26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

RAIS MAGUFULI KAUSEMA UKWELI ULIO MCHUNGU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu wakitoka kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Omumwani mkoani Kagera.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu wakitoka kwenye ukaguzi wa shule ya Sekondari Omumwani mkoani Kagera.

Na ASKOFU METHOD KILAINI,


 

WATU wa Mkoa wa Kagera tangu tupate Rais mpya Dk. John Magufuli, walikuwa wana shauku kubwa ya kutembelewa na Rais wao hasa baada ya kukumbwa na tetemeko la ardhi Septemba 10, 2016.

Ujio wa Rais Januari mosi mwaka huu, ni tofauti na ujio wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kwa sababu Waziri Mkuu alifika wakati wa msiba na mazishi ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko hilo.

Ujio wa Rais Magufuli unabeba sura ya kuanua matanga na kurudia maisha ya kawaida. Si kwamba marehemu wamefufuka au madhara yameisha bali ni kukubali hali na kuendelea mbele.

Kagera kwa namna ya pekee Bukoba mjini na ukanda wa Magharibi mwa Ziwa Victoria (Nyanza), ulipata tetemeko kubwa la ardhi la kipimo cha Richa 5.7, watu takribani 17 walifariki dunia na zaidi ya 400 kujeruhiwa, nyumba zaidi ya 2,000 ziliporomoka na zaidi ya majengo 14,000 yakapata nyufa hatarishi.

Wakazi zaidi ya 126,000 walikuwa katika hali mbaya sana ya kukosa makazi. Hili lilikuwa ni janga kubwa lililoharibu si tu miundombinu bali kukatiza mipango ya maendeleo ya watu wengi.

Mbaya zaidi tetemeko lilikuja wakati Kagera ilikuwa na shida ya ukame, migomba ilikuwa imenyauka na maharage na mahindi yaliyopandwa Agosti mwaka jana kama ilivyo kawaida yalikauka.

Mito mingi ilikauka na watu hasa wa vijijini wakapata shida ya maji na kutumia muda mwingi kutafuta maji. Hata kile kidogo ambacho mtu angeliweza kutumia kukarabati nyumba zilizoathirika zilitumika kununua chakula.

Kusema kweli hali ya Kagera ilikuwa mbaya. Mtu ulipotembelea vijijini kulikuwa ni vilio na mahangaiko. Mwingereza husema kwamba shida zikija hazidondoki kidogo kidogo bali zinamwagika na ni hivyo ilikuwa Kagera.

Kutokana na tukio hilo, ilimlazimu Rais kukatisha safari ya kwenda Zambia kuhudhuria hafla ya kumwapisha Rais mpya wa nchi hiyo na alimwagiza Waziri  Mkuu kesho yake kuwatembelea waathirika na kuwaonyesha mshikamano, mawaziri wa wizara husika walifika eneo la tukio pamoja na timu nzima ya kamati ya Taifa ya maafa.

Mbunge wa Muleba Kusini, Charles Mwijage, akishirikiana na wadau wengine chini ya udhamini wa Waziri Mkuu kama mgeni rasmi walihamasisha na kupata fedha kiasi kusaidia maafa hayo.

Kamati ya Maafa ya Mkoa iliundwa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu, kuratibu shughuli na misaada ya maafa.  Kamati hiyo ilihusisha viongozi wote wa Serikali kutoka wilaya zote zilizoathirika.

Kamati ilifanya tathmini ya madhara ya maafa kutambua watu waliofariki na kujeruhiwa, miundombinu iliyoharibika, nyumba zilizoporomoka na kuharibika.

Kamati hiyo ya maafa ilifanya kazi kubwa sana na kwa nguvu na uwezo wao wote. Mkuu wa mkoa alilivalia njuga aliweza kuwapokea wote walioleta misaada.

Mwitikio wa michango na misaada haukuwa mkubwa kama ilivyotegemewa. Kutoka mwanzo haikuwa wazi nani ategemee nini au nani asaidie nini.

Michango yote ya maafa ilibidi ipitie kwa Kamati ya Maafa na ni kamati hiyo ilikuwa na jukumu la kusambaza mahema, chakula, vifaa vya ujenzi na fedha.

Hii ilikuwa ni kudhibiti uwezekano wa walaghai wa kutumia maafa hayo kujinufaisha. Wakati huo huo kwa Serikali kuchukua jukumu lote kulipunguza kasi ya juhudi za watu binafsi ikaonekana ni kazi na wajibu wa  Serikali kushughulikia maafa hayo.

Zilibakia kampuni kubwa na taasisi zilizotoa msaada na kuweza kutangazwa katika vyombo vya habari kama sehemu ya kujitangaza.

Ilipendeza kwamba Rais alichagua Januari mosi kutembelea Kagera ili kuleta mwelekeo mpya, kuleta mwanzo mpya na matumaini mapya yenye uhalisia.

Ilipendeza kwamba aliamua kwanza kuiweka Kagera mikononi mwa Mungu kwa kuanza na ibada ya mwaka mpya.

Tetemeko, ukame, mnyauko wa migomba na magonjwa haviko katika mamlaka ya binadamu bali ni kumsihi Mungu atuepushe na majanga hayo au kutupa nguvu za kuyakabili.

Kanisani alitoa pole na kuahidi mshikamano, umoja na kujali, aliomba viongozi wa dini zote washiriki kumwomba Mungu na kuliombea Taifa letu na kumwombea yeye atimize vema majukumu yake.

Alipokwenda Kata ya Ishozi na kesho yake shule za sekondari za Mumwani na Ihungo, licha ya kutoa pole alielezea wazi kwamba mwisho wa siku kila mmoja atabeba msalaba wake mwenyewe. Bila shaka kwa wengi huo ulikuwa ukweli mchungu. Lakini husemwa ‘afadhali ukweli mchungu kuliko uongo mtamu.’ Ni kweli kabisa uwezekano wa Serikali kujenga nyumba za watu haupo na haiwezekani.

Ni afadhali kujua mapema na kujipanga kuliko kusubiri kujengewa miaka nenda rudi.

Kuna maeneo hapa nchini watu walipata majanga na kuahidiwa kujengewa lakini hadi leo bado hawajajengewa. Hii haimanishi kwamba pakiwapo uwezo Serikali isiwajengee nyumba watu wenye shida pia isiwape matumaini ya uongo.

Kama nilivyoeleza awali kuwa Rais alikuja kuanua matanga na kutuambia tuvue nguo za msiba au nguo za kaniki na kutoka nje na kuanza kazi ya kujenga upya Kagera yetu.

Je; tumejifunza nini katika mkasa huu wa tetemeko la Kagera. Nilijikuta katikati ya haya maafa, kwanza hata mimi nyumba ninamokaa ilipata nyufa hatarishi tukapaswa kuhama, nilitembea sehemu nyingi kuwatazama waathirika, wengine walinitoa machozi.

Nashukuru nilialikwa na kuhudhuria vikao kadhaa vya Kamati ya Mkoa ya Maafa na kuona juhudi zao kubwa.

Kupitia janga hili nitoe maoni yangu kama ifuatavyo:-

Mosi; Ni kuwashukuru wote waliotoa msaada, Serikali na kamati zake hasa mashirika yaliyojituma kusaidia watu.

Pili; likitokea tetemeko au maafa mengine Serikali isihodhi madaraka yote yaani kuhamasisha, kupokea misaada na kuigawa. Hili linatumia muda mwingi wa watendaji wa Serikali katika ngazi zote,  inatumia rasilimali nyingi katika kuwahusisha wote ndani ya uongozi na inadumaza juhudi nyingine za maendeleo na kuleta malalamiko yasiyo ya lazima.

Wafadhili wengi hasa kutoka nje wanataka walete misaada na kuigawa wenyewe ili watoaji wa misaada hiyo waone misaada yao imetumikaje moja kwa moja bila urasimu. Kuna wafadhili kadhaa walisita shauri ya hilo.

Tatu; Jukumu la Serikali liwe lile la kuweka mazingira mazuri ya kufikisha misaada na kudhibiti walaghai, kushughulikia miundombinu na taasisi za Serikali pamoja na kusaidia raia pale ambapo wana uwezo. Kama michango ni kwa ajili ya miundombinu na taasisi za Serikali ieleweke toka mwanzo kwa hao wanaoitoa. Msimamo aliouweka Rais Dk. Magufuli alipotembelea Bukoba kwamba ni ruksa mtu kupeleka misaada anapotaka ni mzuri sana na ilibidi uwepo toka mwanzo. Wengi wakihusika wanafika mbali hata kama wanaleta kidogo kidogo.

Nne; Kwa kuhamasisha na kutoa msaada wiki mbili za kwanza ni muhimu sana. Baada ya miezi shida huwa butu na kuonekana kama kitu cha kawaida. Hata waathirika huridhika na hali ya shida na kukata tamaa.

Kagera imeanua matanga ya tetemeko lakini bado iko katika hali mbaya ya kimaisha kutokana na majanga mengi yaliyoikumba na mengi yakiwa nje ya uwezo wao. Tunamshukuru Rais Magufuli katika matembezi yake ameleta tumaini kwa watu kwa kuwaahidi mazingira mazuri ya maendeleo kwa sababu tokea wakati wa vita ya Kagera mkoa huo ulikuwa umetengwa.

Ameahidi kodi za zao la kahawa kupunguzwa kwa sababu kwa sasa wale wasioweza kuvusha kimagendo kahawa na kuiuza Uganda wameng’oa mibuni. Wanajiuliza kwanini Uganda nchi isiyo na bandari wapate bei nzuri kuliko Tanzania na soko la dunia ni moja? Ameahidi kuleta meli kubwa itakayofungua milango ya Kagera dunia nzima ili watu na mazao yafike kirahisi soko la nje ya Bukoba.

Pia ameahidi kukarabati shule za Serikali zilizoharibiwa na tetemeko na nyingine kama Ihungo na Nyakato kuzijenga upya na kuboresha Mumwani na Rugambwa. Hiyo ni zawadi kubwa kwa Wana-Kagera. Kwa sababu inajulikana kwamba ahadi zake ni za uhakika tumaini la watu ni kubwa.

Ndugu zangu wa Kagera tuamke tena, tufanye kazi kwa juhudi na nguvu zote na kwa msaada wa Mungu tutatoka na kutembea tena. Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Kagera.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles