25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Malecela: Ni kosa kubwa kumlinganisha Rais Magufuli na Mwalimu Nyerere

Na EVANS MAGEGE


WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Pili, John Malecela, ni miongoni mwa viongozi wachache nchini  waliobahatika kufanya kazi kwa muda mrefu na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Wakati Taifa likiadhimisha miaka 19 ya kifo cha Baba wa Taifa, MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano maalumu na Malecela nyumbani kwake, Upanga Sea View, jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano hayo, amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwamo kauli ya Mwalimu Nyerere juu ya kukijenga chama imara chenye uwezo wa kuikemea Serikali pamoja na mtazamo wake kuhusu ulinganifu wa utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli na Mwalimu Nyerere.

MTANZANIA Jumapili: Wewe ni miongoni mwa watu waliokuwa karibu na Mwalimu Nyerere. Je, ni kauli gani unaikumbuka aliyowahi kukuambia ambayo huwezi kuisahau?

MALECELA: Kuna siku Mwalimu Nyerere alifiwa na dada yake, nakumbuka ilikuwa usiku, tulikwenda mimi na Paul Sozigwa (aliyekuwa mwandishi wa habari wa Hayati Mwalimu Nyerere).

Katika mazungumzo Mwalimu alisema chama anachokitaka ni lazima kiwe kina nguvu, kwamba hata Kamati Kuu (CC) ikimuita hata waziri anatetemeka.

Mwalimu Nyerere aliishi na akakiona hicho kitu, na hata wakati ule anang’atuka madarakani ilikuwa mtu ukiitwa na Kamati Kuu au Halmashauri Kuu lazima utetemeke, kwa sababu Mwalimu alitaka chama kiwe na nguvu kuliko serikali.

Alilenga kwamba watumishi wote, wakiwamo wa Serikali, wawe wanafanya kazi, lakini wakikiogopa na kukiheshimu chama. Kwa kweli hiyo kauli sikuisahau na sitaisahau.

MTANZANIA Jumapili: Mazingira hayo bado yanaishi hadi sasa?

MALECELA: Nasema hayo yalikuwa nyuma, lakini kwa sasa nawaachieni nyinyi mfanye utafiti.

MTANZANIA Jumapili: Nini mtazamo wako kuhusu kumbukizi ya miaka 19 ya kifo cha Mwalimu?

MALECELA: Jambo hili lina maana kwangu na Watanzania wote kwamba tuna uhakika huyu ndiye Baba wa Taifa letu.

Katika ulimwengu wote kila nchi ina Baba wa Taifa, hivyo kumbukumbu hii inatuonyesha kumtambua kuwa Mwalimu Nyerere ndiye kwanza aliongoza harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo na baadaye Tanzania na mpaka akatuvusha salama.

Nasema alituvusha salama kwa sababu tunayo mataifa mengine ya Afrika ambayo hayakupata uhuru kwa amani kama sisi.

Pia, kumbukizi hii ina maana kubwa sana ya kutambua msisitizo wa kina wa Mwalimu Nyerere juu ya umoja wetu kupitia lugha ya Kiswahili.

Hatua hii kubwa imetufanya Watanzania kuwa kitu cha kipekee na adimu ukilinganisha na mataifa mengine, nina hakika wengi watafuata mfano huo kwa sababu Kiswahili si lugha ya kabila moja, bali ni mchanganyiko ya makabila mbalimbali.

Mwalimu alihakikisha mfumo wa elimu unawaunganisha wote na alijenga mfumo imara wa serikali ambao ni shirikishi uliojijenga kitaifa zaidi.

Kwa maana hiyo, ni jambo la kujivunia kuwa na Baba wa Taifa,  hivyo sisi hatuna budi kuchukua mema yake na kuyafuata na huu ni msingi mzuri wa kibinadamu.

 

MTANZANIA Jumapili: Ulipata kufanya kazi na Baba wa Taifa, kwa karibu na muda mrefu,  “unamisi” nini tangu afariki duniani?

MALECELA: Ni kweli nimefanya kazi kwa muda mrefu na Baba wa Taifa katika vyeo vya juu, kuanzia mwaka 1963 aliniteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, nyakati zile ukiwa mkuu wa mkoa ina maana ndio katibu wa chama wa mkoa na pia moja kwa moja ukiwa na nafasi hiyo unakuwa ni mbunge wa mkoa.

Kitu ambacho nilijifunza kwake alikuwa ni mvumilivu sana na alipenda kusikiliza watu, alikuwa na ubinadamu wa hali ya juu.

Mfano katika kufanya naye kazi nilishirikiana naye kuhusu suala la ukombozi wa Afrika, alionyesha uvumilivu wa hali ya juu kusikiliza na kupatanisha vyama vya wapigania uhuru ili viweze kutimiza lengo la kupigania uhuru wa wananchi wao.

MTANZANIA Jumapili: Unadhani Taifa linapungukiwa nini kutokuwapo Baba wa Taifa?

MALECELA: Hapana, ngoja niwaambie nyie kizazi cha sasa, ninawasihi nyie kizazi kipya msiangalie hivyo, msiangalie kwamba mmepungukiwa nini.

Kimantiki kama Taifa hatujapungukiwa kitu chochote, kama kile tulichokuja nacho mpaka tukawa na Baba wa Taifa na pia kuondoka kwake duniani ndio wajibu wa sisi sote kufahamu kuwa chochote kinachozaliwa kitakufa.

Jambo hili litukumbushe kwamba wakati tukiwa tunaishi tujue mambo mema ambayo yatasaidia na wengine.

Mwalimu Nyerere alijitahidi kutuachia mema ya kutusaidia, hivyo hatuwezi kusema kwamba kuondoka kwake sisi kama taifa tumepungukiwa, kwa sababu yale yote mema ameyaacha na sisi kazi yetu ni kuyajenga ili yawe bora zaidi yatusaidie kutupeleke mbele.

Kamwe Watanzania tusiwe tunafikiria habari ya kupungukiwa, tuliachiwa urithi na Baba wa Taifa, inabidi utupeleke mbele kwa mbele.

MTANZANIA Jumapili: Unakitathmini vipi kiwango cha ubinafsi wa Watanzania, kati ya utawala wa Mwalimu Nyerere na tawala zilizofuata?

MALECELA: Ukitaka kuangalia hili suala vizuri anza na kiwango cha binafsi cha binadamu mwenyewe. Kwa kweli kiwango cha ubinafsi cha binadamu kipo na mahali ambapo kiwango hiki kimeruhusiwa kukua, kwa kweli kimekua sana.

Lazima niseme kiwango cha ubinafsi hakina huruma kwa sababu kila siku kinasema mimi, kwa hiyo unakuta mtu ni bilionea wa kutupwa, lakini bado anatafuta fedha.

Ubinafsi kila siku najaribu kujenga mawazo ya kuutetea na ndiyo sababu katika dunia tangu enzi na enzi vita zimekuwa kila siku kati ya wenye nacho na wasio nacho.

Tabia ya ubinafsi inawasukuma watu wapende mali ili wengine wakose na hili suala la ubinafsi kama taifa linapaswa kuangaliwa.

Sisi Tanzania, tukitaka kuusema ule ukweli ni kwamba Watanzania hawana ubinafsi uliokithiri.

Watanzania mara nyingi wana ile tabia ya kumfikiria jirani yake, tazama watu wa Kenya, hatuwezi kuwalinganisha na Watanzania, ndiyo maana Mwalimu aliweka falsafa ya ujamaa na kujitegemea.

Naweza kusema kuwa, Watanzania kwa ujumla hawana ule moyo wa ubinafsi wa hali ya juu kufikia kiwango cha mtu mmoja kutomjali mwenzake anayeteseka.

MTANZANIA Jumapili: Kumekuwapo na matukio mbalimbali ya ufisadi, je, tathmini yako ni ipi katika maisha ya Watanzania juu ya pengo la walionacho na wasionacho?

MALECELA: Nina hakika na ninawaomba Watanzania wenzangu tuwe tunaliangalia kwa mapana zaidi. Ukiangalia kwa kifupi unaweza ukasema tuna watu watano au sita ambao ni mabilionea, wengine masikini wa kutupwa.

Sawa hayo yapo, lakini hatujafika mahali pa kusema kwamba Tanzania tuna tofauti kubwa kati ya walionacho na wasionacho.

Watu wenye kipato kikubwa kwa hapa nchini unaweza ukawahesabu, hapa Dar es Salaam unaweza ukawahesabu, lakini je, ukienda Uganda au Kenya unaweza ukawahesabu?

Sasa tathmini hii inabidi ituonyeshe kwamba sisi Watanzania tuna wajibu wa kupoza ubinafsi, ingawa ni vigumu kuutuliza ukatulia, bali kuwapo mkakati wa kuuzuia.

Kwa sababu hata ufisadi ndio ngazi ya juu ya ubinafsi, yaani mtu kuwa na dhamira ya dhati ya kupata fedha kwa gharama yoyote.

MTANZANIA Jumapili: Unauzungumziaje utawala wa Rais Dk. John Magufuli kwa kuufananisha na wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere?

MALECELA: Haya ni mawazo yangu binafsi, jamani tusilinganishe watu, kumlinganisha Rais Dk. Magufuli na Mwalimu Nyerere ni kosa kubwa, Nyerere alikuwa Nyerere na Magufuli ni Magufuli.

Rais Magufuli tumwangalie kwa mambo anayoyafanya ambayo naweza kusema mema mengi kayafanya na anaendelea kuyafanya, lakini siku akishaondoka kwenye utawala sisi tutakaa na kuhesabu aliyoyafanya.

Tena tutaanza kwa kuhesabu aliyofanya Nyerere, Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Kwa mantiki hiyo, tuangalie vitu walivyofanya, lakini kumlinganisha Magufuli na Mwalimu au kumlinganisha Magufuli na Kikwete hayo ni makosa makubwa sana na hali hii tunaleta uadui tu ambao hauna maana yoyote.

Mwanafalsa mmoja aliyeitwa Ibin Batuta alisema siku tukiondoka msitutafute kwenye makaburi yaliyopakwa chokaa, bali mtutafute kwenye mioyo ya watu.

Na kweli hali hii tunaiona kwa Hayati Baba wa Taifa kwamba bado yupo kwenye mioyo ya Watanzania, anaweza kuendelea kuishi kwa kizazi hiki na kijacho.

MTANZANIA Jumapili: Unaizungumziaje hali ya kisiasa na demokrasia ndani ya nchi?

MALECELA: (kicheko)…Kwanza sijui nitakuwa najikweza, lakini niseme mbele ya Mungu sijikwezi.

Mimi ndiye niliyekuwa Waziri Mkuu wakati vinaanzishwa, mimi ndiye niliyekuwa Waziri Mkuu niliyepeleka muswada bungeni sheria ya kuanzisha vyama vingi, ndiye niliyepeleka mapendekezo ya kwamba vyama vingi vikianzishwa vitakuwaje, kwa maana ya mfumo wa kuvisajili na kadhalika.

Kwa hiyo naweza kusema kwamba Tanzania bado ni taifa la kidemokrasia, ndiyo maana usajili wa vyama vya siasa uko wazi muda wote.

Wakati ule vyama vilivyoandikishwa kwa msajili ni 19, lakini sasa hivi vipo vichache kwa uhalisia wa utendaji kazi.

Demokrasia ya vyama vingi bado ipo na inasimamiwa na sheria za nchi. Vyama vingi vitaondoka, lakini vitajiondoa vyenyewe kwa njaa kwa sababu vimejigeuza moto wa mabua.

MTANZANIA Jumapili: Maono ya Mwalimu Nyerere juu ya wanasiasa wanaonunuliwa ambao aliwaita ‘malaya’, unazungumziaje maono hayo na mwenendo wa viongozi wa kisiasa wa upinzani kujiunga CCM?

MALECELA: Hilo kwanza utanisamehe sana, sisi nyakati zile tukisema juu ya watu kununuliwa tulikuwa tunamaanisha wakoloni walivyokuwa wanawanunua watu wetu na hili ni kweli, lakini kwa kusema kwamba sasa hivi wanasiasa wa upinzani wananunuliwa si kweli.

Hawa wanaoondoka upinzani na kurejea CCM wanarudi nyumbani kwa sababu kisiasa ndiko walikozaliwa, huko waliishi kama wana wapotevu, ambao walikwenda huko wakakosa chakula, mwisho wa siku wakaanza kula hadi chakula cha nguruwe, sasa wameona bora warudi nyumbani wale chakula cha watumishi wa baba yake.

MTANZANIA Jumapili: Baba wa Taifa alikuwa na maono ya kujenga uchumi wa kujitegemea, alianza kwenye viwanda vilivyojengwa chini ya misingi ya Azimio la Arusha, baadaye viwanda hivyo vilikufa, tatizo gani lilitokea?

MALECELA: Mara nyingine vijana muwe mnafanya utafiti kidogo, huko nyuma tulijenga viwanda vingi na vikubwa barani Afrika.

Kwanini vilikufa? Viwanda hivi vilikufa kwa sababu ya menejimenti, hapo sasa tunaweza kulaumiwa kwamba tulikuwa tunajenga viwanda pasipo kuangalia mbele kwamba vitaendeshwa na akina nani, kwa hiyo naweza kusema tulikosa watu sahihi wa kuviendesha. Lakini kwa sasa tunaweza tukaviendesha kwa sababu kizazi kipya kina uelewa mpana zaidi wa masuala ya menejimenti, naamini kinaweza kufanikiwa katika uchumi wa viwanda.

MTANZANIA Jumapili: Unapolitazama andiko la Azimio la Arusha kwa sasa, unadhani kuna hitilafu ya maono yake na mwelekeo wa Tanzania tunayoihitaji sasa?

MALECELA: Swali hilo usiniulize mimi, swali hilo jiulizeni ninyi kizazi kipya kwa sababu kizazi kipya mna vitu vyenu mnataka kufanya, je, mkiangalia azimio na kuliboresha.

MTANZANIA Jumapili: Kwanini lilitokea Azimio la Zanzibar?

MALECELA: (kicheko)…Azimio la Zanzibar ni kitu kirahisi sana, kwamba tuliposema watu wasipangishe majumba na kadhalika, tukajikuta mfano Kariakoo, Buguruni, Manzese, watu wana vijumba vya mbavu za mbwa, sasa hivi kweli nao unataka wasipangishe? Tukasema hapana, tuliona bora tuboreshe hicho tulichotengeneza nyuma, ndiyo Azimio la Zanzibar, lilikuwa ni kama maboresho ya maamuzi ya nyuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles