.

“Kwa sasa kipaumbele kikubwa cha sekretarieti ya maadili ya umma pamoja na mambo mengine ni kuhimiza suala zima la uwajibikaji wa pamoja kwa viongozi, watumishi na wananchi katika ushirikishwaji ili kuwaletea wananchi maendeleo,” amsesema na kuongeza:

“Sisi sote ni mashahidi, hatuna shaka na tunakila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyotafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali katika halmashauri zetu kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo miradi hiyo inahitaji kuwa na viongozi waadilifu kwenye usimamizi wa fedha na usimamizi wa rasilimali zingine ambazo zipo kwenye maeneo yao ya kazi,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles