28 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

MAKONGORO NYERERE: JEURI YA WAKAZI WA ARUSHA SITAISAHAU MAISHANI

Mwandishi wa makala haya Evans Magege (kulia), akiwa katika mahojiano maalumu na Makongoro Nyerere
Mwandishi wa makala haya Evans Magege (kulia), akiwa katika mahojiano maalumu na Makongoro Nyerere

NA EVANS MAGEGE


 

JINA Makongoro Nyerere si geni miongoni mwa wafuatiliaji wa siasa za nchi hii. Kufahamika kwa jina hilo kulianza miaka 22 iliyopita wakati alipoingia rasmi kwenye duru ya siasa za ushindani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

Makongoro ambaye ni mtoto wa tano wa familia ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kwa sasa anatumikia cheo cha kisiasa katika nafasi ya uenyekiti wa wabunge wanaoiwakilisha nchi ndani ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).

MTANZANIA Jumapili limefanya mahojiano na mwanasiasa huyo wiki hii na kuzungumza mambo mbalimbali ya kisiasa, mwenendo wa nchi na mshikamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ujumla.

MTANZANIA Jumapili: Baada ya mchakato wa kumpata mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, umekuwa kimya sana. Nini kimekusibu?

Makongoro: Okay! ..Kwanza mimi si mkimya isipokuwa huwa napenda kuzungumza pale ambapo huwa panahitajika kuzungumza na mambo ambayo yanahitajika kuzungumzwa.

Wakati wa mchakato wa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni jambo la kawaida kabisa na ni busara ya kawaida kwamba unapoomba jambo,  hata kama ni masikini uko barabarani, yule anayewafahamisha watu wengi kwamba yeye ni masikini anaomba ana uwezekano wa kila siku kukusanya zaidi kuliko yule ambaye haelezi kuwa yeye ni masikini na nia yake anaomba.

Sasa kwenye kugombea udiwani, ubunge na urais inavyofikia msimu inabidi upigepige kelele za kutosha ili watu wahusika wajue. Kwa hiyo kwa wakati ule niliongezeka kusikika, ilikuwa ndiyo wakati wake na kulikuwa hamna namna nyingine zaidi ya kujaribu kusikika.

Kwa sasa nipo kimya kwa sababu msimu wa kugombea urais ndani ya CCM umekwisha na nchi yetu tayari ina Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa bahati nzuri kabisa ametoka  CCM.

Hata hivyo, baada ya kushindwa kupata nafasi ya kupewa ridhaa na chama, nilirejea kwenye kazi yangu ya ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki kuiwakilisha nchi yangu. Kwa hiyo siri ya ukimya inategemea tu tafsiri yake kama unataka nisiwe mkimya kama nataka kugombea urais utaratibu huo sina kwa sababu Rais tumeshampata kwa maana hiyo basi mimi ni mkimya lakini kwa upande mwingine huku naongea sana  na mara moja moja tunaonekana kwenye  vyombo vya habari tukiwa tunafanya kazi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika chombo kinachoitwa Bunge.

MTANZANIA Jumapili: Ushindani wa kumpata mwakilishi wa CCM wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi ulikuwa mkubwa sana na ukizingatia idadi ya wagombea nayo ilivunja rekodi kwa wingi wa watu waliojitokeza kutangaza nia, wewe ukiwa miongoni mwao. Ulijifunza nini katika mchakato ule?

Makongoro: Kwanza nilichojifunza ni kwamba, nikilinganisha na vyama vingine katika kumpata mgombea wao, sikumbuki vizuri kuhusu ACT –Wazalendo, lakini kwa vyama vingine ambavyo nimevifuatilia nadhani mfumo wa CCM wa kupata wagombea wake ulikuwa wa kidemokrasia zaidi.

Lakini nikilinganisha na upatikanaji wa mgombea wa urais ndani ya CCM na nyakati zilizopita kidogo safari hii kulikuwa kuna ukiukwaji wa taratibu kuliko safari nyingine zote huko nyuma.

Sasa pamoja na hayo makosa ya kiufundi ambayo yalikuwapo bado naweza kusema kwamba CCM utaratibu wake bado unaeleweka na wa kidemokrasia zaidi. Yako makosa ya kiufundi ambayo yalifanyika yakafanya hali isiwe nzuri kama safari nyingine ambapo tulifanya zoezi lile….Eh! Kuna watu ambao walikiuka taratibu za CCM.

Katiba ya CCM kwa mfano inasema utakapofika wakati wa uchaguzi inaelekeza mambo kadhaa lakini kimsingi inaelekea kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (CC) ndiyo itatangaza tarehe rasmi ya zoezi hilo kuanza, lakini kuna watu walianza zoezi hilo kabla, sasa ukitoka kwenye katiba, kanuni zinadai watu wanaoanza kabla ya mchakato lazima wachukuliwe hatua, walianza kabla hawakuchukuliwa hatua yoyote sasa baada ya hapo ukafika muda wale ambao tulitii na kuheshimu taratibu za chama tukaingia kuanza mbio pamoja na wale ambao walikwisha kuanza kabla yetu.

Tukaingia nao halafu mwisho bila hata ya kuitwa kuhojiwa, ilipokuja kuteuliwa watu wa kuingia tano bora katika wale tano bora …wote hatukuitwa sawa mimi silalamiki lakini nachosema hili ni tatizo la kiufundi …Ingawa wote hatukuitwa lakini palikuwapo mle wajumbe ambao walikuwa wamevunja utaratibu.

Sasa huo ni uongozi mbaya sana wa ngazi ya juu ya chama chetu. Walau kama unaheshimu nafasi zetu, kutokutumia madaraka vibaya ni pamoja na kuona kwamba kuna watu ambao hawakuvunja utaratibu.

Sasa wewe hata kama usiwaite waje kujieleza hapa wakati mnafanya maamuzi, walau mimi mwenyewe nihakikishe wale ambao hawakufuata utaratibu hawafiki hata kwenye tano bora.

MTANZANIA Jumapili: Mwaka mmoja nyuma kabla ya pazia la kuusaka urais kufunguliwa na chama, kuna makada sita  walipewa onyo la kutojishughulisha na siasa kwa miezi 12, inakuwaje useme uongozi haukufanya lolote?

Makongoro: Hivi kulikuwa kuna watu waliopewa hukumu? Hapana ..eh! kulikuwa na wazo kama hilo lakini hakuna aliyepewa hukumu, labda unikumbushe …ninachokikumbuka kulikuwa kuna shughuli hiyo inataka kufanyika lakini haikufanyika na kila mtu aliachiwa.

Najua waliitwa na wakajieleza lakini hakuna kitu kilichofanywa, sasa hapa CCM imeonyesha ghafla kubadilika na kuingiwa na tabia ya uvunjaji wa taratibu zake na kanuni zake na maadili.

Wale waliitwa tu  najuwa kulikuwa na mapendekezo ya kufanya lakini waliitwa tu…mapendekezo yalitoka na wakaonekana wanahatia lakini hakuna kitu ambacho walifanyiwa.

Sasa kwa safari hii nilijifunza sababu za kufanya hivyo ni nini hasa kwa kuomba kazi pasipo kufuata utaratibu.Yaani mtu anaomba kazi kinyume na utaratibu na ni kazi ya uongozi wa nchi yetu na chama chetu, unamuachaje na ili iweje?

Kwa hiyo nasema huo ni mfano mmoja palikuwapo na hivyo vikosa vya kiufundi lakini sasa hivi sina ninacholalamika, mchakato tulimaliza na nchi yetu imeishapata Rais na hatimaye Rais huyu ndiye mwenyekiti wa chama chetu.

MTANZANIA Jumapili: Sehemu kubwa ya hotuba zako ulizozitoa kwa wanachama wakati unatafuta wadhamini zilijipambanua katika sura ya kupambana na ufisadi. Na Rais aliyepo madarakani sasa Dk. John Magufuli amekuwa katika mtazamo huo huo na tayari dhamira yake imeonyesha msingi wa kuinyosha nchi. Unauzungumziaje mwenendo wa utawala wa Awamu ya Tano?

Makongoro: (1)Bado ni mapema  lakini angali ni mapem naweza kusema kwa uhakika kabisa dalili zote kuanzia asubuhi hii ya mapema  zinaonyesha kwamba Rais aliyepo madarakani  anachukizwa  na tabia ya watendaji wa umma kutokuwa waadilifu, anachukizwa sana na hilo.

(2)Rais aliyepo madarakani  anachukizwa na tabia za makusudi za uvunjaji wa sheria zetu  hasa ya ukwepaji wa kulipa kodi.

Kwa ujumla Rais Dk. Magufuli ambaye tumempata kwa mwenendo wake na matendo yake anakerwa na ukweli wa jinsi ambavyo nchi yetu ni tajiri sana lakini wananchi wake ni masikini sana. Rais anakerwa na umasikini uliokithiri wa Watanzania .

Sasa tuliomba wengi na inawezekana katika wale tulioomba labda kuna mmoja anayeweza kufanya kazi nzuri zaidi ya bwana mkubwa au katika wale hawakuomba  kabisa wangeliweza kufanya kazi nzuri kuliko bwana mkubwa lakini kwa sasa hivi simfahamu Mtanzania  ambaye anaweza kufanya kazi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  vizuri kuliko Dk. Magufuli.

Ah!..inawezekana yupo lakini kwa kweli taarifa naye sina na sijamsikia kwa hiyo kama yuko sehemu fulani anisamehe sana.

MTANZANIA Jumapili: Dhana ya utumbuaji majipu ambayo Rais Dk. Magufuli ameshikilia kama nyenzo ya kuinyosha nchi unaizungumziaje?

Makongoro:  Kama nilivyokujibu kwenye swali lako la hapo nyuma kidogo kama tuliwekeana utaratibu wa kufuata na ukawa wazi  lakini mtu hutaki kuufuata Rais atakuacha achaje na kwa ajili gani akuache?. Tukubali ukweli maana utaratibu tulijiwekea sisi wenyewe lazima tuuheshimu.

MTANZANIA Jumapili: Rais Dk. Magufuli katika kofia yake ya uongozi wa CCM ameanza kuonyesha dalili ya mabadiliko makubwa, ikiwamo uamuzi wa hivi karibuni wa kupunguza idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kutoka wajumbe 388 hadi wajumbe 158. Unayazungumziaje mabadiliko hayo?

Makongoro:  Mabadiliko yanayofanyika katika chama yana taratibu zake. Kwa hiyo mabadiliko haya yaliyokwishakufanyika hadi hivi sasa, mimi si mjumbe wa vikao hivi lakini yamepita kwenye vikao husika ambapo idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu imepungua, taarifa nilizonazo hadi sasa hata wajumbe wa Kamati Kuu imepungua.

Na pale ambapo mkutano haupo, mkutano mkuu huwa umekasimu madaraka yake kwa Halmashauri Kuu ya Mkutano Mkuu wa CCM.

Sasa kwanza ni mabadiliko ambayo binafsi nayaunga mkono kwa moyo wangu wote. Yameletwa kwenye chombo husika, chombo husika kikasikia na kikaafiki yafanyike kama ambavyo mabadiliko hayo yalivyoletwa kwenye chombo hicho hicho na chombo hicho kikaafiki idadi ya wajumbe ikaongezeka.

Haya nayaafiki kwa sababu yamelengwa katika kupunguza gharama za vikao vya chama. Hapa inaonekana kumepunguzwa wajumbe 230. Unapowaita hawa nchi nzima kuja kwenye Halmashauri Kuu kuja Dar es Salaam au Dodoma gharama yake leo imepungua  kupita wajumbe waliopunguzwa 230. Kwa mlengo huo kwamba kinacholengwa  ni kupunguza gharama hiyo nakubaliana nayo.

Pia ukiangalia wenzetu China wana wananchi bilioni 1.3 au 1.4 na wana chama cha Kikomunist China. Kamati Kuu ya China inaundwa na watu ambao hawafiki hata tisa. Sasa kama nchi ina watu zaidi ya bilioni moja ina wajumbe wa kamati kuu ambao hawazidi tisa, hivi Tanzania kuwa na wajumbe wa Kamati Kuu  wachache, nasikia walikuwa takribani 36, wajumbe 26 wanazidi hata platuni ya kijeshi.

Ukiangalia kwa udogo tulionao si muhimu kuwa na idadi hiyo ya wajumbe, tupe watu wachache waadilifu ili watupe mwongozo , sera tutazijadili kwenye taratibu za chama na pale ambapo tutaona hazifai tutawaambia, eh!..kuliko kuwa na watu wengi sana na hakuna haja ya kufananisha Kamati Kuu na Halimashauri Kuu kama vikao vya mkutano wa hadhara.

Kwa hiyo nasema haya ni mawazo yangu na mimi mjumbe,  binafsi nayaunga mkono na pia naweka akiba kama kuna mwingine anaweza kuwa na mawazo tofauti na mimi.

MTANZANIA Jumapili: Muda wa kutumikia Bunge la Afrika Mashariki unaelekea kukoma miezi michache ijayo, vipi una mpango wa kugombea tena?

Makongoro: Ndiyo. ..(kicheko) Nina mpango wa kugombea tena. Bunge la Afrika Mashariki, bunge moja linadumu kwa muda wa miaka mitano na tangu tuingie kwenye Bunge hilo mwaka 2012  huu ni mwaka wa tano. Bunge la Afrika Mashariki kwa mwaka mmoja linakaa mara sita vikao vya wiki mbili mbili ambavyo huwa vinatanguliwa na kamati za Bunge,  baada ya hapo ni kwenda kufuatilia yale yaliyopitishwa na baada ya kipindi hicho zinaanza tena kamati za Bunge.

Kwa mwaka huu wa tano Bunge letu limeishakaa mara tatu  na sasa linakwenda kukaa vikao vitatu vya mwisho, hapo ndio itakuwa basi tena, Bunge hili la Tatua la Afrika Mashariki . Kwahiyo ndani ya siku 10 zijazo tutakutana Kampala (Uganda) kwa muda wa wiki mbili baada ya hapo tutapumzika kwa wiki tatu tutakuwa tumemaliza kikao cha Kampala ambacho kwa mwaka huu kitakuwa cha nne na kikao cha tano tutakutana Kigali, Rwanda Machi.

Baada ya hicho, Mei tutakutana Arusha na hicho ndio kikao cha mwisho ambacho kitamalizika wiki ya kwanza Juni  na hapo Bunge hilo litakuwa limekoma.

Kwa mujibu wa taratibu mbunge atagombea kwa vipindi viwili, kwamba baada ya kumaliza muhula wa kwanza una haki na ruhusa ya kugombea muhula mwingine lakini kama umeishamaliza vipindi viwili huruhusiwi ugombee kipindi cha tatu.

Sasa hivi tupo jumla ya wabunge tisa tunaoiwakilisha nchi katika Bunge la Afrika Mashariki na katika hao wabunge tisa ni Abdulah Mwinyi  yeye ndio anamaliza muda wake wa kipindi cha pili kwa hiyo taratibu hazimruhusu kugombea tena. Kwa kweli alikuwa ni mbunge mzuri sana, umri wake unaruhusu na uwezo wake ni mzuri sana lakini taratibu hazimruhusu.

Wabunge wanane tuliobakia taratibu zinaturuhusu wote na kwa taarifa nilizonazo wote nane tunataka kugombea tena nafasi hiyo. Ninaiheshimu sana hiyo kazi na pia naipenda  na ninawaheshimu Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  maana ndiyo waliochaguliwa na Watanzania na sehemu ya majukumu yao kuchagua wawakilishi wa nchi ndani ya Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MTANZANIA Jumapili: Ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utumishi wako ndani ya Bunge la Afrikia Mashariki ni mambo gani makubwa ambayo umeyasimamia wewe binafsi au ndani ya timu nzima ya wabunge wanaoiwakilisha nchi?.

Makongoro: Okay! Kazi ya mbunge wa Bunge lolote ni kutunga sheria na katika hiyo kazi ya kwanza tumehakikisha kwamba sheria zinazopitishwa hazidhuru masilahi ya Tanzania kama mwanachama wa EAC.

Kazi ya pili ya mbunge ni kuhoji na kupitisha bajeti na kwa bunge hili sisi ndio tulikuwa tunahoji na kupitisha bajeti ya EAC.

Kazi ya tatu ni kwenda kuangalia au kukagua yaliyopitishwa. Pia tumewawakilisha mawazo ya wananchi katika Bunge hilo. Unajua Bunge la EAC ndiyo chombo pekee cha kisiasa katika vyombo ambavyo vimeundwa na jumuiya hii mpya ya EAC.

MTANZANIA Jumapili: Ndani ya Bunge la Afrika Mashariki suala la mgogoro wa Burundi mmelichukuliaje na nini jitihada zenu katika utatuzi wa mgogoro huo?

Makongoro: Kwanza mgogoro ule sisi  unatusikitisha na kwa taarifa yako katika kamati za Bunge la EALA ipo kamati inahusiana na masuala ya utatuzi wa migogoro na bahati nzuri mwenyekiti wake ni Mtanzania  Abdullah Mwinyi.  Na kwa mujibu wa mkataba uliounda upya jumuiya mpya ya EAC ni jukumu letu kuuliza kwanini mgogoro umetokea. Na sehemu ya mkataba huo inasema ni kuhakikisha wananchi wa EAC wanaishi kwa amani na utulivu.

Na mapendekezo  yaliyopendekeza yalipelekwa kwa wahusika ambao ni mkutano wa marais, kabla au baada ya mapendekezo yenyewe maraisi wamekwisha amaua kwamba mgogoro ule utasimamiwa na Rais Yower Museveni ambaye yeye alimteua Rais Benjamin Mkapa kusimamia yale mazungumzo.

MTANZANIA Jumapili: Kumekuwa na mnyukano mkali wa kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki, hali ambayo imewahi kutoa tafsiri ya mvutano kama si mgogoro kati ya Tanzania na Kenya. Vipi hali hiyo ikoje ndani ya Bunge EALA, hususani uhusiano wa wabunge wa Kenya na Tanzania, pia Kenya na Uganda?

Makongoro: Hakuna mvutano wowote wa kiuchumi, Jumuiya ya EAC iliyoundwa mwanzo  ilikuwa ina mashirika yake ambayo ilikuwa inaajiri wana EAC wote  na yalikuwa yanatoa huduma kwa wana- EAC wote. Sasa hivi jumuiya hiyo haipo tena, lakini tumeunda upya kwa kujaribu kutoa fursa kwa wananchi kushirikiana katika maeneo mbalimbali  kwa muhimu wafanye biashara.

Fursa ni za kila mtu kuzichangamkia na si za upendeleo wa nchi fulani kwa mfano Kenya kwa sasa ndio nchi yenye kampuni nyingi ndani ya jumuiya kuliko nchi zote na katika nchi zote Kenya ina kampuni nyingi zaidi Tanzania kuliko nchi nyingine ndani ya jumuiya nadhani kwa sababu ya nchi yetu kuwa na utulivu, sasa huu si mvutano .

Kenya wapo hadi Sudan Kusini lakini hawajisikii vizuri kama wanapokuwa Tanzania, Rwanda na Uganda.

Kwa hiyo hakuna mvutano na kwa sisi wabunge tunaelewana  na tunapendana sana.

MTANZANIA Jumapili: Tanzania imeamua kumuunga mkono mgombea wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Balozi Amina Mohammed ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya. Je, nini tafsiri ya uamuzi wa Tanzania kutosa azimio la SADC la kumuunga mkono mgombea wa kanda yao Dk. Pelomoni Venson-Moitoi wa Botswana, na badala yake itamuunga mkono mgombea wa kanda ya EAC?

Makongoro: Swali ni zuri sana ila kwa bahati mbaya limeulizwa kwa mtu asiyehusika. Naomba nikiri kwamba ni mapenzi ya Serikali yangu ya Tanzania  kwamba tukimchagua Balozi Amina Mohammed kwangu mimi ni heri. Tanzania wakiamua kumuunga mkono yule wa SADC kwangu ni heri pia.

Lakini kama ndiyo nia ya Serikali ya Tanzania kuweka umoja wa EAC basi mimi naomba niunge mkono msimamo huo ila naomba nikiri wazi kuwa swali hili liko nje ya uwezo wangu.

MTANZANIA Jumapili: Tunaelekea kuadhimisha siku ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, je una jambo lolote la kuzungumzia kuelekea kwenye maadhimisho hayo?

Makongoro: Kwanza kabisa ifahamike kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika kwa lazima. Viongozi wa kisiasa Bara walikuwa na mahusiano na viongozi wa kisiasa Zanzibar tangu Bara haijapata uhuru.

Mzee Nyerere na wenzake huku akina mzee Rashid Kawawa, Mzee Abeid Karume na wenzake kule  akina Marehemu Thabit Kombo hawa walikuwa ni marafiki na walikuwa wanaelewana na walikuwa wakishauriwa sana na Mwalimu Nyerere kwamba wasipate uhuru wao kwa kumwaga damu, wapige kura.

Kwa hiyo Zanzibar kulipigwa kura, halafu ile kura kukaonekana kwamba hamna mshindi, Mwalimu Nyerere alikwenda Zanzibar kabla hata Tanganyika haijapata uhuru akaenda akawaambia anayewanyanyasa ni Sultani ambaye ni Mwarabu na ana wenzake Waarabu.

Akawaambia kuwa wengine wote wanatakiwa wafanye kitu chochote  lakini kosa walilolifanya kuna wengine miongoni mwao wajiangalia kwamba wao ni wahindi, wengine Washirazi na wengine Waafrika.

Hivyo, akawashauri kwamba wakitaka kura yao ikae vizuri waunganishe nguvu  kwa maana ya kuunganisha vyama vyao na waende kwenye uchaguzi ilikuwa rahisi kweli.

Mwingereza ndiye aliyekuwa anasimamia  lakini ilionekana wazi alikuwa anamtaka Sultani kwa hiyo akaweka mazingira ya kumbeba Sultani.

Walimwambia Mwalimu Nyerere hayo mambo yake kutaka kupiga kura yanawasumbua kidogo lakini yeye aliwatia moyo kwamba waende kupiga kura.

Kwa hiyo hatua iliyofuata walimficha Mwalimu Nyerere, wakaingia wenyewe kimya kimya, wakapanga mikakati na siku moja alfajiri  wakamwambia Mwalimu kwamba sisi huku tumeishapindua nchi. Walifanya hivyo kwa sababu walimuona kama anawashika jezi.

Ukiangalia historia ya Zanzibar ilisaidia Mwalimu Nyerere kukaa madarakani muda mrefu, kwa sababu alikuja kusaidia kurudisha uchaguzi Zanzibar  kwa sababu viongozi waliopita  waliingia madarakani wakiwa wanaona uchaguzi ni kitu kibaya sana.

Mwalimu Nyerere alijitahidi polepole kuwafanya Wazanzibari wakubali tena kuamini uchaguzi lakini waliuchukia kabisa kwa mtazamo kwamba Sultani alikuwa anautumia kukandamiza haki yao.

Sasa basi wao walioingia na kuchukua nchi walikuwa ni raia wa kawaida walikuwa na mawe, marungu, mapanga na wakavamia kituo cha polisi wakachukua silaha chache na ndizo hizo walitumia kwa haraka haraka pamoja na sapoti ya Wananchi, wakamuondoa Sultani ambaye walijua kabisa ana msaada wa Waingereza.

Kwa hiyo kwa haraka kabisa baada ya kupindua walitaka Muungano. Hofu yao wale viongozi wa mapinduzi kwamba wangekaa peke yao  Sultani angejipanga upya na kurudi… nasikia mpaka leo yuko Uingereza.

Hata hivyo uharaka wao wa kutaka Muungano ulicheleweshwa kidogo na Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuandaa maandishi ya makubaliano ya kuungana, Mwalimu alifanya hivyo kwa kuogopa maneno huko tuendako na hata leo ukikaa utayasikia sikia maneno ya watu wanafiki, ambao hawakujihusisha chochote na ule muungano lakini wanataka kukorofisha watu.

Kwa ujumla Mapinduzi hayo yalikuwa ni muhimu sana na yalihitajika kufanya hivyo ili kukomboa maisha ya Wazanzibari. Na mapinduzi hayo ndiyo yaliyosababisha Muungano ukawa wa lazima na Muungano wetu hautakufa kwa sababu ndio unaolinda mapinduzi ya Zanzibar na Wazanzibari wengi wanalijua hilo ingawa kuna maneno maneno na hiyo inatokana na haki tuliyonayo katika Katiba yetu, yani uhuru wa kuongea.

MTANZANIA Jumapili: Katika Maisha yako ni jambo gani lililowahi kukutokea na hautalisahau maishani?

Makongoro: Wengi huwa wanazungumzia ajali, mimi sizungumzi ajali, jambo ambalo liliwahi kunitokea na sitalisahau maishani mwangu  kwangu mimi ilikuwa furaha ni kuingia bungeni nikiwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa mara ya kwanza hilo siwezi kulisahau.

Kwanini siwezi kulisahau kwamba nilichaguliwa na wananchi wa Arusha kwa hiyo kila ninapopata nafasi huwa nasema hilo.

Licha ya kwamba nilikuwa chama cha upinzani lakini wananchi waliniona mimi wakatumia haki yao kunichagua kuwa mwakilishi wao bungeni. Kusema ukweli siku nilipoapishwa nilisema hii ni jeuri ya wananchi wa Arusha mjini maana bila wao mimi nisingeingia katika jengo lile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles